Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amewataka waajiri nchini kuzingatia viwango vya kima cha chini cha mshahara vilivyowekwa na Serikali ili kuhakikisha wafanyakazi katika sekta binafsi wanapata stahiki zao kwa mujibu wa sheria hatua itakayosaidia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Mhe. Sangu ametoa wito huo Juni 25, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 67 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) uliofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam ambapo amesema ulipaji wa mishahara inayokidhi viwango vya chini vilivyowekwa kisheria ni wajibu wa kila mwajiri ambapo inaongeza motisha kwa wafanyakazi na kuimarisha uzalishaji katika maeneo ya kazi.
Waziri Sangu amesema ili sekta ya kazi kuendelea kuwa na mafanikio ni jambo muhimu kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuhakikisha nguvu kazi ya wafanyakazi inalindwa na wakati huo huo kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara yanabaki rafiki, shindani na endelevu.
Amesema Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waajiri watakaobainika kukiuka masharti ya mishahara kwa kuwalipa wafanyakazi kiwango cha chini ya kile kilichoainishwa katika sheria na kanuni za kazi.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo












