CCM yatoa neno ziara ya Rais Samia Kenya

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepongeza hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa.

Chama kimesema hatua zinazochukuliwa na Rais Samia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, inayoagiza kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine na kufungua fursa kupitia diplomasia ya uchumi.

Hayo yalielezwa jijini hapa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alipozungumza kuhusu ziara ya siku mbili ya Rais Samia nchini Kenya ambako kwa kushirikiana na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta, waliweka maazimio mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha uhusiano na kuchochea fursa za kibiashara kwa nchi zao.

“Sera ya mambo ya nje ya Tanzania ni kuendeleza diplomasia ya kiuchumi baada ya kupata mafanikio makubwa ya kujitangaza, kuweka bayana misimamo yake hatimaye kufahamika kimataifa kuanzia awamu ya kwanza hadi ya sita.

“Chama kinaridhishwa na juhudi za kisera zitokanazo na ufanisi upeo na maarifa aliyonayo Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan katika medani za kimataifa ukiwa ni utekelezaji wa sera ya nje na kuimarisha sera ya Diplomasia ya Uchumi,” alisema Shaka.

Alisema ziara ya Rais Samia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika masuala ya kidipomasia.

Shaka alisema ilani hiyo katika kifungu cha 132 (a ) inaeleza; “Chama kitaielekeza Serikali kuboresha utekelezaji wa mipango ya kuimarisha diplomasia ya siasa ya kimkakati kwa ajili ya kulinda amani, uhuru, maslahi ya taifa na kuimarisha ujirani mwema na kushiriki kikamilifu kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kukuza uhusiano wa kiuchumi na mataifa, jumuiya za kikanda na taasisi zingine za kimataifa.”

Kwa mujibu wa Shaka, Chama pia kimempongeza Rais Samia kwa kuendeleza msisitizo kwa kuyapa msukumo masuala ya ulinzi na usalama na mapambano dhidi Covid-19.

Post a Comment

0 Comments