Rais Mwinyi aishukuru Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kwa ushirikiano mzuri

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuboresha maisha ya kaya maskini, urasimishaji ardhi, biashara na utoaji wa fursa za ajira kwa uwiano uliokubalika kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na vikao vya mashirikiano vya Mawaziri kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, anaripoti James K.Mwanamyoto (OR-Utumishi) Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora leo katika Ikulu ya Zanzibar wakati ujumbe huo ulioongozwa na Mhe. Mchengerwa ulipoenda kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa baadhi ya majukumu ya taasisi zake.

Mhe. Rais Mwinyi ameyasema hayo Mei 11, 2021 Ikulu ya Zanzibar alipokuwa akizungumza na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ulioongozwa na Waziri mwenye dhamana ya Ofisi hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Mhe. Rais Mwinyi amesema ni matarajio yake kuona ushirikiano huo ukiendelezwa na kuondoa changamoto za kiutendaji zilizopo ili wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar wanufaike na masuala yote yanayohusu MKURABITA, fursa za ajira na ruzuku inayotolewa na TASAF.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akitoa neno la utangulizi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati Waziri Mchengerwa alipoenda kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya baadhi ya majukumu ya taasisi zake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akizungumza na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora leo Ikulu ya Zanzibar.

Kuhusiana na fursa za ajira kwa Wazanzibari, Rais Mwinyi amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa utashi wake katika kusisitiza uzingatiaji wa makubaliano ya uwiano wa Ajira kwa taasisi za Muungano ambapo katika vikao vya Bunge ilikubalika kuwa Tanzania Bara iwe na asilimia 79% na Tanzania Zanzibar asilimia 21% ya nafasi za Ajira kila zinapotangazwa.

Akizungumzia suala la kujengeana uwezo kwenye mchakato wa ajira, Mhe. Rais amesema ni muhimu Zanzibar ikajifunza kutoka Bara kwa kuwa na kanzidata ya waombaji wa ajira ili fursa za ajira zinapotolewa iwe rahisi kuwapata watu sahihi wanaohitajika.

Akizungumiza melekezo ya Mhe. Rais Mwinyi, Mhe. Mchengerwa amesema, Ofisi yake imejipanga kuhakikisha suala la kubadilishana uzoefu kwa Watumishi wa Umma wa pande zote mbili litafanyiwa kazi.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, atashirikiana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Utumishi wa Umma Zanzibar kuhakikisha Watumishi wa Umma wanapata mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tutajipanga vizuri kuhakikisha wataalam wa vyuo vya Utumishi wa Umma Tanzania Bara na Zanzibar wanakutana na kupanga namna bora ya kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata mafunzo yenye tija katika utumishi wao.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amemueleza Rais Mwinyi kuwa, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 112.87 kwa upande wa Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu.

Amefafanua kuwa, kiasi hicho kitatumika katika kutekeleza miradi ya kutoa ajira za muda, ikiwa ni pamoja na kuondoa mapungufu yaliyopo katika sekta ya elimu, afya na maji na kuongeza kuwa wazee wataendelea kupata ruzuku kama kawaida kwani hawana uwezo wa kushiriki katika miradi ya kutoa ajira za muda.

Naye Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amesema urasimishaji wa biashara kwa upande wa Zanzibar umefanyika katika maeneo 8 ambapo wameweza kuwafikia wananchi kwa kutoa mafunzo na kusajili biashara zao ambapo watu 2926 wamepata leseni za biashara na utambulisho wa mlipa kodi ambao umewawezesha kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Ladislaus Mwamanga akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Ikulu ya Zanzibar.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Ikulu ya Zanzibar.Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Ikulu ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Omar Mchengerwa leo katika Ikulu ya Zanzibar wakati Waziri Mchengewa pamoja na ujumbe wake walipoenda kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa baadhi ya majukumu ya taasisi zake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Wa kwanza kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Omar Mchengerwa na wa kwanza kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman.

Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi amesema Ofisi yake iliyoko Zanzibar itahakikisha inatoa elimu kwa wahitimu ili waweze kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kuomba ajira zinazotangazwa.

Ameongeza kuwa, Ofisi yake hivi sasa imeanzisha dirisha litakalowawezesha waombaji wa fursa za ajira kupata taarifa za ajira, kuwasilisha maombi popote walipo na kupata mrejesho wa maombi yao.

Rais Mwinyi amekutana na ujumbe kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora uliolenga kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa upande wa Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news