Serikali yatangaza 'Operesheni Punguza Mahabusu'

Na Abubakari Akida,MOHA

Katika kukabiliana na wimbi la mahabusu katika magereza mbalimbali nchini na kuwapunguzia mzigo Jeshi la Magereza Serikali imeanzisha Operesheni Maalumu ijulikanayo kwa jina la “Operesheni Punguza Mahabusu” ambayo inafanyika nchi nzima.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo wakati akizungumza katika kikao kilichohusisha Wafungwa na Mahabusu wanawake katika Gereza Ruanda jijini Mbeya ambapo pia alitoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo magodoro, Taulo za Kike, Miswaki na sabuni kwa wafungwa na mahabusu hao.

“Miongoni mwa mambo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani hapendi kuyaona ni mrundikano na muongezeko wa watu katika majela hasa wanawake kwa kuwa anaamini wanawake ndio wanaojenga nchi na jamii wakishirikiana na wanaume, kikubwa tunaichukua changamoto na tayari tunaanzisha operesheni maalumu itakayoitwa Operesheni Punguza Mahabusu,”amesema.

Ameongeza pia tayari serikali imeanza kuyaendea mbio baadhi ya mambo ikiwemo changamoto ya kuchelewa kwa upelelezi, utolewaji dhamana kwa kesi ndogondogo ambazo ndio zinaongoza kwa kujaza mahabusu wengi katika magereza hali inayopelekea magereza kuhemewa na mzigo mkubwa wa kulisha mahabusu.

Akizungumzia hali ya msongamano katika Gereza hilo Mkuu wa Gereza la Wanawake, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Rehema Mwailunga alikiri kuwepo kwa msongamano ambao unasababishwa na mkoa wa Mbeya kuwa na Mahakama ya kanda.

“Mheshimiwa Naibu Waziri,nashauri ili kupunguza msongamano nashauri tuone umuhimu wa kujenga bweni la wafungwa na mahabusu wa kike sambamba na hili lililopo hapa lakini nakiri msongamano huu unasababishwa na kuwepo kwa mahakama ya Kanda hapa Mbeya hivyo mahabusu na wafungwa wengi kutoka magereza ya wilaya wanakuja kusikiliza kesi na rufaa zao hapa,"amesema SSP Rehema

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news