WATAALAMU WA NDANI WAPONGEZWA NA VIONGOZI WASTAAFU WA KITAIFA KWA KUSIMAMIA UJENZI WA MRADI WA KUFUA UMEME WA JULIUS NYERERE

Na James K. Mwanamyoto, Rufiji

Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu Waheshimiwa Marais na Mawaziri Wakuu wamewapongeza wataalamu wa ndani kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) ambao ujenzi wake umefikia asilimia hamsini na nne (54%).
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wa wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Pongezi hizo wamezitoa walipoutembelea mradi huo kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi na kutoa ushauri utakaoboresha ukamilishaji wa ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kitaifa unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Ali Hassan Mwinyi amesema amefurahishwa na namna wataalamu wa kitanzania walivyoweza kusimamia mradi huo kwa ustadi mkubwa hivyo amewapongeza kwa kutumia vema taaluma yao kusimamia ujenzi wa Mradi huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza waliohusika kuchora mchoro wa mradi, wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo na kwa kipekee amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuupokea mradi na kuuendeleza.

Aidha, Mhe. Kikwete amempongeza Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa kutafuta fedha na kuanza ujenzi wa mradi huo ili kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mhe. Kikwete amesema, ndoto ya Baba wa Taifa ilikuwa ni kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme, lenye shughuli ya utalii, litakalopunguza mafuriko sehemu ya chini ya mto Rufiji na kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kitakacholisha takribani watu milioni ishirini, hivyo ametoa wito kwa wadau wa kilimo waanze kujipanga kutumia fursa ya kilimo cha umwagiliaji.
Mwonekano wa mendeleo ya ujenzi wa eneo mojawapo la Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Malecela amesema, watanzania wanapaswa kujivuna kwa kutekeleza mradi huo kwa fedha zao wenyewe na kuongeza kuwa, watanzania wajisikie fahari kwani mradi huo unasimamiwa na wazawa ambao wameonesha uzalendo kwa taifa kwa kusimamia vema ujenzi wake.

Mhe. Malecela amefafanua kuwa, tangu taifa lipate uhuru halijawahi kutekeleza mradi mkubwa kama huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere hivyo watanzania hawanabudi kujivunia mradi huo.

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Cleopa Msuya amempongeza Waziri wa Nishati Mhe. Medard Karemani na wataalamu wake wa kitanzania kwa kujitoa na kuwajibika kikamilifu katika usimamizi wa ujenzi wa mradi huo.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda ameipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi mzuri wa mradi huo mkubwa ambao ujenzi wake umefikia asilimia 54% na kutoa wito kwa watanzania kuhakikisha mradi huo unatumika vizuri ili kukamilisha ndoto ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Malecela akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Karemani amesema mradi ukikamilika nchi itakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wenye gharama nafuu hivyo ametoa wito kwa wenye nia ya kuwekeza kujitokeza na kuwekeza kwenye shughuli za kilimo, umwagiliaji na utalii.

Mhe. Kalemani amesisitiza kuwa, kupitia uzoefu wa usimamizi wa mradi huo watanzania tumejifunza kwamba hata miradi mingine itakayoanza kutekelezwa itasimamiwa na watanzania wenyewe kwani wataalamu wazawa wanao uwezo huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wote wanaosimamia miradi ya mikubwa ya kimkakati na mingine kuhakikisha ina kamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.
Waziri wa Nishati, Mhe. Medard Karemani akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.
Viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi za Umma mara baada ya kumaliza ziara yao ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Greyson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa ya kujionea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere unaojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kukamilisha mradi huo ifikapo mwakani ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi mingine ya kimkakati na kutoa wito kwa wasimamizi wa miradi kusimamia vizuri kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotumika na kuwaonya watakaokwamisha miradi kuwa watachukuliwa hatua stahiki.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Greyson Msigwa amewahakikishia watanzania kuwa, miradi yote mikubwa ya kimkakati itakamilika kwa wakati kama ambavyo Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria.

Ujenzi wa Mradi huo wa Kufua Umeme kwa Nguvu za Maji wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Haydropower Project) unatarajia kukamilika tarehe 14 Juni, 2022 na utakuwa na uwezo wa kufua umeme wa Megawati 2115.

Post a Comment

0 Comments