Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa nchini (TALGWU) chataka wanachama wapewe huduma bora

Na Yusuph Mussa, Korogwe

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa nchini (TALGWU) kimewataka viongozi ngazi ya mkoa, wilaya na matawi kuwahudumia wanachama ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo stahili zao.

Na kwa kutoa huduma nzuri, itawafanya wanachama hao wasiwakimbie na kujiunga na vyama vingine kama baadhi yao walivyokimbia na kwenda kwenye vyama vingine ikiwemo Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE).
Zoezi la kuhesabu kura kwa viongozi waliochaguliwa kwenye Mkutano Mkuu wa TALGWU Mkoa wa Tanga.

Akifungua Mkutano Mkuu wa chama hicho Mkoa wa Tanga Julai 5, mwaka huu uliofanyika wilayani Korogwe, Mweka Hazina wa TALGWU Taifa, Siston Mizengo, alisema viongozi wa chama hicho wana dhima katika kutoa huduma bora, na kuwarudisha waliokimbia.

"Jambo lingine la msingi ambalo ningependa wajumbe wa mkutano huu mkuu mlizingatie ni kutoa huduma bora kwa wanachama kadri iwezekanavyo kwa kuzingatia hivi sasa watumishi wengi wanakiamini chama, na ule wasiwasi mkubwa wa TUGHE na TANNA umeanza kutoweka. Hivyo tuendelee kujiimarisha na kupiga kazi ili ikiwezekana watumishi wote waliohama warudi na wale waliopo wasihamie vyama vingine,"amesema Mizengo.

Mizengo alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwenye chama hicho ikiwemo viongozi wa mkoa wa Tanga kufanya ziara ya kuwatembelea wanachama wilayani na kusikiliza kero zao, bado watumishi wengi wa Serikali hasa wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) wapo nje ya chama. Hivyo wakati umefika wa kuwavuta walio wengi ili kujiunga na TALGWU.
Masanduku ya kura kwa waliogombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Mkutano Mkuu wa TALGWU Mkoa wa Tanga.

"Ila niwaombe kuendelea kuongeza nguvu katika zoezi la usajili, kwani bado kuna kundi kubwa la wafanyakazi ambao bado hawajajiunga na chama. Endapo tutafanikiwa kusajili wafanyakazi wote, basi TALGWU itakuwa na nguvu kubwa ya kuwasemea wanachama wetu, na ndipo uimara wa chama unapozaliwa,"amesema Mizengo.

Katika mkutano huo ambao ulikwenda sambamba na Uchaguzi Mkuu wa viongozi wa TALGWU Mkoa wa Tanga, Mizengo aliwataka wajumbe kuwachagua viongozi bora ambao watawaongoza kwa miaka mitano, huku akiwataka wale ambao kura hazitatosha waendelee kukipigania chama.

Katika uchaguzi huo, TALGWU Mkoa wa Tanga ilipata Mwenyekiti mpya Dkt. Clarence Mangowi ambaye ni daktari wa binadamu na yupo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Lakini pia Salome Nyangusi amechaguliwa kuwa Mweka Hazina wa Kamati ya Ushauri ya Wafanyakazi Wanawake (TALGWU) Mkoa wa Tanga. Nyangusi ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Idara ya Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news