DC Jokate akasirika, aagiza viongozi wa chuo wawekwe chini ya ulinzi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mheshimiwa Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam ameonekana kukasirishwa na kuagiza kuwekwa chini ya ulinzi kwa viongozi wa Chuo cha Lubando Training College.

Ni chuo kilichopo Mtaa wa Butiama Kata ya Mtoni Kijichi baada ya kubaini chuo hicho kinaendeshwa kinyume cha sheria nchini.
Mheshimiwa Jokate ametoa agizo hilo wakati alipoungana na wataalamu katika ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ambapo aliambatana pia na Mkurugenzi wa Uthibiti, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Dkt. Joefrey Oleke.

DC Jokate baada ya kufanya mahojiano na Mkuu wa chuo hicho alibaini kuwa, kwa muda sasa chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo bila kupata usajili, pamoja na kutoa mafunzo kwenye mazingira yasiyo rasmi.

"Hamna kitu kibaya kama kufanya utapeli, halafu ukadhani hutagundulika, Serikali ina macho kila sehemu, NACTE kaeni hapa na Polisi, lazima tupate 'information' (taarifa), chuo hakijasajiliwa.

"Lakini hata mandhari yake haistahili, kuna watu wanatoa huduma ambazo kiuhalisia hawastahili kutoa, tushirikiane katika ufuatiliaji, hawa wachukuliwe hatua kali huu ni utapeli,"ameagiza Mkuu huyo wa wilaya.

Naye Dkt. Jofrey Oleke amechukua uamuzi wa kusitisha shughuli zote zinazoendelea katika chuo hicho.

Dkt.Oleke ameeleza kuwa,taratibu nyingine za kisheria zitafuatwa huku akisema kwa ukaguzi uliofanyika chuo hicho hakitambuliki na VETA wala Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)

Post a Comment

0 Comments