IGP Sirro: Kukata viungo vya binadamu ni ushamba, sheria itatumika kuwanyoosha

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema yoyote atakayekutwa amekata kiungo cha binadamu mwenzake kwa lengo la kujipatia utajiri atamshughulikia.

Ni kwa mujibu wa sheria akisema kufanya hivyo ni unyama na ushamba na haikubaliki katika jamii iliyostaharabika ya Kitanzania.
IGP Sirro ameyasema hayo leo Novemba 19, 2021 wakati wa ziara yake ya kukagua jengo la ofisi za Jeshi la Polisi zinazojengwa wilayani Lushoto mkoani Tanga.

IGP Sirro ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya tukio la kufukuliwa kwa maiti ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi,
Heri Shehe Kijangwa (45) aliyezikwa Julai 4,2020 na kukatwa mguu na watu waliokamatwa na kukiri kufanya hivyo katika Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga.

Amesema kuwa, Jeshi la Polisi halina huruma na muhalifu wanaofanya matukio hayo kwani huo ni ushamba wakudanganywa na waganga wa kienyeji kuwa kupata utarijiri lazima ukate kiungo cha binadamu.

"Acheni kudanganywa na waganga wa kienyeji sababu mganga atakupaje utajiri wakati yeye mwenyewe ni masikini? Nyumba anayokaa haieleweki na wala hajasomesha watoto wake,"amesema Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi huku akisisitiza jeshi hilo lina timu ya kupambana na mauaji ya aina zote.

IGP Sirro amesema, mtu akipelekwa mahakamani kwa kosa hilo la kukata kiungo cha binadamu atanyongwa kwa kuwa mtu huyo ni mnyama, hivyo lazima ashughulikiwe.

"Suala la kukata viungo unategemea kuwa tajiri vilishapitwa na wakati halafu ni ushamba, unakata mtu kiungo maana yake anakufa tukikukamata adhabu yake ni kunyongwa," amesema IGP Sirro.

Amewaomba viongozi wa dini na wanasiasa kusaidia kutoa elimu kwa jamii ili waache na hizo imani za kishirikana.

Akizungumzia hali ya amani, IGP Sirro amesema kwa Lushoto hali ni shwari tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na ugaidi wa kutisha huku akisema waliokuwa wanajihusisha na ugaidi walikamatwa mlima Simba mkoani Tanga.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkaoni Tanga, Safia Jongo amesema kuwa Serikali imewapatia Shilingi Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo huku jeshi hilo kupitia mfuko wake wa tuzo na tozo imetoa Shilingi Milioni 160 japo fedha zilizokuwa zinahitaka kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo ni Shilingi Milioni 500.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro amehidi kutoa ushirikiano kuendeleza na ujenzi wa jengo hilo ambalo litakuwa na ofisi za utawala, kituo cha polisi na upande wa upelelezi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news