DUNIA SIYO YENYEWE:Majeshi alijazia, wao wakambwekea

NA LWAGA MWAMBADE (KiMPAB)

DUNIA siyo yenyewe, haya yanayotokea,

Huku silaha zenyewe, vita vinaendelea,

Kwingine wao wenyewe, maneno waelezea,

Hivi haki iko wapi?


Alitishia tishia, kule anaelekea,

Majeshi alijazia, wao wakambwekea,

Na yeye hakutulia, bali aliendelea,

Hivi haki iko wapi?


Vita kajitangazia, kule ameelekea,

Ni kama ajipigia, mwingine ajitetea,

Kule alikimbilia, kwa maneno wabwekea,

Hihi haki iko wapi?


Kama ukiangalia, jamaa alipotea,

Bomu amelikalia, kwingine aelekea,

Hali angeangalia, kwao singeegemea,

Hivi haki iko wapi?

 

Vita ukiangalia, mwingine yamwelemea,

Sasa analialia, kipigo anapokea,

Kule alikimbilia, kusema waendelea,

Hivi haki iko wapi?


Putin amepania, vile inaelekea,

Nani atamzuia, kile atekelezea?

Wababe wamwangalia, hali imewalemea,

Hivi haki iko wapi?

 

Mabomu ajipigia, kusema waendelea,

Nchi inaangamia, vikwazo waongezea,

Wapi watakoishia, mwenzao yamwelemea?

Hivi haki iko wapi?




Wababe nakutajia, duniani waelea,

Marekani na Russia, sote tunawapepea,

Kivita kuwavamia, hiyo haitatokea,

Hivi haki iko wapi?




Kama unawatania, watake kukomeshea,

Wewe utaangamia, ukome kuwachezea,

Huwezi kuwazuia, huna kwa kuegemea,

Hivi haki iko wapi?




Ukraine sikia, shari umejiletea,

Huko umekimbilia, Russia wambwekea,

Yeye anajipigia, hadi utapolegea,

Hivi haki iko wapi?




Hili ninaangalia, kama linaelekea,

Kyuba lilikoanzia, vita kutokezea,

Marekani nakwambia, walitaka kutokea,

Hivi haki iko wapi?




Wakubwa kiwasikia, kile wanaelezea,

Hawataki kusikia, adui akisogea,

NATO ikiwafikia, hawataki kutokea,

Hivi haki iko wapi?




Hao wangeangalia, kiwezacho kutokea,

Singesisitizia, Ukraine kupokea,

Huyo wangemuambia, kwao asije sogea,

Hivi haki iko wapi?




Ona sasa analia, yale yanayotokea,

Nani atalipizia, Russia kuitokea?

Kelele tunasikia, ndizo wanaibwekea,

Hivi haki iko wapi?




Tutateseka dunia, haya yanayotokea,

Hakuna kuingilia, kivita kutatokea,

Tutazidi kusikia, kubweka kunatokea,

Hivi haki iko wapi?




Ngumi tukiangalia, jukwaani zatokea,

Uzito wa mabondia, wale wanajitetea,

Huwa unafanania, si yanayoendelea,

Hivi haki iko wapi?




Heri tunawatakia, yale yanayotokea,

Muda wa kushambulia, usije kuendelea,

Maafa yakazidia, watu wengi kupotea,

Hivi haki iko wapi?




Lile lakuulizia, nini kitachotokea?

Vikwazo kuzidishia, Putin atapotea?

Marekani NATO pia, meno yameshapotea?

Hivi haki iko wapi?




Saddam nakumbukia, kipigo alipokea,

Kuwait kuvamia, wakubwa alichezea,

Naamini kwa Russia, hilo halitatokea,

Hivi haki iko wapi?




Habari metufikia, siyo ya kupendelea,

Kuna watu waumia, na wengine wapotea,

Taifa kubwa Russia, tuzidi kulibwekea,

Hivi haki iko wapi?



Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news