Wanufaika elimu ya matumizi sahihi ya mbolea watakiwa kuwa mabalozi

*TFRA yawapa wakulima mbinu kwa matokeo makubwa

MATILDA KASANGA NA NURU MWASAMPETA

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo amewataka viongozi na wana vikundi vya wakulima Mkoa wa Lindi kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya mbolea kwa kilimo chenye tija.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Dkt.Stephen Ngailo  akiwa katika shamba la Eva Alex Kachime ambaye ni Bibi shamba wa Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa aliyenufaika na uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea.

Dkt. Ngailo ametoa wito huo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kukagua mashamba ya mfano yaliyolenga kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea bora kwa wakati kwa shughuli za kilimo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Aidha, Dkt. Ngailo amewataka wakulima wa mazao ya mahindi kufuata kanuni zote za kilimo ikiwa ni pamoja na kuchagua shamba, kuandaa shamba kwa wakati, kupanda kwa kutumia mbolea sahihi ya kupandia na kwa wakati, kuweka mbolea ya kukuzia na kupalilia kwa wakati.
Mmoja wa mwanakikundi cha Jikomboe akiwa katika shamba la mfano katika eneo la Mbemba Chigugu wilayani Masasi. Nyuma ni mahindi yaliyopandwa kwa kutumia mbolea na mbele hayajatumia mbolea.

"Shamba likifuata kanuni zote za kilimo huwa na matokeo mazuri na hivyo kuongeza tija kwa mkulima na taifa kwa ujumla,"Dkt.Ngailo alisisitiza.

Dkt. Ngailo aliongeza kuwa, kufuatia kutokuwepo kwa matumizi ya mbolea kwa wakulima katika mikoa ya Lindi na Mtwara, mamlaka iliona ni vyema kufanya uhamasishaji kwa njia ya kuanzisha mashamba ya mfano ambayo vikundi vya wakulima vinashiriki kikamilifu kuanzia msimu wa kupanda mpaka msimu wa mavuno ili kujionea kila hatua ziavyokwenda na kupata ujuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (kushoto) akimsikiliza Swalehe Tendwa ( wa pili kulia) Bwana shamba kata ya Kitere alipofika kukagua maendeleo ya mashamba hayo.

Pamoja na kuanzisha mashamba ya mfano mamlaka imewawezesha wanakikundi mmoja mmoja ili kwenda kutumia kwenye mashamba yao binafsi ili wananchi wengine waweze kujifunza.

Amesema, wakulima wakihamasika kutumia mbolea suala la njaa litakuwa historia kwa mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Ruangwa.
Swalehe Tendwa ambaye ni Bwana shamba Kata ya Kitere akieleza jambo kuhusu kilimo cha mpunga kwa viongozi walioambatana na Mkurugenzi wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo (hayupo pichani) alipofanya ziara katika mashamba hayo kuona manufaa ya matumizi bora ya mbolea katika kilimo.

"Tutatokomeza njaa, lakini pia kipato cha mkulima mmoja mmoja kitaongezeka na kupunguza umaskini,"alikazia.

Aidha, Bibi shamba Eva Alex  Kachime aliishukuru mamlaka kwa kuanzisha mashamba ya mfano katika kata anayoisimamia na kueleza wakulima wamehamasika na kuona utofauti mkubwa kati ya shamba lililopandwa kwa mbolea na lisilotumia mbolea.
Wanakikundi wa jitegemee wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (hayupo pichani) aliyefika kukagua maendeleo ya mashamba katika eneo la Mnacho wilayani Ruangwa.

Amesema, tangu kuanza kwa uhamasishaji huo wakulima 51 wameweza kujifunza namna bora ya kutumia mbolea na kumi miongoni mwao walihamasika kutumia mbolea.

"Tuiombe Serikali iendelee kutoa hamasa kwa miaka mitatu mfululizo ili kuhamasisha wakulima wengi zaidi waweze kutumia mbolea na kuachana na kilimo bibi (kilimo cha kutotumia mbolea),"amesema.

Amesema, Kata ya Mnacho ni kata inayotegemewa kwa kuzalisha chakula kwa wingi hivyo uhamasishaji wa mbolea utaongeza tija zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo wa pili kulia akizungumza na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Lindi, Majid Myao alipofika ofisini kwake kuzungumzia maandalizi ya siku ya mkulima katika mkoa huo.

Kwa upande wake, Said Mnangona Afisa kilimo Kata ya Chigugu Masasi DC alieleza kuwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea imeongeza tija kwake na kwa wakulima wengine kwani katika heka moja na nusu aliyolima anatarajia kuvuna gunia 30 za mahindi tofauti na awali alipokuwa akivuna chini ya gunia nane za mahindi.

Mzee Rashid Mandumba mwanakikundi wa Jitegemee anasema huko awali alikuwa hatumii mbolea kulingana na desturi na mazoea na kukiri kuwa uhamasishaji wa matumizi ya mbolea umeleta tija kwake na jamii yake kwa ujumla.

Amesema, mbolea inawasaidia kulima eneo dogo lakini wanapata matokeo na kipato kikubwa kuliko kulima eneo kubwa bila mbolea na kuambulia hasara pamoja na kupoteza nguvu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akizungumza na kikundi cha wakulima cha Jitegemee katika Kata ya Mnacho alipofika kukagua maendeleo ya mashamba ya mfano na ya wakulima hao katika kuhamasisha matumizi ya mbolea katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi tarehe 10, 2022.

Ziara hii ni hatua ya maandalizi kuelekea siku ya mkulima yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea inayotarajia kufikia kilele mwezi Aprili 2022 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news