Waziri Balozi Dkt.Chana azikaribisha wizara,taasisi katika Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu, Balozi Dkt.Pindi Chana ameziagiza wizara, halmashauri na taasisi nyingine za umma kuendelea kuitumia Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuchapisha nyaraka muhimu za Serikali.
Mheshimiwa Dkt.Chana ameyabainisha hayo leo Machi 18,2022 baada ya kutembelea Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali iliyopo Keko jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na idara hiyo na kusikiliza changamoto zilizopo ili Serikali ione namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Amesema,lengo kuu la idara hiyo ni kutoa huduma za uchapaji kwa wakati, kwa kuzingatia ubora na kwa gharama nafuu.

Pia amesema, idara hiyo inaongozwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ambaye husimamia vitengo vya Udhibiti wa Ubora, Uzalishaji, Ufundi, Masoko na Maduka ya Vitabu ya Serikali ina umuhimu mkubwa nchini, hivyo kwa umuhimu huo taasisi hizo zinapaswa kuitumia kwa maslahi mapana ya Taifa.

Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ndiyo yenye jukumu la kuchapisha nyaraka mbalimbali za Serikali ikiwemo sheria mbalimbali na Gazeti la Serikali ambapo machapisho yake huyauza kupitia maduka ya Serikali (government shops).
Mheshimiwa Balozi Dkt.Chana amewashauri wafanyakazi wa idara hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa bidii, uaminifu na uzalendo wa hali ya juu kwa kuwa jukumu wanalotekeleza Serikali inalithamini na itaendelea kuwa nao karibu.

"Endeleeni na uzalendo wenu huu, licha ya uchache wenu nimeshuhudia namna ambavyo mnafanya kazi kubwa, tena kwa bidii. Hii ni hatua njema sana, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inathamini sana mchango wa wafanyakazi katika kulijenga Taifa letu, nanyi ni sehemu ya kundi hilo, tupo pamoja nanyi na kazi iendelee,"amesema.

"Nirejee tena wito wangu kwa wizara zote, halmashauri na taasisi nyingine za umma ziendelee kutumia idara hii kwa ajili ya kuchapisha nyaraka muhimu za Serikali. Hii idara ni tegemeo kubwa sana kwa Taifa letu, mfano tunapoelekea katika Sensa ya Watu na Makazi pamoja na Anuani za Makazi, idara hii inafanya kazi kubwa sana,"amesema Waziri Balozi Dkt.Chana.

Pia amewataka kuendelea kutumia zaidi malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa ajili ya uchapishaji na pale inapolazimika kwa kuona malighafi hizo hazipatikani ndipo utaratibu ufuatwe kwa ajili ya kuagiza nje.

"Tuendelee kuzitumia kwa wingi malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa ajili ya kufanikisha uchapaji, ninaamini malighafi hizo zinapatikana, na pale ambapo itaonekana hazipatikani, baada ya kutafiti kila mahali nchini, ndipo utaratibu ufuatwe kwa ajili ya kuagiza nje. Tukifanya hivyo, tutaendelea kukuza uchumi wetu na kuwainua wazalishaji waliopo hapa nchini kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla,"amesema Balozi Dkt.Chana.

Maktaba

Akiwa katika Maktaba ambayo pia inasimamia Duka la Nyaraka za Serikali, Waziri Balozi Dkt. Chana ameelezwa na Mpiga Chapa Msaidizi Mkuu, Bw. Alistid Wanyuke kuwa, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Serikali inapaswa kuona umuhimu wa kuanza kutunza nyaraka hizo kwa mfumo wa kidigitali na kuondoka katika analojia.
Mfumo ambao, Bw.Wanyuke amesema, ni hatari zaidi hususani katika kipindi hiki ambacho majanga ya moto yamezidi kuwa changamoto katika maeneo mengi.

"Ninaiomba Serikali itenge bajeti kidogo kwa ajili ya kufanikisha mfumo wa kuweka nyaraka za Serikali katika mfumo wa kidigitali na kuondoka huku kwenye analojia ambapo tunatunza kwa njia za kawada, itasaidia sana kukabiliana na changamoto za maafa mfano ya moto,"amesema.

Pia amesema kuwa, kwa sasa duka la nyaraka za Serikali lililokuwa katikati ya jiji la Dar es Salaam kwa sasa wanaweza kupata huduma hiyo katika Duka la Nyaraka za Serikali lililopo katika Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Keko jijini Dar es Salaam.

Waziri aguswa

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana amesema, wazo la kuingia katika mfumo wa kidigitali kwa ajili ya kutunza nyaraka za Serikali ni jambo muhimu na la msingi.

Amesema, wataangalia namna ya kushirikiana na wenzao wanaosimamia mfumo huo ili kuona namna ambavyo hilo litafanyiwa kazi.
Balozi Dkt.Chana ameelezwa kuwa,mfumo huo ukisimamiwa vizuri unaweza pia kuwa njia rahisi kwa wananchi kununua kupitia mtandao nyaraka hizo kadri wanavyozihitaji.

Kitengo cha Usanifu

Katika hatua nyingine, Mpiga Chapa Msaidizi Idara ya Usanifu, Bi.Catherine Joseph amemweleza Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana kuwa, wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi pamoja na vitendea kazi vya kisasa ili kuongeza ufanisi katika kazi.

"Mheshimiwa Waziri, changamoto yetu hapa ni upungufu wa wafanyakazi ambao unachangiwa na baadhi kustaafu au wengine kufariki. Vile vile tuna mahitaji ya vitendea kazi mfano printers za kisasa ambazo zikipatikana zitasaidia kuongeza ufanisi katika kazi,"amesema Bi.Joseph.
Hata hivyo, Waziri Balozi Dkt.Pindi Chana amesema kuwa, wamezipokea changamoto na maoni ya wafanyakazi katika idara hiyo na watazifanyia kazi hatua kwa hatua ili kuongeza ufanisi katika idara hiyo.

Post a Comment

0 Comments