Naibu Meya Manispaa ya Musoma asisitiza ufanisi Kituo cha Afya Bweri

NA FRESHA KINASA

NAIBU Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Mheshimiwa Haji Mtete amewataka Watumishi wa Kituo cha Afya cha Bweri kilichopo katika manispaa hiyo, kufanya kazi kwa weledi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa kituo hicho katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Kituo cha Afya Bweri na kuhudhuriwa pia na Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Afisa Ustawi wa Jamii, Kamati ya Afya Kata ya Bweri, Diwani wa kata hiyo, na Afisa Mtendaji wa kata ambapo kililenga kuwahimiza kuzingatia maadili katika utumishi wao.

Mheshimiwa Mtete amesema kuwa, yapo baadhi ya malalamiko yamekuwa yakitolewa na wananchi wakilalamikia huduma katika kituo hicho ikiwemo lugha zisizofaa ambazo hutolewa na baadhi ya watumishi kwa wagonjwa wanapofika kutibiwa kituoni hapo na kupelekea baadhi ya watu kutokwenda kutibiwa katika kituo hicho pindi wanapougua jambo ambalo halifai.

"Wapo wagonjwa wanakuja na kadi za CHF zilizobooreshwa, lakini wanaambiwa kadi zao hapa hazifanyi kazi. Serikali inatumia nguvu kubwa kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF kama kadi ya mgonjwa ina tatizo, umeigundua mwambie kwa lugha nzuri sio kumfokea. Tumieni lugha zinazofaa kwa wananchi, na pia uongozi wa kituo uwe haraka kutoa taarifa ngazi husika pale kunapokuwa na upungufu wa vifaa au jambo lolote badala ya kukaa kimya hadi wananchi wanaanza kufikisha malalamiko yao ngazi za juu wakati uongozi wa kituo umekaa kimya,"amesema Mheshimiwa Mtete.
"Kama mgonjwa amekuja kutibiwa kaandikiwa dawa ambayo haipo, basi aambiwe kwa lugha rafiki kusudi siku nyingine tena aje kupata huduma. Toeni huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya kazi, Serikali inaendelea kuongeza bajeti sekta ya afya ili wananchi waendelee kupata huduma bora mnapolalamikiwa kiasi kikubwa hamwatendei haki wananchi. Niwaombe zidini kufanya kazi kwa upendo na kujituma,"amesema Mheshimiwa Mtete.

Kwa upande wake Dkt.Magreth Shaku ambaye ni Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, alipongeza hatua za Naibu Meya kukaa pamoja na watumishi hao na kuwakumbusha wajibu wao, huku pia akiwasisitiza kuzingatia misingi yao ya kazi sambamba na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

"Niwasihi Watumishi fanyeni kazi kwa nidhamu na pia tusichafua image nzima ya halmashauri yetu, hivi karibuni tilifanya kikao tukakumbushana juu ya uwajibikaji,lakini bado. Mtumishi ukitoa kauli mbaya kwa mgonjwa lawama zinaelekezwa serikalini jambo ambalo halifai, toeni kauli njema kwa wagonjwa ili kusudi kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi juu yenu. Muwe na hofu ya Mungu mnapotekeleza majukumu yenu ili mtoe huduma bora,"amesema Dkt. Shaku.

Diwani wa Kata ya Bweri, Mheshimiwa Nickson Mwandala alibainisha kwamba, amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakilalamikia baadhi ya watumishi kufanya kazi kinyume cha taratibu.

"Haipendezi mgonjwa anapofika kutibiwa aondoke kwa manung'uniko, niwahimize sana ndugu zangu hakikisheni mnawatendea haki wananchi wanaofika kupata matibabu, haipendezi kituo kiwe na sifa mbaya lindeni heshima ya kituo hiki na mzidi kusifika kwa wema kwani wananchi wanawapima kwa kile mnachokifanya,"amesema Mheshimiwa Mwandalala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news