Elimu ya utunzaji mazingira, vyanzo vya maji Mara yapongezwa

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Kijiji cha Marasibora Kata ya Kisumwa Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara, wamepongeza hatua ya Chama cha Msalaba Mwekundu (Tanzania Red Cross Society)Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji katika maeneo yao.
Wameyasema hayo Aprili Mosi, 2022 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI Blog kijijini hapo mara baada ya kuelimishwa umuhimu wa kutunza mazingira na vyanzo vya maji kwa manufaa endelevu katika kuchochea shughuli za maendeleo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mathias Marwa amesema kuwa, elimu hiyo itasaidia kwa kiwango kikubwa wananchi kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti maeneo ya vyanzo kusudi visikauke kwa matumizi endelevu ya shughuli za maendeleo.

Neema Ogori amesema, awali hakuwa na ufahamu thabiti, kama kufanya shughuli za kilimo karibu na vyanzo vya maji kunachangia vyanzo kukauka. Ambapo kwa sasa elimu aliyoipata amesema atashiriki vyema katika kulinda vyanzo na kuwaelimisha wengine.
"Elimu hii iliyotolewa ina faida kubwa kwetu wananchi, tuna wajibu sasa wa kutunza mazingira ikiwemo kupanda miti katika maeneo yetu na kutofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya mto Mara na vyanzo vya maji,"amesema Fidellica Onyango.

Paul Julias ameomba elimu ya utunzaji wa mazingira iendelee kutolewa maeneo mbalimbali kusudi wananchi wazidi kufahamu kwa upana zaidi faida za utunzaji wa mazingira na uzingatiaji wa sheria za mazingira.
Abdulatif Rajab ni Afisa Maendeleo ya Jamii na pia ni Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara amewataka wananchi hao, kutofanya shughuli za kilimo maeneo ya vyanzo vya maji na pia wazingatie umbali wa mita 60 kufanya shughuli zao kutoka vyanzo vya maji.

Pia amewahimiza kuendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi wengine, huku akisisitiza kuwa shughuli za kibinadamu zinapaswa kufanywa kwa kusingatia utunzaji wa mazingira kwa ajili ya kulinda maisha ya viumbe hai.
Jacob Nyalusi ni Mratibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Mara amewataka wananchi hao kuchukua tahadhari ya kukabilina na majanga kabla hayajatokea kuliko kusubiria serikali kwa kuachana na tabia hatarishi ambazo zinaweza kusababisha majanga hayo.

Pia, Nyalusi amewahimiza kupunguza taharuki pindi majanga yanapotokea na kutafuta njia sahihi za kuyashughulikia sambamba na kuzingatia utaratibu wa utoaji taarifa katika mamlaka za Serikali kupitia vijiji,mitaa, kata na wilaya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news