Wanafunzi Kizumbi Sekondari iliyopo Shinyanga Mjini wajisaidia vichakani

NA DIRAMAKINI

UHABA na uchafu wa vyoo unahatarisha afya za wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kizumbi iliyopo Kata ya Kizumbi katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga.
Pia imebainishwa kuwa, wanafunzi 267 wa shule hiyo wapo katika hatari ya kuugua magonjwa ya tumbo, yakiwemo ya kuharisha kutokana na kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo, hali inayowalazimu baadhi yao kujisaidia ovyo vichakani.

Hali hiyo imetokea baada ya choo walichokuwa wanatumia kutitia na kuanguka, hali hiyo imepelekea kutumia vyoo chakavu ambavyo sio salama kwa mazingira ya ndani.

Wanafunzi wa shule hiyo wamewaeleza waandishi wa habari kuwa,hali ya ukosefu wa vyoo, inapelekea wao kuchelewa vipindi kutokana na foleni vyooni na wakati mwingine wanalazimika kujisaidia haja kubwa na ndogo vichakani, kitu ambacho ni vigumu wao kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Diwani anasemaje?

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kizumbi, Ruben Kitinya ameeleza kusikitishwa na kitendo cha viongozi kulikalia kimya suala hilo wakati wanalijua na wamefika shuleni hapo na kujionea hali halisi ilivyo.

"Mkuu wa wilaya na Mbunge walishafika na kuahidi kutengeneza, lakini mpaka sasa ni miezi kadhaa imepita hakuna kilichofanyika.

"Wanafunzi wanajisaidia hata kwenye vichaka kitu ambacho kinaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, nilishatoa taarifa kwa viongozi, lakini hawajalichukulia katika hali ya dharulr, naomba halmashauri pamoja na Serikali kulichukulia ni jambo la dharura kuwanusuru watoto wetu,"amesema Ruben.

Mjumbe mmoja ambaye ni mjumbe katika kamati ya shule hiyo ameeleza kuwa, mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia katika shule ni kichocheo kwa mwanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na kupata maarifa na ujuzi yatakayowasaidia katika maisha yao.

"Muda mwingi tunawaona wanafunzi wakizurura mitaani na kuomba kutumia vyoo vya watu waliojenga karibu na shule, kitu ambacho wanatumia muda mwingi katika kutafuta sehemu ya kujistiri, kuliko muda wa kukaa darasani,"amesema Mjumbe huo ambaye hakutaka jina lake kutajwa.

Hali halisi

Utafiti wa awali umebaini kuwepo kwa shule nyingi za msingi na sekondari ambazo hazina mazingira rafiki kwa wanafunzi, ikiwepo mifumo mizuri ya maji safi na taka, vyoo na vifaa vya usafi na sehemu ya kuhifadhia taulo za wasichana.

Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 622, ambao hutumia matundu manne tu, hiyo inamaana wanafunzi 84 hutumia tundu moja la choo.

Kwa mujibu wa Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2009, inaelekeza wasichana 20, watumie tundu moja la choo na wavulana 25, watumie tundu moja la choo.

Shule ya Kizumbi Sekondari inajumla ya wasichana 355, ambao hutumia matundu manne, na hili idadi hiyo ya wasichana ikidhi uwiano wa 1:20 inatakiwa wasichana hao wapate matundu ya 17, ambayo kwa sasa wana matundu manne.Kwa muktadha huo wanahitaji matundu kumi na tatu kukidhi mahitaji yote ya vyoo.

Idadi wavulana wa shule hiyo, wapo jumla 267, ambao ndio wahanga wakubwa wa changamoto ya kutokuwa na choo, na hivyo kuwalazimu kutumia vyoo chakavu vilivyokuwa vinatumika na wasichana miaka kadhaa nyuma, ambavyo navyo kiafya sio salama, na kuwalazimu kujisaidia vichakani.

Kulingana na Sera ya Elimu kwa upande wa wavulana tu katika shule hiyo wanapaswa kuwa na matundu ya vyoo kumi na tatu, ili kukidhi mahitaji yote ya wavulana shuleni hapo.

Kwa ujumla shule hiyo ina mapungu ya makubwa ya vyoo vya wanawake na inakabiliwa na changamoto ya kukosa vyoo vya wanaume na ni hatari zaidi, pale wanafunzi wanapojisaidia vichakani, hali iliyotufanya kufika shuleni hapo kujionea hali halisi ilivyo shuleni hapo.

"Mara kadhaa viongozi wamekuwa wakifika shuleni hapo na kuahidi kulipatia ufumbuzi na pindi wanapoondoka inabaki kama simulizi za bunuwazi," amesema Mjumbe mmoja wa kamati ya shule.

Kukosekana kwa vyoo vya wavulana katika sekondari hiyo inaweza kuhakisi hali halisi iliyopo katika shule mbalimbali mkoani humo, ambapo kuna shule zingine hazina vyoo kabisa, na zipo ambazo zina vyoo vichache ambavyo havikidhi mahitaji ya wanafunzi na kwenda kinyume na maelekezo ya Sera, na kuhatarisha afya za wanafunzi hasa wa kike ambao hupata hedhi kila mwezi.

Licha ya kutokuwepo kwa vyoo vya wavulana katika shule hiyo, lakini walimu bado wanalazimika kuwafundisha wanafunzi namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha afya za wanafunzi zinapewa kipaumbele.

DC

Mkuu wa Wilaya, Jasinta Mboneko baada ya waandishi kuomba kupata ufafanuzi kuhusiana na changamoto hiyo, aliwaelekeza kwenda kwa Afisa Elimu Sekondari ili atoe ufafanuzi kuhusu changamoto hiyo, kwa kuwa yeye hayupo ofisini amepatwa na msiba.

Aidha, jitihada za kumpata Afisa Elimu huyo kwa ajili ya ufafanuzi hazikufanikiwa, baada ya simu yake kuita bila mafanikio.Tunaendelea kufuatilia zaidi ili kufahamu mikakati iliyopo ya kuwanusuru watoto hao dhidi ya milipuko ya magonjwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news