Serikali yazindua Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka wa Kesi za Rushwa nchini

NA GODFREY NNKO

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Geophrey Mizengo Pinda (Mb) amezindua Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka wa Kesi za Rushwa ambao umetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 18 na 24 vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka, Sura ya 430 nchini.
Uzinduzi huo ameufanya kwa niaba ya waziri, Dkt.Damas Ndumbaro leo Mei 31, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo wadau mbalimbali wakiwemo mawakili wa Serikali na washirika wa maendeleo wameshiriki.

Mheshimiwa Geophrey Pinda amesema kuwa, Serikali kupitia wizara hiyo itashirikana kwa karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuhakikisha mfumo bora wa utoaji haki kwa wananchi inazidi kuimarika na kuleta ufanisi.
"Mahakama ya Tanzania imefanya mabadiliko makubwa sana, lakini haiwezi kuperfom kama nyie hamna vitendea kazi vya kusaidia kesi zao kwenda, kwa hiyo tumekubalina kwenye Mpango wa Serikali tunakuja na mageuzi makubwa na ya idara zote zinazosaidia katika huduma za utoaji haki.
"Lazima tuziimarishe moja wapo ni kitengo hiki cha DPP, kwa Mwanasheria Mkuu, lakini tumeenda mbali zaidi lazima tufanye kazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kule tuna play part kubwa sana tunazo magereza zetu zinatakiwa kuimarishwa,"amesema Mheshimiwa Geophrey Pinda na kuongeza,

"Na nyie Mahakama ile huduma ambayo mmeanza kutoa lazima iwe connected na nyie kwa maana ya Video Conference Programs ambazo zinaendelea upande wa Mahakama kwa kusikiliza kesi zikiwa mbali kwa hiyo lazima tujenge uwezo tushirikiane na idara ya polisi kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani tuweze kuhakikisha kwamba huduma zinaimarishwa maeneo yote ya utoaji haki, sasa hata tukijiimarisha sisi Wizara ya Katiba na Sheria tukawaacha wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani bado tunakuwa hatujafikia lile lengo ambalo ndilo lengo kuu kabisa,"amesema Mheshimiwa Pinda.

Ameongeza kuwa, dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwa na mfumo mzuri wa utoaji haki kwa wananchi hivyo ushirikiano wa dhati wa wizara hizo ni muhimu sana kuwezesha wananchi kupata haki zao pamoja na kuendesha shughuli za maendeleo kwa ufanisi.
"Niwaombe tuwe na ushirikiano wa kutosha na pale sisi ni wasemaji wenu kwa maana ya Serikali, ninyi hamna majukwaa ya kusemea sisi ndio tunasema tukikaa kwenye eneo. Tushirikishwe kwa asilimia zote ili tujenge mfumo bora na tujenge mfumo bora wenye matokeo makubwa badala ya kuacha tusishirikiane,"amesema.

Akizungumzia kipindi hiki cha bajeti, Mheshimiwa Geophrey Pinda amesema, "tumepambana sana kujengea uwezo DPPOs hela iliyoongezeka haikuwa lengo letu, tuliomba hela nyingi, lakini kutokana na uwezo wa Serikali wametuhold kidogo tunasubiri subiri, lakini matarajio yetu ni kwamba lazima tuwajengee uwezo ili muweze kufika kila kona zote za nchi muwe na ofisi mahali pote, lakini vitendea kazi kuna wilaya hazijafikia na huduma zenu tunahitaji mtoke wilaya moja muende kuhudumia wilaya zingine...ili muende sambamba na mabadiliko,"amesema Mheshimiwa Pinda.
DPP

Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, DPP Sylivester Mwakitalu amewapongeza wadau wa maendelo ikiwemo Serikali ya Uingereza na Umoja wa Ulaya ambao wameshiriki kikamilifu kufanikisha juhudi mbalimbali za Serikali katika kupambana na vitendo vya rushwa.

Amesema kuwa, upelelezi wa makosa ya rushwa unahitaji umakini wa hali ya juu kutokana na makosa hayo kufanywa na watu wenye weledi, hivyo upelelezi wake unahitaji umakini na umahiri ndiyo maana Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kwa kushirikiana na wadau waliona ni vyema wakatengeneza mwongozo huo ambao utawasaidia wapelelezi na waendesha mashitaka wanapoendesha kesi hizo ili kuleta usawa.
"Kwa kipindi ambacho tuliwapatia madaraka waendesha mashitaka wa mikoa na wilaya tuligundua ziko changamoto za hapa na pale hati za mashitaka za mahali pamoja zinatofautiana na hati za mashitaka sehemu nyingine, na namna uchunguzi unavyopita sehemu moja na sehemu nyingine kwa hiyo tukaona kwa kushirikiana pamoja tutengeneze mwongozo ambao utawaongoza waendesha mashitaka na wachunguzi ili waweze kufanya kazi hiyo kwa weledi, lakini tupate tija na tupate matokeo chanya,"amesema DPP Mwakitalu.

"Mwongozo huu unaozinduliwa leo, haukusudii kubadilisha dira, taratibu zilizopo ni nyongeza tu ya kile ambacho tayari kipo kitawasaidia watumishi wote ambao watashiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
"Mwongozo huu utawawezesha wapelelezi na waendesha mashitaka kushughulikia kesi za rushwa kwa urahisi na tija. Baada ya kuzinduliwa utasambazwa na kuhakikisha kwamba watendaji wote wanaupata na pale itakapolazimika kufanya mafunzo ili kurahisisha wauelewe na wautumie kikamilifu.Mwongozo huu ni nyenzo muhimu sana utatusaidia kupata matokeo chanya katika kupambana na rushwa,"amesema DPP Mwakitalu.

Naibu Mkurugenzi

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP), Bw.Joseph Pande amesema kuwa, mwongozo huo utasaidia kwa kiwango kikubwa ikiwemo kuongeza mahusiano kuanzia tukio linapotokea mpaka kesi iishe mahakamani.

"Mwongozo utatengeneza mahusiano kuanzia tukio limetokea mpaka kesi iishe mahakamani, kazi kubwa ni kushiriki katika uzinduzi wa mwongozo kwa ngazi ya upelelezi mpaka ngazi ya upitishaji na usimamiaji wa mashitaka ni nyenzo muhimu sana. Baada ya uzinduzi wa leo (umezinduliwa tayari) tutabakiwa na kazi moja kubwa ya kuwawezesha ma RPOs na RPC DPs kuelewa huu mwongozo na kuusimamia niishukuru Ofisi ya TAKUKURU, Mahakama, Polisi na wadau wengine kwa kushiriki kutengeneza huu mwongozo,"amesema Naibu DPP Pande.
Kuhusu Mwongozo

Mkurugenzi wa Divisheni ya Utenganishaji wa Shughuli za Mashtaka na Upelelezi, Bw. Oswald Tibabyekomya amesema kuwa, Mwongozo wa Kiutendaji wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka wa Kesi za Rushwa (Standard Operating Procedures for Investigation and Prosecution of Corruption and Related Offences),umetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 18 na 24 vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka, Sura ya 430 (The National Prosecutions Service Act, Cap 430).

Vifungu ambavyo amesema, vinampa Mkurugenzi wa Mashtaka mamlaka ya kutengeza miongozo kwa ajili ya kuratibu upelelezi na kusimamia mashtaka.

"Lengo la Mwongozo huu ni kuweka mfumo unaofanana wa kupeleleza na kuendesha mashtaka kwa kuelekeza masuala muhimu ya kuzingatia na kutengeneza nyenzo kama vile mpango wa uchunguzi (Investigation Plan), uendeshaji mashtaka ( Prosecution Plan) na uchambuzi wa viini vya makosa ya rushwa (Elements Worksheet) ambavyo vitasaidia kuweka utaratibu unaofanana katika kushughulikia kesi hizi,"amefafanua Mkurugenzi huyo.

Mambo Muhimu

Bw.Tibabyekomya amesema, mambo muhimu yanayosisitizwa katika mwongozo ni Kushauriana na Kuratibu Kesi Kubwa za Rushwa Mapema ( Early Case Consultation and Coordination).
"Katika eneo hili Mwongozo unawataka Wachunguzi baada ya kujiridhisha kuwa kosa limetendeka kutoa taarifa kwa Viongozi wa Mashtaka kwenye Ofisi za Taifa za Mashtaka ngazi ya Wilaya na Mikoa au Mkurugenzi wa Mashtaka ili waweze kuteua Mwendesha Mashtaka kuratibu upelelezi huo.

"Mwendesha Mashtaka anayeteuliwa anashirikiana na wachunguzi kwenye hatua zote muhimu za upelelezi kwa ajili ya kuhakikisha ushahidi wenye ubora unakusanywa ili kuwezesha kuwa na matokeo mazuri mahakamani,"amesema.

Pia anasema, ili kuhakikisha kunakuwepo na uratibu mzuri, mwongozo unataka wachunguzi na waendesha mashtaka kufanya vikao vya pamoja kabla na baada ya kukamata watuhumiwa (pre-arrest conference, post arrest conference) au wakati wowote linapotokea jambo la dharura (emergency conference) kwa ajili ya kujadili mwenendo na masuala muhimu ya upelelezi.

Utaratibu wa Kuzingatiwa

Katika, mwongozo huo, Mkurugenzi Tibabyekomya anasema,wakati wa ukusanyaji ushahidi mwongozo unafafanua utaratibu wa kufuata wakati wa ukamataji, upekuzi na ukusanyaji wa ushahidi wa aina mbalimbali kama vile uchukuaji wa maelezo ya mashahidi, maelezo ya washtakiwa ushahidi wa kitaalam ili kuhakuikisha ushahidi unakusanywa kwa kuzingatia sheria.
Upelelezi wa Mburulo wa Kifedha ( Financial Investigation).

Kwa kuzingatia kuwa, makosa ya rushwa ni makosa ambayo yanatendeka kwa ajili ya kupata fedha au mali, amesema mwongozo unawataka wachunguzi kufanya uchunguzi wa mali mapema wanapoanza uchunguzi wa makosa ya rushwa ili waweze kubaini mali hizo na kuchukua hatua stahilifu mapema.

Majadiliano ya Wachunguzi na Waendesha Mashtaka wa Kupitia Majalada ya Tuhuma

Ili kuhakikisha maamuzi yanatolewa baada ya kuelewa vizuri ushahidi, Mwongozo unasisitiza kufanya vikao vya majadiliano kati ya Wachunguzi na Waendesha Mashtaka wakati jalada linapowasilishwa Ofisi za Taifa za Mashtaka au baada ya kuwa jalada limepitiwa na waendesha mashtaka katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Vikao hivi vinaweza kuombwa na Wachunguzi au kuitishwa na Waendesha Mashtaka wanapoona kuna jambo linalohitaji majadiliano.

Maandalizi Mazuri ya Kesi

Baada ya upelelezi kukamilika na kesi kufunguliwa mahakamani Mwongozo unawataka wachunguzi na waendesha mashtaka kufanya maandalizi vizuri kabla ya kesi kuanza kusikilizwa kwa kufanya vikao kabla ya kesi kuanza (pre-trial conference) kati ya wachunguzi na waendesha mashtaka. Mwongozo pia umetengeza nyenzo (templates) kama vile nyenzo za kutumia kuwatayarisha na kuwaongaza mashahidi mahakamani na nyenzo ya kutumia kutoa vilelezo mahakamani kwa ajili ya kuahakikisha maandalizi mazuri yanafanyika.

Nyenzo ya Uchambuzi wa Viini vya Makosa

Mwongozo pia umetengeneza nyaraka ya uchambuzi wa makosa yote yaliyopo katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo inachambua viini vya makosa hayo na kutoa mifano ya hati za mashtaka. Lengo la kutengeneza nyenzo hii ni kuhakikisha wachunguzi na waendesha mashtaka wanaelewa vizuri viini vya makosa ili viwasaidie wakati wa upelelezi, maandalizi ya hati za mashtaka na wakati wa uendeshaji wa kesi mahakamani.

Washirika

Kwa upande wao wawakilishi wa mabalozi, Bw.Simon Charter kwa niaba ya Balozi wa Uingereza nchini Tanzania na Simon Van Broek kwa niaba ya Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania wamesema kuwa, wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na vitendo vya rushwa.

Sambamba na shughuli mbalimbali za maendeleo Ili iweze kutekeleza kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news