WAGONJWA KUTAFUTA DAWA NJE YA KITUO NI KUWATESA-DKT.NKUNGU

NA MWANDISHI WETU

WATOA Huduma za Matibabu wamesema wako tayari kutekeleza agizo la Serikali la kutowaandikia wagonjwa fomu za kuchukua dawa kwenye maduka ya dawa nje ya kituo cha matibabu na badala yake watahakikisha huduma zote ikiwemo ya dawa inapatikana ndani ya kituo.
Wamesema kuwa agizo hilo linalenga kuimarisha huduma katika vituo na kumwondolea mzigo mgonjwa wa kutembea na fomu katika maduka ya dawa kitendo ambacho wamesema ni kumtesa mgonjwa.

Akizungumzia maandalizi ya utekelezaji wa agizo hilo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu amesema kuwa “Hii ni hatua nzuri na kubwa katika kuhakikisha huduma zinaimarishwa na zinapatikana kwa kiwango cha kutosha ndani ya hospitali zetu, itatusaidia sana katika utoaji wa huduma bora lakini pia kuongeza mapato ya kituo,” alisema Dkt. Nkungu.

Alisema kuwa baada ya kutolewa kwa agizo hilo, Hospitali hiyo imejipanga kuhakikisha inamaliza tatizo la ukosefu wa dawa ambao ulikuwa ukisababisha kuandika Fomu 2C ambayo inamuwezesha mgonjwa ambaye ni mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwenda kuchukua dawa kwenye duka la dawa nje ya kituo.
Alisema kuwa kitendo cha kumpatia mgonjwa huduma zote anazohitaji ndani ya eneo moja inamsaidia kuwa na imani kubwa na kituo lakini pia inamfanya aridhike na huduma aliyopewa kuanzia ya kumuona daktari na huduma zingine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga ambaye alitembelea hospitali hiyo kuona namna ilivyojipanga katika kuwahudumia wanachama alisema kuwa Mfuko utashirikiana kwa karibu na vituo vyote vinavyohudumia wanachama wake katika kuhakikisha wanapata huduma na agizo hilo linatekelezeka bila kusababisha usumbufu kwa wanachama.

“Lengo la kufika hapa ni kuona namna mlivyojipanga katika hili, niseme tu kwamba NHIF tumejipanga na tutahakikisha tunashirikiana nanyi kwa karibu sana kuhakikisha dawa zinapatikana, tunao mpango wa mkopo nafuu wa dawa ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na tatizo hili hivyo milango yetu iko wazi tushirikiane,” alisema Bw. Konga.

Alisema kuwa mkakati huu wa kuwezesha vituo viwe na dawa za kutosha utaimarisha huduma katika vituo hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Bima ya Afya kwa wote ambapo wananchi wengi zaidi watahitaji huduma kupitia mfumo wa bima.
“Kwa sasa tunahudumia Watanzania kama Milioni nne na laki tano hivi lakini tukianza kutekeleza Bima ya Afya kwa wote ina maana itakuwa ni Watanzania milioni 60 hivyo hatutaweza kuendelea na mfumo wa wanachama kutembea na fomu barabarani kutafuta dawa ni lazima tuanze sasa kuimarisha hili hivyo tuko tayari kutekeleza agizo la Serikali,” alisema Bw. Konga.

Agizo la kupiga marufuku Vituo vya huduma kutoa fomu 2C kwa wanachama wa NHIF limetolewa na Wizara ya Afya kupitia Katibu Mkuu wake Prof. Abel Makubi ambaye amevitaka vituo vyote kuhakikisha vinakuwa na dawa na wanachama wapate huduma zote ndani ya kituo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news