Balozi Prof.Kilagi aorodhesha fursa zinazowafaa Watanzania nchini Brazil

NA GODFREY NNKO

BALOZI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Brazil, Mhe.Prof. Adelarous Kilangi amesema katika Taifa hilo la Amerika Kusini kuna fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo Watanzania wakizichangamkia zitawezesha kustawisha uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo leo Agosti 31, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka jijini Brasilia nchini Brazil kuelezea kuhusu utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na fursa zinazopatikana nchini humo.

Chimbuko la mkutano huo ambao unaongozwa na kauli mbiu ya 'Tuchangamkie Fursa Zinazopatikana kupitia Diplomasia ya Uchumi' limetokana na mikutano iliyotangulia ambayo sehemu kubwa imeandaliwa na Tanzania Watch.

Tanzania Watch imekuwa ikiandaa mikutano hii kwa ajili ya kuwajuza Watanzania kuhusu fursa zinazopatikana kupitia Diplomasia ya Uchumi.

Hizi ni fursa zinazopatikana kupitia uwakilishi wa Tanzania katika nchi mbalimbali, kupitia balozi zetu kote duniani ambapo katika mkutano wa mwisho wa Agosti 27, 2022 ulioangazia fursa zinazopatikana nchini Canada, Umoja wa Mataifa, Cuba na Brazili) kulijitokeza masuala mawili, ambayo ni:

Uelewa wa wananchi wa kawaida kuhusu fursa, na namna ya kuzifikia, na Ufikishaji taarifa sahihi na suala zima la upashanaji habari kuhusu fursa hizo.

Kwa kuzingatia masuala hayo mawili yaliyojitokeza, pamoja na mambo mengine, malengo ya mkutano huu ni kuainisha fursa zinazopatikana kupitia Diplomasia ya Uchumi katika ujumla wake.

Fursa halisi zinazopatikana kupitia Ubalozi wa Tanzania Brazili na namna ya kuzichangamkia na namna Ubalozi ulivyojipanga kuwasaidia Watanzania kuzipata fursa hizo

Sekta ya Kilimo

Balozi Prof. Kilagi akizungumzia katika Sekta ya Kilimo amesema, ubalozi umefanyia kazi fursa za kilimo cha maharage ya Soya na Mtama na Mahindi ya Njano.

"Brazil inafahamika kwa kuwa namba moja kwa uzalishaji wa maharage ya soya. Pia inazalisha mtama na mahindi ya njano kwa wingi. Kwa kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini China, Ubalozi uliweza kuitembelea Kampuni ya Longping High Tech huko eneo la Libeirao Praeto mwezi Aprili 2022, na kujionea kilimo cha Soya, mtama na mahindi ya njano, ikiwemo maabara za utafiti, uzalishaji mbegu bora na kilimo chenyewe na kisha kutoa mrejesho kwa Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Kilimo na Ubalozi wa Tanzania nchini China.

"Kampuni hiyo imeishakuja nchini Tanzania na kwa usimamizi wa Wizara ya Kilimo inaendelea na maandalizi ya kulima zao la soya kwa kiwango kikubwa, ikitarajia kulima ekari 100,000. Inatarajiwa kuwa kampuni itaingia pia kwenye kilimo cha mtama na mahindi ya njano,"amesema Balozi Prof.Kilagi.

Amefafanua kuwa, fursa iliyopo katika eneo hili ni pamoja na wakulima nchini Tanzania kuweza kulima kwa wingi zao la soya na baadaye mtama na mahindi ya njano.

Sambamba na kujifunza kutoka Brazil matumizi ya teknolojia na utaalam wa kisasa katika kilimo cha mazao hayo ili kuyazalisha kwa wingi huku yakiwa na ubora wa kutosha.

Zana za Kilimo

Balozi Prof.Kilagi amesema, katika eneo la zana za kilimo, Ubalozi ulitembelea maonesho ya zana hizo huko mjini wa Libeirao Praeto mwezi Aprili 2022, na kujionea zana za kila aina.

"Kisha Ubalozi ukatembelea makampuni kadhaa ya kutengeneza zana za kilimo kwa hatua zote, yaani zana za kusafisha mashamba, kung´oa visiki, kulima, kupanda kupalilia, kumwagilia, kuvuna,kufungasha na nyinginezo.

"Zana za kilimo zinazotengenezwa Brazil kwa ujumla zinasifika kuwa na ubora mkubwa.Ubalozi unashauri kufanya ushirikiano wa karibu na kampuni hizo ili zana hizo ziweze kufika Tanzania na kusaidia kuboresha kilimo,"amefafanua Balozi Prof.Kilagi.

Pia, amebainisha kuw,a Ubalozi unatoa wito kwa wadau mbalimbali wa kilimo nchini Tanzania kuanzisha ushirikiano na kampuni za Brazil ili kupata zana bora na madhubuti.

Kilimo cha miwa

Wakati huo huo, Balozi Prof.Kilagi amesema kuwa, Brazil inasifika kwa kuwa namba moja katika uzalishaji wa sukari duniani.

Kutokana na hatua hiyo, Ubalozi umefaulu kufanya ziara kwenye mojawapo ya viwanda vikubwa vya kuzalisha sukari cha Uzina Coruripe mwezi Mei 2022, ambacho pia kinamiliki mashamba makubwa ya miwa.

"Ubalozi ulifaulu kuwashawishi kuangalia uwezekano wa kuwekeza Tanzania kwa ubia au kwa njia nyingine yeyote, katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, na wahusika walionesha nia na utayari wa kufanya hivyo.

"Ubalozi unatoa wito kwa wadau wote wa kilimo cha miwa na utengenezaji wa sukari nchini Tanzania kuangalia uwezekano wa kuitumia fursa hii kwa kuanzisha ushirikiano na Brazil katika kukuza kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari kwa kutumia teknolojia ya kisasa,"amefafanua Balozi Prof.Kilagi.

Kahawa

Balozi Prof.Kilagi amesema, katika zao la kahawa, Brazil inaongoza kwa uzalishaji duniani. "Hata hivyo, ubalozi katika utafiti wake umegundua kuwa kahawa ya Tanzania ina mvuto wa kipekee hata kwa Brazil na kwa hiyo inaweza kupata soko kubwa sana nchini Brazil.

"Mnamo mwezi Juni 2022 Ubalozi uliratibu ziara ya kampuni ya African Pride kuja Tanzania na pamoja na mambo mengine kampuni hiyo ilikutana na wazalishaji wa kahawa.

"Ubalozi unatoa wito kwa wadau wote wa uzalishaji wa kahawa nchini Tanzania kuangalia uwezekano wa kuiendea fursa ya soko la Brazil. Ubalozi utafanya uratibu,"amebainisha.

Pia,amesema wadau wa kilimo cha kahawa Tanzania wanaweza kuangalia uwezekano wa fursa ya kushirikiana na Brazil katika kuboresha kilimo cha kahawa nchini Tanzania hasa katika utafiti na katika kutumia teknolojia ya kisasa.

Kilimo cha Pamba

Amesema, Ubalozi umekuwa unafuatilia mradi wa kilimo cha pamba unaotekelezwa maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa unaofadhiliwa na Brazil.

Balozi Prof.Kilagi amesema, Ubalozi umeshuhudia utiwaji saini mwezi Julai 2022 wa awamu ya pili ya mradi huo unaoitwa 'beyond cotton', ambao unahusu kilimo mseto cha pamba ikichanganywa na mazao mengine ya chakula.

Katika eneo hili wito wa Ubalozi ni kuwa wadau wa kilimo cha pamba wanaoguswa na mradi huu kuchota maarifa na kuyatumia katika kulima pamba kimseto kwa kuchanganya na mazao mengine ya chakula, hivyo kufanya kilimo cha pamba kisiwe chanzo cha kuathiri uhakika wa upatikanaji wa chakula.

Utengenezaji wa Mbolea

Balozi Prof.Kilagi akizungumzia katika eneo la utengenezaji mbolea, amesema Ubalozi mwezi Mei 2022, ulifanya ziara ya kutembelea mojawapo ya makampuni makubwa ya kutengenezambolea iitwayo Agronelli.

Katika ziara hiyo, ubalozi uligundua kuwa malighafi kubwa inayotumika kutengeneza mbolea hiyo ni madini ya gypsum ambayo yanapatikana kwa wingi maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

"Ubalozi uliishawishi kampuni hiyo kuangalia uwezekano wa kuja Tanzania katika uzalishaji wa mbolea. Kampuni hiyo ilikubali,"amesema Prof.Kilagi.

Aidha,Ubalozi unatoa wito kwa wadau mbalimbali wa kilimo nchini Tanzania kuangalia uwezekano wa kufanya ushirikiano na kampuni ya Agronelli na hata kampuni nyingine zenye lengo hilo katika uzalishaji wa mbolea nchini Tanzania, hivyo kupunguza bei ya mbolea.

Umwagiliaji

Prof. Kilagi akizungumzia katika eneo la umwagiliaji, amesema taifa la Brazil limepiga hatua kubwa sana. Amesema, katika eneo hili, mnamo mwezi Julai ubalozi uliwasiliana na baadhi ya kampuni ambazo zinaweza kuja Tanzania kutekeleza miradi ya umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

"Mawasiliano haya yalifanyika kwa kupitia kampuni ya African Pride nayo ya nchini Brazil. Lengo la mawasiliano haya lilikuwa ni kufaidika na maendeleo katika teknolojia na uzalishaji wa vifaa vya umwagiliaji ambavyo ni madhubuti, lakini vyenye gharama nafuu, na pia kufaidika na utaalamu, ujuzi, na maarifa ya kumwagilia maeneo makubwa ya mashamba.

"Makampuni hayo yamefanya mawasiliano ya awali na Tume ya Umwagiliaji ya Tanzania ambayo imeonesha nia ya kuwakabidhi maeneo yafuatayo,

Mosi, eneo la Malagalasi Mkoa wa Kigoma (hekta 7,000), pili eneo la Mwamapuli Mkoani Katavi (hekta 13,000), tatu eneo la Kasinde Mkoa wa Songwe (Hekta 35,000), nne eneo la Kamsamba Mkoa wa Songwe (Hekta 25,000) na Eneo la Ikombe Mkoa wa Songwe (Hekta 650).

Hii ni fursa kubwa sana kwa wadau mbalimbali na hasa wananchi na wakulima wa maeneo hayo. Ni fursa ya kuchota ujuzi na maarifa; ni fursa ya ajira; ni fursa ya kuongeza tija katika uzalishaji,"amefafanua Balozi Prof.Kilagi.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Balozi Prof.Kilagi amesema, katika sekta hiyo ya kilimo, Ubalozi unendelea pia kufanyia kazi maeneo ya zao la Ngano, Mhogo, na Matunda.

Sekta ya Mifugo na Uvuvi

Mheshimiwa Prof.Kilagi akizungumzia upande wa ufugaji wa ng'ombe amesema,Brazil inasifika kwa ufugaji wa kisasa wa ng'ombe.

Amesema,mwezi Mei 2022, Ubalozi ulifanya ziara kwenye maonesho ya ng'ombe huko Uberaba. Kisha ulitembelea Kampuni ya Geneal inayojihusisha na uzalishaji wa mbegu bora za ng’ombe. Baadaye Ubalozi ukatembelea mashamba ya mifugo ya ng'ombe aina ya Guzera, Hollandeza na Girolanda.

"Kwa kuwa Brazil iko tayari kushirikisha utaalam kuhusu ufugaji wa ng'ombe bila malipo, Ubalozi unashauri kuwa wadau mbalimbali wa ufugaji wa ng'ombe wachangamkie fursa hii ya kupata elimu na maarifa ya ufugaji wa ng'ombe huku Brazil wakati elimu na maarifa haya yanapatikana bila malipo.

"Ubalozi unashauri pia kuwa wadau waangalie uwezekano wa kutumia fursa ya mbegu bora zilizopo Brazil na kujaribu kufuga mbegu hizo nchini Tanzania,"amefafanua Balozi Prof.Kilagi.

Usindikaji wa Nyama na Maziwa

Katika eneo la usindikaji wa nyama na maziwa,Mheshimiwa Balozi Prof.Kilagi amesema, Ubalozi ulitembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya mifugo na kujionea matumizi ya teknolojia na mashine za kisasa za kukamua maziwa, kuchinja ng’ombe na kusindika nyama na maziwa.

Amesema, ubalozi unaendelea na mazungumzo na majadiliano na makampuni mbalimbali ili kuwekeza nchini Tanzania katika utengenezaji au uwezeshaji wa upatikanaji wa vifaa na mashine za kukamua maziwa, kuchinja ng’ombe, na kusindika nyam ana maziwa.

"Ubalozi unatoa wito kwa wadau wa ufugaji kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa teknolojia mpya na vifaa vya kisasa vya kukamua maziwa, kuchinja ng’ombe, na kusindika nyama na maziwa,"amefafanua Mheshimiwa Balozi Kilagi.

Uchakataji wa Ngozi

Katika eneo la uchakataji wa ngozi, amesema Ubalozi ulikutana na Kampuni ya Arcangel inayojihusisha na uchakataji wa ngozi na utengezaji wa bidhaa za ngozi.

Amesema, Ubalozi uligundua kuwa uchakataji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa sehemu kubwa unafanywa na wawekezaji wadogo wadogo (small scale operators). Pamoja na ukweli huo, bidhaa zao zina kiwango cha juu cha kimataifa.

"Ubalozi unashauri kuwa wadau wa mifugo na ngozi nchini Tanzania wanaweza kunufaika na uzoefu, utaalam, ujuzi na maarifa toka nchini Brazil kwa sababu wao wameshapiga hatua kubwa. Pia ni aina ya shughuli ambazo zinaweza kufanywa na wafugaji wadogo na wa kati, na pia wajasiriamali wadogo na wa kati,"amesema Balozi Prof.Kilagi.

Chakula cha Samaki

Pia amesema, kwa kuwasiliana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ubalozi umegundua kuwepo hitaji kubwa la chakula cha samaki kwa wavuvi wa samaki na Serikali ina mpango wa kupanua ufugaji wa samaki.

Kufuatia hali hiyo,Ubalozi ulifanya utafiti wa makampuni ya kutengeneza chakula cha samaki kwa kuzingatia kuwa Brazil imepiga hatua sana katika ufugaji wa samaki na utengenezaji wa chakula cha samaki.

"Yamepatikana makampuni kadhaa ambapo mazungumzo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi yanaendelea. Ubalozi unashauri kuwa, uwekezaji huo katika kutengeneza chakula cha samaki utakapoanza, basi wadau wachangamkie fursa mbambali ikiwemo ajira, kukiuzia kiwanda malighafi na hata kuingia ubia katika uzalishaji.

"Pia, Ubalozi unashauri kuwa kwa kutarajia kuwa chakula cha samaki kitashuka bei baada ya kuanza kuzalishwa Tanzania, basi watu wengi zaidi wanaweza kuingia katika ufugaji wa samaki ili kujipatia kipato,"amesema.

Maeneo Mengine

Mheshimiwa Balozi Prof.Kilagi akizungumzia maeneo mengine katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi ambayo ubalozi unaendelea kuyafanyia kazi amesema ni chakula cha mifugo na dawa za mifugo.

Sekta ya Mafuta na Gesi, Umeme na Nishati Nyingine

Nishati ya Ethanol

Mheshimiwa Balozi Prof.Kilagi amesema, nchi ya Brazil inajulikana sana kwa uzalishaji mkubwa wa nishati ya ethanol.Kwa sasa inatumika kupunguza gharama za mafuta.

Amesema, Ubalozi ulitembelea kiwanda cha Usina Coruripe kama mzalishaji mmojawapo mkubwa wa Ethanol nchini Brazil.

Kampuni hiyo ilionesha utayari wa kuangalia uwezekanao wa kuwekeza Tanzania. Hata hivyo kampuni ilisema ni lazima pawepo na mapitio ya sera.

"Ubalozi unashauri pawepo mapitio ya sera pamoja na kuwakaribisha wadau mbalimbali kuchangamkia fursa ya kuzalisha ethanol kama njia ya kuongeza usalama wa nishati ya kimkakati,"amesema Prof.Kilagi.

Mafuta na Gesi

Amesema, Ubalozi ulifanya ziara mwezi April 2022 kutembelea Mamlaka ya Mafuta na Gesi na pia ikafanya mazungumzo na ushirika wa makapuni ya mafuta ikiwemo Petrobras.

Mheshimiwa Prof.Kilagi amesema, Ubalozi ulifanikiwa kufufua mazungumzo kwa ajili ya kuelekea kusaini mikataba itakayowezesha kujenga uwezo kwa taasisi za serikali zinazohusika na sekta ya mafuta na gesi kama vile PURA, EWURA na TPDC.

Nishati Nyingine

Amesema, katika kutembelea Kampuni ya Umeme inayoendesha bwawa la kuzalisha umeme la Itaipu linalomilikiwa kati ya Brazil na Paraguay, Ubalozi uligundua kuwepo kwa utengenezaji wa nishati itokanayo na kuozesha mabaki ya mimea.

Balozi Prof.Kilagi amesema, baada ya kuozesha mabaki hayo na kupata gesi, mabaki nayo yanachakatwa na kuwa mbolea ya kiasili (organic fertilizer).

"Ubalozi unaendelea na mazungumzo na kampuni ya itaipu kwa ajili ya kutoa fursa kwa watanzania kujifunza teknolojia hiyo.

"Kwa vyovyote vile, hii itakuwa ni fursa kubwa kwa wakulima wadogowadogo nchini Tanzania kutumia mimea iotayo mashambani mwao, kama nyasi, kuzalisha umeme na kutengeneza mbolea ya mboji,"amesema.

Sekta ya Utalii

Amesema, katika ziara ya kikazi ya Ubalozi mjini Sao Paulo mwezi Aprili na Mei, 2022 Ubalozi uliweza kukutana na kufanya mazungumzo na kampuni ya Beyond Africa inayohusika kuitangaza Tanzania katika sekta ya utalii.

"Nia ya kampuni hiyo, pamoja na mambo mengine ni kusaidia Ubalozi katika kuitangaza na kuitambulisha Tanzania katika jumuiya mbalimbali za Brazil.

"Tayari kampuni hiyo imekubali kutengeneza makala fupi kwa lugha ya Kireno itakayoonyesha utamaduni na vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana nchini Tanzania,"amesema.

Globo TV

Pia amesema, Kampuni ya Globo TV ilitembelea Tanzania kati ya Juni na Julai 2022 na kutengeneza makala fupi katika runinga ya Globo ambayo ina watazamaji wengi katika eneo la Amerika ya Kusini.

African Pride

Amesema, Kampuni ya African Pride ina lengo la kuiungansha Afrika na Brazil. "Kampuni hiyo ilitembelea Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara kipindi cha mwezi Mei na Juni 2022 na kuongea na Mamlaka za Tanzania Visiwani na Bara kuhusu utalii.

"Mojawapo ya masuala yanayoshughulikiwa na kampuni hii ni kuwepo usafiri wa moja kwa moja (direct route) kati ya Tanzania na Brazil.

"Iwapo mipango yao itakamilika,itafungua fursa kubwa katika utalii kwa kufungua soko la Brazil kwa utalii, vivutio vya utalii vya Tanzania. Hii itakuwa fursa kubwa kabisa katika sekta ya utalii Tanzania, na utanufaisha kada zote katika sekta ya usafiri ikiwemo malazi, chakula, usafiri, afya, bima nyinginezo.

Sekta ya Viwanda na Biashara

Shirikisho la wenye Viwanda Firjan

Amesema, katika jitihada za kutafuta teknolojia na uwekezaji viwandani, Ubalozi ulishiriki katika ziara ya pamoja ya Mabalozi wa Afrika nchini Brazil kutembelea Muungano wa Ushirika wa Wenye Viwanda mjini Rio de Janeiro mwezi Aprili, 2022.

"Katika ziara hiyo, Ubalozi uliweza kuona hatua kubwa iliyopigwa na Shirikisho la wenye Viwanda (Firjan) kuwekeza kwenye utafiti na hivyo kupendekeza kuanzisha mahusiano ya kibiashara yatakayosaidia kuiunganisha Jumuiya ya Wenye Viwanda nchini Tanzania na Firjan. Firjan wako tayari kwaushirikiano na Tanzania.

Ubalozi umeshafanya mawasiliano na Jumuiya ya wenye Viwanda Tanzania, kupitia mamlaka husika, ili kuanzisha mahusiano hayo na kuwawezesha wadau husika kupata mafunzo nchini Brazil ambayo hayatozwi gharama zozote isipokuwa gharama za kuishi peke yake. Ubalozi unashauri Jumuiya ya wenye Viwanda Tanzania kuchangamkia fursa hiyo,"amesema Balozi Prof.Kilagi.

Ujenzi wa Nyumba-Kampuni ya BSI

Amesema, Ubalozi kupitia kampuni ya African Pride umeweza kuongea na kampuni ya Black Swan Innovations ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa makazi ya kisasa, lakini ya gharama nafuu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Kampuni hiyo ikiwakilishwa na African Pride iliweza kufanya mazungumzo na mamlaka kadhaa katika ziara yake nchini Tanzania mwezi Mei na Juni 2022.

Mamlaka hizo ni Wizara ya Ardhi na Nyumba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Wizara ya Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),Jiji la Mwanza,Jeshi la Magereza ana nyinginezo.

"Ubalozi unashauri kuwa hao wadau na wanufaika tarajiwa wachangamkie fursa hiyo kwa ajili ya kuendeleza makazi nchini Tanzania.

"Fursa hiyo pia itazalisha ajira nyingi sana Tanzania pamoja na kukuza biashara ya vifaa vya ujenzi. Itatoa pia nafasi ya kuhaulisha teknolojia, ujuzi na maarifa,"amesema Balozi Prof.Kilagi.

Sekta ya Michezo na Lugha ya Kiswahili

Mafunzo kwa Timu za Vijana na Makocha

Amesema, katika ziara ya kikazi ya Ubalozi mjini Sao Paulo Ubalozi uliweza kutembelea na kufanya mazungumzo na mkurugenzi wa kituo cha kuendeleza mpira wa mguu cha ZICCO.

Mheshimiwa Balozi Prof.Kilagi amesema, ubalozi uliweza kushawishi kituo cha ZICCO na kukubali kushirikiana na Tanzania katika kuifundisha timu ya mpira wa miguu ya vijana wa chini ya miaka 17na 15 pamoja na kuwajengea uwezo makocha wa timu hizo.

Pia kituo hicho kilikubali kuwapokea timu ya Taifa ya vijana kwenda kufanya mazoezi pamoja na kucheza mechi za kirafiki kwa lengo la la kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana na kuwajengea uwezo makocha wa timu za hizo.

Amesema,Ubalozi kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo unandelea kukamilisha rasimu ya hati ya makubaliano ya kuanzisha ushirikiano kati yake na kituo cha michezo cha ZICCO. "Ubalozi unashauri wadau husika kutoka ushirikiano ili kufaidika na fursa hiyo,"amesema.

Lugha ya Kiswahili

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Balozi Prof.Kilagi amesema, Ubalozi unafanya mawasiliano na mamlaka husika Tanzania kufundisha Kiswahili hasa katika jiji la Sao Paolo ambalo ni kitovu cha biashara cha Amerika ya Kusini.

Sekta ya Afya, Vifaa Tiba na Madawa

Amesema, katika ziara ya kikazi ya Sao Paulo, Ubalozi uliweza kubaini pia uwepo wa kampuni ya Eurofarma inayohusika na uzalishaji wa dawa za binadamu.

"Ubalozi umeona hii ni fursa ambayo Serikali kupitia Wizara ya Afya inaweza kuitumia kwa kuanzisha ushirikiano na wadau mbalimbali wanaohusika na uzalishaji wa dawa za binadamu nchini Brazil, ikiwemo Eurofarma ili kuwezesha upatikanaji wa dawa za binadamu na mifugo nchini Tanzania katika viwango bora.

"Kampuni ya Eurofarma inatarajia kuja Tanzania mwezi Oktoba 2022 kukutana na wadau mbalimbali. Tunashauri wadau hao kutoa ushirikiano ili kuweza kuidaka fursa hiyo, kwani inaonekana kampuni hiyo inashawishiwa kwenda mataifa kadhaa,"amesema.

Hata hivyo, Balozi Prof.Kilagi amesema kuwa,Ubalozi umejipanga kuwasaidia Watanzania kuzipata fursa hizo kupitia njia mbalimbali.

Miongoni mwa njia hizo ni tovuti ya Ubalozi,madawati ya kisekta,mawasiliano na wizara husika,mawasiliano na taasisi husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news