Rais Dkt.Mwinyi:Serikali inathamini sana mchango wa vyombo vya ulinzi na usalama

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Mwinyi amesema Serikali itatoa kila aina ya msaada kuhakikisha Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,IJP Camillus Mongoso Wambura, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,IJP Camillus Mongoso Wambura, ambapo pamoja na mambo mengine amefika kwa ajili ya kujitambulisha.

Amesema, Serikali inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo, hivyo akabainisha azma ya Serikali katika kuzitafutia ufumbuzi ili kuliwezesha jeshi hilo kutekeleza vyema majukumu yake.

Amesema, lengo la kuwepo vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kunakuwepo usalama wa kutosha hapa nchini, huku akibainisha ushirikiano kuwa ndio kichocheo cha kuleta ufanisi wa vyombo hivyo.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaridhishwa na utendaji kazi wa jeshi hilo na hivyo akasisitiza azma ya kuendeleza ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na jeshi hilo.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza IJP Wambura kwa uteuzi aliopata katika chombo hicho kikubwa na chenye umuhimu mkubwa katika usalama wa nchi.

Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IJP Camillus Mongoso Wambura alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, imekuwa katika juhudi kubwa ya kuipatia ufumbuzi changamoto ya upungufu wa vifaa na vitendea kazi muhimu vya Jeshi hilo, hususanI katika nyanja ya usafiri.

Amesema, pamoja na Serikali kutoa fedha za kutosha kwa jeshi hilo kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, lakini hivi karibuni imepokea msaada mkubwa wa magari 72, huku magari mngine 78 yakiwa njiani (katika meli) kuja nchini.

“Kuna magari mengine 117 yanaendelea na matengenezo kiwandani kwa ajili ya jeshi letu na mara tu yatakapokamilika yataletwa hapa nchini,”amesema.

IJP Wambura alisema ugavi wa magari hayo tayari umefanyika ambapo Jeshi la Polisi Zanzibar limepatiwa jumla ya magari 10 kwa ajili ya mikoa mitano, Chuo cha Polisi Ziwani pamoja na Kikosi cha Kutuliza Ghasia ‘Field Force Unit’.

Aidha, amesema mikoa hiyo pamoja na mikoa mingine ya Tanzania Bara itaendelea kupatiwa magari hayo kadri yatakavyowasili hapa nchini.
Akigusia suala la kukosekana kwa usalama katika mipaka ya Zanzibar, IJP Wambura alisema, kwa kuitikia agizo la Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu, jeshi hilo linalifanyika kazi kikamilifu suala hilo kwa kuzingatia umuhimu wa usalama nchini.

Alisema, kwa kuanzia wamefanya kikao muhimu kilichowashirikisha maofisa wa jeshi hilo kutoka pande mbili za Muungano ili kubaini chanzo cha tatizo hilo pamoja na kuzingatia uwepo wa rasilimali watu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news