Rais Dkt.Mwinyi aomboleza kifo cha Askofu John Ackland Ramadhani

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na wakristo wa Kanisa la Anglikana Tanzania kutokana na msiba wa Askofu Mkuu mstaafu wa kanisa hilo, John Ackland Ramadhani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Mwinyi.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 13, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bw.Charles Hillary.

"Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Baba Askofu John Ackland Ramadhani, Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, marehemu Baba Askofu Ramadhani wakati wa uhai wake aliwahi kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Katika salamu zake za pole, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amewataka wanafamilia na wakristo wa Kanisa la Anglikana Tanzania kuwa na moyo wa subira.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Askofu Ramadhani atakumbukwa kwa busara, upole na unyenyekevu uliotukuka na kiongozi aliyetamani kuona kanisa linakuwa chini ya misingi ya amani.Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemuombea malazi mema.

Awali, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mwinjilisti Canon Bethuel Mlula imeeleza kuwa, Baba Askofu Ramadhani amefariki Septemba 12, 2022.

"Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Kanisa la Angilikana Tanzania, Maimbo William Mndolwa kwa masikitiko makubwa, anatangaza kifo cha John Ackland Ramadhani, Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania kilichotokea Septemba 12, 2022 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alikuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.

"Mhashamu Askofu John Ackland Ramadhani alizaliwa huko Zanzibar mnamo tarehe 1 Agosti, 1932 akiwa mtoto wa Mathew Douglas Ramadhani na Bridget Ann Constance Masoud,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news