Serikali yatoa maagizo kwa kamati za usimamizi wa maafa

NA MWANDISHI WETU

KAMATI za usimamizi wa maafa nchini zimetakiwa kuandaa mipango ya dharura itakayoelekeza hatua za kuchukua kwa kila taasisi na wananchi kwenye maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambapo mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mjini Dodoma.

Taarifa ya utabiri huo inahusu maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Kutakuwa na upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo mengi unaoweza kuathiri ukuaji wa mazao, kusababisha uwepo wa visumbufu vya mazao na magonjwa.

"Kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususani katika maeneo mengi yanayotegemea mvua za vuli, hivyo kusababisha upungufu wa maji kwa matumizi mbalimbali.
PICHA NA OWM.

“Mlipuko wa magonjwa unaweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama,”amesema.

Waziri ametoa rai kwa kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi zote kushirikisha wadau wa maafa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo ikiwemo kupanda mazao yanayokomaa mapema na kuvuna maji.

“Kamati za usimamizi wa maafa, zichukue hatua za kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta za maji na umeme kuweka mipango yao ya tahadhari ili kuhakikisha kuwa usumbufu unaotokana na ukosefu wa maji na nishati unapewa ufumbuzi mapema,”amesema.

Waziri amehimiza kuimarisha udhibiti wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori ikiwa ni pamoja na kuzuia muingiliano kadri inavyowezekana; sambamba na kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa na kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news