Waziri Dkt.Tax awaita wawekezaji kutoka Poland

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt.Stergomena Tax amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Poland waje nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi wa buluu na madini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt.Stergomena Tax akisalimiana na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Poland, Bw. Zbigniew Sokal alipowasili kwenye ofisi za taasisi hiyo jijini Warsaw, Poland kwa ajili ya kushiriki mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland wenye nia ya kuwekeza nchini. Wakati wa mkutano huo kampuni 10 ziliwasilisha mada. Mhe.Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Poland.

Waziri Tax ameyasema hayo, wakati akihutubia mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland. Mkutano huo ambao uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Poland na Ubalozi wa Tanzania nchini humo umefanyika katika Ofisi za Taasisi ya Uwekezaji na Biashara ya Poland zilizopo jijini Warsaw.
Mhe. Dkt. Tax akizungumza wakati wa Mkutano uliowakutanisha wawakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Taasisi za Kiuchumi za Poland wenye nia ya kuwekeza nchini. 

Pamoja na mambo mengine aliwaeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini ikiwemo uchimbaji madini, uchumi wa bluu kilimo na miundombinu,

Mhe. Dkt. Tax amesema Serikali chini ya uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wengi wenye tija na mitaji waje kuwekeza nchini.
Wajumbe kutoka Tanzania na Poland walifuatilia mkutano. Walioketi upande wa kushoto ni Balozi wa Poland nchini Tanzania, (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (katikati) na Brigedia Jenerali, Mkeremy.

Ameyataja maeneo ambayo yanahitaji wawekezaji kutoka Poland na sehemu nyingine duniani kuwa ni pamoja uchimbaji madini, uchumi wa bluu, teknolojia ya habari na mawasiliano, viwanda vya sukari na nguo na miundombinu.

Amesema ili kuhakikisha wawekezaji wanaofika nchini wanafikia malengo yao, Serikali inaendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwemo, kuboresha upatikanaji wa viza na vibali mbalimbali lakini pia Serikali inaboresha mikataba mbalimbali ili kuondokana na urasimu wote kwenye sekta hiyo muhimu ya uwekezaji.
Mkutano ukiendelea.

Pia Serikali imeendelea kuboresha miundombinu yake ikiwemo Bandari ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wawekezaji. Huduma zingine zinazoboreshwa ni kuwa na umeme wa uhakika ambapo hadi sasa ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115 na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea nchini.
Mhe. Dkt. Tax akimsikiliza Bw. Sokal akizungumza. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Poland, Mhe.Abdallah Possi.

Amesema ziara yake nchini Poland pamoja na mambo mengine inalenga kukuza baiashara na uwekezaji kati ya nchini hizi mbili.

“Ninawakaribisha wafanyabaiasha na wawekezaji kutoka Poland kuja Tanzania. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia imejipanga kikamilifu kuwahudumia. Tunaendelea siku hadi siku kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini,"alisema Dkt.Tax.

Amesema mbali na maboresho hayo, Tanzania ni nchi sahihi kwa wawekezaji kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo amani, miundombinu ya kisasa ya barabara, reli, bandari na soko la uhakika kupitia uanachama wa Tanzania kwenye Jumuiya za kikanda za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara Barani Afrika (CFTA).
Sehemu ya wajumbe kutoka Poland na Tanzania wakifuatilia mkutano.

“Serikali imeendelea kuondoa vikwazo vya kuanzisha na kuendesha biashara kwa kupitia upya sheria, kanuni na taratibu za biashara na kuzifuta zile ambazo zimethibitika kuwa zinayafanya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kuwa magumu.”
Sehemu nyingine ya wajumbe.

Mhe. Waziri amesema kwa kuwa nchi ya Poland imepiga hatua kubwa katika masuala mengi ikiwemo teknolojia ya usimamizi wa maji, Tanzania ingefurahi kuona wawekezaji kutoka nchi hiyo wanawekeza kwenye sekta hiyo kwa wingi.
Sehemu nyingine ya wajumbe.

Amesema kuwa uchimbaji wa madini kama vile Tanzanite na mengine mengi, ni fursa nyingine ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wa Poland wanakaribishwa kuichangamkia hapa nchini.
Sehemu nyingine ya wajumbe.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Taasisi hiyo, Bw. Zbigniew Sokal alitumia fursa hiyo kumweleza utayari wa Taasisi yake kushirikiana na Taasisi za Uwekezaji nchini ikiwemo TIC na ZIPA ili kujiimarisha zaidi. Alisema tayari makampuni kadhaa ya Poland yapo tayari kuwekeza nchini Tanzania.
Mkutano ukiendelea.

Wakati wa Mkutano huo Wawakilishi kutoka Kampuni 10 za Poland zinazojishughulisha na masuala mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa mitambo ya kilimo, uchimbaji visima virefu, usimamizi wa maji na utunzaji wa mazingira, teknolojia mpya ya uchomeleaji vyuma na umeme wa jua waliwasilisha mada kuhusu Kampuni zao.

Wakati huhuo, Mhe. Waziri Dkt. Tax alipata fursa ya kutembelea Mradi mkubwa wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfera uliopo katika mji wa Jozefow.
Mhe. Dkt. Tax na ujumbe wake wakifuatilia mada kuhusu Mradi wa Usimamizi wa Majitaka wa Hydrosfora kutoka kwa Rais wa Kampuni hiyo Bw. Stanisław Zdanowicz.

Mradi huo wa aina yake pamoja na mambo mengine hususanya majitaka kutoka majumbani na kuyatibu kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji miti na maua katika mji huo.
Mhe.Dkt.Tax na ujumbe wake wakifuatilia mada.

Kadhalika takangumu zingine hutayarishwa kitaalam na kuwa mbolea ya samadi kwa ajili ya mazao hayo ya miti na maua.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Rais wa Kampuni hiyo, Bw. Stanslaw Zdanowicz amesema mradi huo ambao unaendeshwa kisasa, pamoja na mambo mengine umesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za uondoshaji majitaka majumbani kwao.
Mhe. Dkt Tax akipata maelezo ya namna wanavyobadilisha taka ngumu kuwa mbolea.
Mhe. Dkt.Tax akiwa kwenye moja ya maabara kwenye kampuni hiyo.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Tax alishukuru kupata fursa ya kutembelea Kampuni hiyo na kujionea teknolojia ya hali ya juu ya usimamizi wa kisasa wa majitaka na alitumia fursa hiyo kuwakaribisha nchini kuja kuwekeza pamoja na kutembelea vivutio vya utalii vya nchini ikiwemo Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

Mhe. Dkt.Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Tax akipokea zawadi ya mchoro wa jengo hilo.
Mhe. Dkt Tax akimpatia zawadi Rais wa Kampuni hiyo.

Katika ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Ukuzaji Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news