Waziri Mkuu:Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini kuboresha huduma za kijamii

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la Idara ya Macho katika Hospitali ya Kanda Bugando ambalo limekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa kwa kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za kibingwa za macho.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Christopher Mwanansao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Macho katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando wakati alipozindua Jengo la Huduma ya Macho katika hospitali hiyo jijini Mwanza, Oktoba 16, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Ujenzi wa mradi huu unakwenda kupunguza usumbufu kwa wagonjwa waliokuwa wakisafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 1,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda hospitali ya KCMC au Muhimbili kwa ajili ya kupata huduma bora za macho.”

Waziri Mkuu amezindua jengo hilo Oktoba 16, 2022 katika Hospitali ya Kanda Bugando j[j[ni Mwanza akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu kukagua shughuli za maendeleo zinazotekeleza na Serikali mkoani hapa. Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 3.7.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kuzindua Jengo la Huduma ya Macho, Oktoba 16, 2022. Viongozi hao kutoka kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula,Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt. Fabian Massaga, Askoku Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu wa Jimbo la Geita, Flavian Kassala. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua mradi huo unaolenga kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma bora za kibingwa na zinazokidhi matakwa na matarajio ya wagonjwa, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini likiwemo Kanisa Katoliki katika kuboresha huduma za jamii yakiwemo matibabu.

“Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha utoaji wa huduma za jamii nchini imepanuwa wigo kwa kushirikisha sekta binafsi, taasisi za dini na mashirika mbalimbali. Kanisa Katoliki ni mojawapo ya taasisi ambazo serikali imeendelea kushirikiana nazo katika utoaji wa huduma za jamii.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika Hospitali ya Bugando Serikali imekuwa na ubia na kanisa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kugharamia mishahara kwa watumishi 1,191 sawa na asilimia 66 ya watumishi wote wa hospitali ambapo kila mwezi jumla ya shilingi bilioni 1.7 hulipwa na Serikali.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu wa Jimbo la Geita , Flavian Kasalaa (wa tatu kushoto) wakizindua Jengo la Huduma ya Macho katika Hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza Oktoba 16, 2022. Wa pili kulia ni Askofu Mkuu Renatus Nkwande wa Jimbo Kuu la Mwanza, kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula, wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando, Dkt. Fabian Massaga amesema hospitali hiyo inatoa huduma kwa kushirikiana na Serikali na kwamba mradi huo uliozinduliwa leo unalenga kupunguza upofu unaozuilika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ujenzi wa mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 100 ulianza Februali 3, 2021 na ulikamilika Juni 23, 2022.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya.

Naye, Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Muhashamu Baba Askofu Mkuu Renatus Nkwande, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa ambao umewezesha hospitali hiyo kuongeza idadi ya madaktari wa macho.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali pamoja watumishi wa Taasisi ya Christian Blind Mission ya Ujerumani baada ya kuzindua Jengo la Huduma ya Macho katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza, Oktoba 16, 2022. Kushoto kwake ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katolika Tanzania (TEC), na Askofu wa Jimbo la Geita, Flavian Kassala na kulia kwake ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Muhashamu Baba Askofu Mkuu Nkwande amesema ongezeko hilo la madaktari limesaidia kuboresha huduma za tiba ya macho katika Kanda ya Ziwa. “Tangu kuanzishwa hospitali hiyo kwa zaidi ya miaka 40 ilikuwa na daktari mmoja tu wa macho aliyehudumia kanda nzima lakini sasa tunao sita.”

Post a Comment

0 Comments