Tanzania the Royal Tour yazidi kutiki ndani na nje

NA KASSIM NYAKI-NCAA

KUNDI la watumishi wa Serikali 95 kutoka Mkoa wa Kilimanjaro wametembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia filamu ya ‘Tanzania the Royal Tour’ ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliongoza filamu hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Abbas Kayanda aliyeongoza Ujumbe wa wakurugenzi wa Halmashauri na watumishi wa Mkoa wa Kilimanjaro ameeleza kuwa ziara hiyo ni hamasa ya watumishi wenyewe walioamua kuchanga fedha na kutembelea vivutio vya utalii nchini na kuamua kuanza na hifadhi ya Ngorongoro kujionea utajiri wa vivutio ikiwemo wanyamapori, Kreta ya Ngorongoro, vituo vya malikale kama eneo la Olduvai lenye historia ya chimbuko wa binadamu wa kale duniani.

“Nitoe rai kwa watumishi wa mikoa mingine kuunga mkono jitihada za Mhe Rais kwa kutembelea vivutio hivi.

Tuhamasishane ili sisi wenyewe tujenge utamaduni wa kutembelea maeneo ya utalii na kuwaelimisha Watoto wetu kujua utajiri tulionao ili tuwarithishe na wao wakiwa wakubwa wawe mabalozi wa urithi na utajiri wa vivutio vya kipekee tulivyonavyo Tanzania” alibainisha Kayanda.

Mratibu ziara ya watumishi hao Rashid Rashidi ameeleza kuwa watumishi wa mkoa wa Kilimanjaro wamehamasisika na filamu ya ‘Tanzania the Royal tour’ na kuamua kushirikiana na kampuni ya Zara tours na kuamua kutumia siku za mwisho wa wiki kutembelea maeneo ya utalii ili kuona urithi wa nchi na kuonyesha jamii umuhimu wa kutangaza urithi tulionao na kuwa mabalozi wa kuhamasisha makundi mengi zaidi yaweze kuvitembelea.

Afisa Uhifadhi Mkuu wa NCAA Peter Makutian anayesimamia shughuli za utalii amebainisha kuwa ujio wa kundi la watumishi hao ni muendelezo wa makundi ya watumishi wa Serikali, Sekta binafsi, viongozi wa Serikali, wanasiasa, na viongozi wa dini.

Wengine ni wanafunzi na taasisi mbalimbali kuja Ngorongoro mara kwa mara hali iliyoongeza idadi ya watalii ambapo kwa sasa idadi ya watalii wa ndani ya nchi inashabihiana na watalii kutoka nje ya nchi tofauti ilivyokuwa siku za nyuma.

Alieleza kuwa, uongozi wa NCAA unaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha wageni wanaotembelea hifadhi hiyo wanapata huduma bora na kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments