NA MWANDISHI WETU
AFISA Mtendaji Mkuu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa amepata tuzo ya utendaji bora na kuwa miongoni mwa Watendaji Wakuu Bora 100 waliotunukiwa tuzo hizo kwa mwaka 2022.

Bw. Nyaisa ni miongoni mwa Wakurugenzi Wakuu na Maafisa Watendaji Wakuu sita bora wa Taasisi za Serikali ambao wamepata tuzo, akiwemo pia Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania, Bw. Ladislaus Matindi na Afisa Mtendaji Mkuu wa kutoka Watumishi Housing Investment, Dkt. Fred Msemwa.
Akizungumza na watumishi wa BRELA katika Ofisi za BRELA leo tarehe 28 Novemba, 2022 baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Bw. Nyaisa amesema ushirikiano anaoupata kutoka kwa watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ndiyo uliowezesha kutambuliwa na kuwa miongoni mwa Maafisa Watendaji Wakuu waliopata tuzo.
Bw. Nyaisa amesema tuzo hiyo iwe chachu ya utendaji bora wa kazi kwa watumishi wote kwani utendaji mzuri wa kazi unaofanywa na watumishi ndiyo uliyoiwezesha BRELA kutambulika na kuchaguliwa miongoni mwa Taasisi za Serikali.
