BUNDI WA GAMBOSHI SEHEMU YA 54

NA WILLIAM BOMBOM

HAPA niseme kidogo, ndugu msomaji vifo vya ajabu ajabu au vya ghafla ndani ya jamii huwa na siri kubwa nyuma ya pazia.

Katika sheria za kichawi idadi kubwa ya wachawi huwa na dawa ya uhai mfupi kwa mtu yeyote. Dawa hiyo inaweza kumfanya maiti kusimama, kutembea, kuzungumza na kufanya mambo mbalimbali.

Endelea...

Lakini uhai huo hudumu ndani ya saa ishirini na nne, baada ya hapo mtu huyo hufa ghafla. Vifo vyao mara nyingi huwa vya kuugua kichwa, tumbo kuuma au maumivu makali ya kifua.

Hili ndilo lililofanyika kwa mzee huyo, japo kijana wake alikuwa akiujua ukweli halisi. Watu toka maeneo mbalimbali walikusanyika katika mji huo kwa ajili ya kuwatia faraja.

Mshirika wetu akisaidiwa na wachawi wenzangu waliokwenda msibani hapo, walitumia muda huo kulia sana huku wakigalagala chini. Msiba ulitia simanzi kwa kila muombolezaji, chanzo cha kifo kilikuwa ni kuumwa kwa kichwa kwa mzee huyo. Suala la kulogwa lilibaki kuwa siri ya waliokuwa wakifahamu ukweli wenyewe.

Siku ya maziko alichukuliwa maiti na kupelekwa makaburini, kiukweli ilikuwa ni maiti halisi ya mzee mwenyewe. Maana yeye hakuchukuliwa msukule bali aliuliwa kabisa baada ya kupigwa vya kutosha.

Walipofika makaburini waliendelea na taratibu za kuzika. Kabla ya kuushusha mwili wa maiti kaburini, walijitokeza nyuki wengi wakaanza kuwashambulia wazikaji.

Kila mtu alikimbia kuepusha uhai wake, kitendo hicho kilidumu muda mchache kisha nyuki hao wakapotea.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji ukihudhuria msiba kukawa matukio ya ajabu ajabu kama haya tambua kuwa kifo hicho ni cha kishirikina. Ukiona gari iliyobeba maiti inapata ajali au anatokea mnyama mkali na kuleta taharuki basi tambua kuna nguvu za ziada.

Hali ilipokuwa shwari waliendelea na maziko, lakini wakiwa wanamalizia kuzika ghafla tena alijitokeza joka mkubwa. Joka huyo alianza kuwakimbiza wazikaji hao kwa lengo la kuwadhuru, wazikaji hao walitumia majembe, mapanga na chepe kumshambulia joka huyo mpaka wakamuua.

Walimalizia maziko na kurudi nyumbani, kwa kuwa nyumbani haikuwa mbali na eneo la maziko walitumia muda mchache kufika nyumbani.

Mambo haya yalimuumiza sana kijana huyo, akaamua kutoroka nyumbani na kwenda kusikojulikana. Baada ya kutafutwa kwa madawa tulibaini alikuwa amekwenda kwa mganga huyo.

Mama yake ambaye ni mchawi mwenzetu aliamua kwenda kwa mganga huyo kumchukua kijana wake. Mama huyo alikwenda mchana kweupe akiwa hana dawa hata chembe.

Alichokutana nacho mama huyo kilituudhi kambi nzima, mganga huyo alimtuhumu mama huyo kuhusika na kifo cha mumewe. Mbaya zaidi hata kijana aliungana na mganga kumshambulia mama yake huku akisimulia kila kitu juu ya kifo cha baba yake.

Mama huyo alikuja kutusimulia kila kitu,THE BOMBOM nikishirikiana na wachawi watatu tulimfuata mganga huyo kistaarabu.

Cha ajabu alitujibu kwa jeuri, akatudhalilisha kwa maneno ya shombo. Yamkini nguvu za madawa alizokuwa anamiliki ndizo zilizokuwa zikimpa kiburi.

Tuliondoka kwa mganga huyo tukiwa na hasira juu yake, lakini tulipofika kambini hatukuwahi kumfanyia jambo lolote.

Tulisahau kama kulikuwa na jambo baya tulilokuwa tumefanyiwa na mganga huyo, kwa namna moja alikuwa katumia madawa ya sisi kumsahau.

Kwa kiasi kikubwa madawa haya yalimsaidia, toka siku hiyo tulimsahau yule kijana na mganga mwenyewe. Hakuna aliyekumbuka kwenda kulipa kisasi, maana wachawi hupenda sana kulipa visasi kwa hasimu wao.

Ndugu msomaji ugomvi huo baina yetu na mganga huyo ulianzia hapo, miezi kama sita nyuma iliyopita. Kwa kifupi mganga ndiye aliyetuchokoza kwa kumng'ang'ania mtoto wa mchawi mwenzetu aliyekuwa ameshuhudia mauaji ya baba yake.

Mzozo wa pili baina ya mganga huyo na kambi yetu ya kichawi ulikuwa hivi. Siku moja tulikuwa na sherehe yetu wachawi, sherehe hiyo ilifanyika pale kambini kwetu mji wa majengo miezi mitatu iliyopita.

Sherehe hiyo iliambatana na utoaji wa kafara za binadamu kwenye kambi yetu ya UJENZI WA GAMBOSHI MPYA. Kwa kuwa sherehe hiyo ilikuwa kubwa tulikuwa tumealika viongozi wa wachawi toka kambi mbalimbali.

Moja ya ajenda ya kuwaalika viongozi wa kambi hizo ilikuwa ni kuwashawishi kuungana na kambi yetu. Kumbuka lengo kuu la ujenzi wa GAMBOSHI MPYA ilikuwa ni kuua kambi zote ndogondogo za kichawi, ili kambi hiyo iwe miongoni mwa kambi kuu ukanda wa ziwa magharibi.

Katika sherehe hiyo tuliwaalika wachawi wa, Igagala, Usinge, Kaliua, Urambo na Tabora yenyewe. Pia tuliwaalika wachawi wa Mabanini, Uvinza, Kazuramimba, Kandaga, Sumbawanga, Mpanda nk.

Ilikuwa ni sherehe kubwa kwani ilikuwa imehusisha vigogo wa kichawi. Ndugu msomaji ngoja nikuibie siri kidogo, kama mchawi amesafi na kwenda eneo fulani kwa mchawi mwenzake huwa wanachukua maumbo ya wanyama wengine.

Maumbo hayo hutegemea na namna ambavyo wachawi hao watapenda, wanaweza wakawa paka, mbwa, mbuzi na kondoo. Kuna muda huwa wanachukua maumbo ya ndege hasa njiwa, kunguru, mwewe, popo na kuku kwa kiasi kidogo.

Kwa kuwa wanakuwa ugenini na muda wa kurudi nyumbani haujafika, basi huendelea kubaki kwa mwenyeji wao huku mchana wakivaa maumbo ya wanyama bandia.

Mfano unapokuta kundi kubwa la mbuzi wakiwa kwenye makundi makundi, muda mwingine mbuzi hao huwa ni binadamu.

Kuna muda huvaa picha ya mbwa, hapa utawakuta katika makundi makubwa ya mbwa. Mara nyingi mbwa mmoja atakuwa jike huku wengine watasalia kuwa madume.

Kwa kuwa ni jambo la kawaida kuwaona mbwa katika makundi hayo, ni vigumu kwa mtu wa kawaida kutambua kuwa wale siyo mbwa bali binadamu. Vivyo hivyo katika umbo la kondoo na paka pia utawaona mchana kweupe wakiwa kwenye makundi makundi wakitembea.

Basi katika sherehe hiyo tulichinja makumi ya ng'ombe, mbuzi na kondoo. Hata hivyo tulichinja binadamu watano kama kitoeo, maana wageni wengi kiasi hicho ingekuwa aibu kutowapa mboga nzuri.

Sherehe ilifanyika usiku katika eneo la kambi yetu ya majengo. Ilikuwa ni sherehe nzuri yenye kupendeza.

Wakati sherehe ikiendelea kuna watu tuliwabaini kuhudhuria sherehe pasipo mualiko. Katika sherehe kama hizo waganga wengi wenye madawa ya hali ya juu, mara nyingi huja kushiriki nasi pasipo kuwaona.

Kupitia madawa yao yenye nguvu zaidi huwa tunashindwa kuwaona. Vivyo katika sherehe yetu wapo waganga waliohudhuria, waganga hao waliambatana na vijana wao wa uganga.

Kwa bahati nzuri tuliwanasa vijana wawili katika mitego yetu, baada ya kuwanasa tuliwapatia kichapo kizuri huku tukiwahoji maswali.

Kipigo kilipokolea walijikuta wakimtaja mganga huyo ndiye aliyewaleta. Kiukweli mganga huyo alikuwa akiendelea kutuchokoza, tukakumbuka na lile tukio la kumng'ang'ania yule kijana.

Kwa kuwa tulijawa hasira tuliamua kuwachinja vijana wake kisha tukawapika na kuwala nyama. Sherehe kwa pamoja walikubaliana kutomuacha mganga huyo akiwa hai.

Sherehe ilikamilika kila mmoja akaenda nyumbani kwake huku tukiwa tumedhamiria kumfanyia kitu mbaya mganga huyo. Cha kushangaza kila mchawi tulisahau tukio hilo, hatukumbuka maazimio yetu juu ya mganga huyo. Nadhani madawa yake yalisababisha tusahau kumshughulikia.

Maisha yakaendelea pasipo kukumbuka nini alichokuwa katufanyia mganga huyo. Majuma matatu yaliyopita, mganga huyo katufanyia tukio jingine la tatu. Hii haikuwa bahati mbaya bali kusudi kabisa. Hapa tukabaini kuwa mganga huyo alitaka vita na sisi, vita iliyohitaji kuchukua uhai wa mmoja baina yetu au yeye. Tukio hilo lilikuwa hivi.

Siku moja tulialikwa kwenye kikao cha wachawi wa mji wa Nguruka. Kikao hicho kilifanyika kweye uwanja wa shuke ya msingi Nyangabo, kikao hicho kikihudhuriwa na wachawi wachache sana kulingana na unyeti wake...

Ndugu msomaji unadhani ni tukio gani jingine alililifanya mganga huyo dhidi ya wachawi? Unadhani nini kitampata mganga huyo? Tafadhali endelea kufuatilia simulizi hii ya Uhalisijabu kutoka kwa THE BOMBOM ili ujue mwisho wake.

Ninaomba ujiandae kusoma simulizi ya KANISA LA KICHAWI na KABURI LA RAIS WA HOVYO zitakazokuwa zinakuijia mara mbilimbili kila juma. Simulizi hizo ni mali ya WILLIAM DAUD BOMBOM.

ULAKOMEYE?
THE BOMBOM

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news