UIMARA WA CCM UNATEGEMEA UIMARA WA VYAMA VYA UPINZANI

NA WILLIAM BOMBOM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kikawa imara na makini endapo vyama vya upinzani vitakuwa dhaifu.

Ukiona kiongozi yeyote wa Chama Cha Mapinduzi anatumia hila na mabavu kuvipoteza vyama vya upinzani, basi atakuwa hakitakii mema chama chake na taifa kwa ujumla.

Uwepo wa vyama imara vya upinzani ndani ya nchi, ni msaada kwa Chama Cha Mapinduzi kufanya kazi yenye tija zaidi kwa raia.

Mathalani, Simba SC haiwezi kuwa imara endapo kutakuwa na Yanga SC dhaifu, pia Daimond Platinum kamwe hawezi kuwa imara endapo hakutakuwa na King Kiba au Konde boy.

Chama Cha Mapinduzi ni miongoni mwa vyama vyenye viongozi imara na wenye weledi, hata hivyo ndani ya chama hiki wamo viongozi dhaifu bin dhoofu ambao wamekipaka matope chama hicho.

Rejea sakata la Richmond, ESCROW, Buzwagi na mengineyo. Katika sakata hilo watuhumiwa walikuwa viongozi au wanachama wa chama hicho.

Wakati kiongozi mkuu wa chama anahangaika kukijenga chama, wanachama wa hovyo wanamrudisha nyuma. Tuhuma za waziri mmojawapo aliyetumbuliwa baada ya kujenga nyumba ughaibuni kwa gharama za ajabu ni miongoni mwa ushahidi.

Sitaki kuzungumzia sakata la mabalozi wanaowakilisha nchi zetu, madudu ni mengi mpaka inaumiza. Tumewasikia wabunge wakizungumzia wizi wa fedha za umma unaofanyika kwenye halmashauri zetu, ukimsikiliza mbunge wa Bunda pamoja na wabunge wangine wanavyozungumzia wizi wa fedha za umma katika halmashauli unaweza kulia.

Yapo matukio mengi yanayopoteza fedha za umma, kwa uzembe au kusudi yanayofanywa na viongozi wa hovyo.

Kwa sasa hakuna chama mbadala ya CCM nchini Tanzania, maana vyama vya upinzani kama vimejifia. Ukiangalia Chama cha Demokrasia na Maendeleo hakipo tena, kimechoka. Viongozi wake wanafanya siasa za kuvizia, yaani wale viongozi wa hovyo ndani ya CCM wakifanya yao ndipo nao wanapata cha kuzungumza.

Mbali ya kujinasibu kuwa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo, lakini hawaamini katika Demokrasia. Toka mwenyekiti wao aingie madarakani hajawahi kubadilika, wakati CCM kina wenyeviti wanne toka kipindi hicho.

Je, hapo kuna demokrasia kweli? Sitaki kuzungumzia yaliyomkuta marehemu Chacha Wangwe, vipi kuhusu Mhe Sumaye? Kwa upande wa Mhe. Zitto Zuberi Kabwe naweza nikawaelewa hoja yao. Maana Zitto mwenyewe alikiri kuwafanyia mizungu wakamtimua.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo cha sasa siyo kile cha nyuma tulichokuwa tukikiona kuwa mbadala wa CCM, viongozi wake wamekimbilia ughaibuni huku wakitumbua fedha za chama kama zao.

Wengine tumewasikia wakishabikia haki za binadamu yaani suala la ushoga na usagaji. Fedha za chama chao zinatumbuliwa na watu wachache huku wanachama wakiwa hawana pakukimbilia.

Je, hizi ni siasa sahihi au siasa za Kijinga ? Chama kina umri wa zaidi ya miaka 25, kinapokea ruzuku toka serekalini, lakini ofisi zake ni mbwa kachoka?.

Chama cha ACT Wazalendo hakina jipya, kiongozi wao mkuu Mhe.Zitto Kabwe ndiyo walewale. Yeye ndiye alifa na omega katika chama chake, kuna umbea nimeusikia kuwa yeye ndiye Mungu wa chama hicho akisema amemaliza hata kama atakuwa hayuko sawa.

Amewahi kukutwa na kashfa ya kuwasaliti Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Kama aliweza kuwasaliti chama waliomlea na kumkuza kisiasa, itakuwaje endapo tutampa mamlaka makuu ya nchi?.

Wanyama wetu watakuwa kwenye hali gani? Madini yetu yatakuwa salama? Kodi zetu zitakuwa salama? Ni hatari sana kuwa na kiongozi ndumilakuwili katika maslahi ya nchi na Taifa kwa ujumla. Kwangu mimi bado naona chama hiki bado hakijawa na uwezo wa kushindana na CCM.

Vyama vingine kama NCCR Mageuzi, tumekiona hakina jipya kabisa. Miaka nenda rudi mwenyekiti ni Mzee wangu Mbatia, hakuna Demokrasia hata kidogo. Hakina ofisi za maana zilizozagaa nchi nzima.

Kama wanachama wake hawamuamini mwenyekiti wao, itawezekana vipi raia wa kawaida tuwaamini na kuwapa mamlaka ya nchi? Sitaki kuzungumzia CHAUMA, TLP, CUF na vyama vingine.

Chama Cha Mapinduzi kwangu mimi ninaona kipo bora kuliko vyama vingine ndani ya Taifa hili, jambo la msingi la kuzingatia hapa.

Mosi, wanachama wa chama hiki wanapaswa kuwa makini katika chaguzi za viongozi wao. Ni swala la ajabu sana kwa mtumishi au kiongozi wa chama kusema chanzo cha mgao wa umeme Mkoa wa Dar es Salaam ni kunguru kutua juu ya nyaya.

Pili, Chama Cha Mapinduzi wanapaswa kuwa wa kwanza kuwabaini viongozi wao wa hovyo ambao wanaharibu taswira ya chama chao.

Wimbi la vijana wa CCM kuwa makasuku hakitasaidia chama na Taifa kwa ujumla. Badala ya kukosoa wao wamekuwa mstari wa mbele kusifia hata mambo yasiyo na tija kwa Taifa.

Tatu, CCM wanapaswa kuja na mabadiliko makubwa yenye tija kwa nchi, hili linawezekana endapo kutakuwa na viongozi safi na wenye uwezo na nia safi kwa nchi. Ni aibu kwa Taifa kuwa na mgao wa umeme na maji, wakati huko tulishaondoka zamani.

Nne, kuna umuhimu mkubwa kuamini katika sayansi na teknolojia. Kama malighafi tunazo wapi tunaposhindwa kubuni mambo yetu? Njia hizi zitatusaidia kupata eneo la kuingiza kodi, ni aibu kuendelea kuvizi Kodi kwenye vifurushi, umeme, bidhaa nk wakati nchi ina madini, ardhi safi, wanyama, samaki, vyanzo vya maji safi, raia wenye uthubutu.

Chama Cha Mapinduzi bado ni chama bora, kuliko chama chochote nchini Tanzania. Ni vyema tukazingatia ushauri tunaopewa kutoka kwa watu wenye tija. Hii itasaidia kuondoa siasa za kijinga zinazoweza kuletwa na wanasiasa wajinga wanaopenda kiki za kijinga ili kueneza ujinga.

NI NDOTO YANGU

THE BOMBOM

Muhimu

Maoni ya mwandishi hapo juu ni mtazamo wa mwandishi mwenyewe na si msimamo wa DIRAMAKINI, hivyo kwa maswali au hoja yanaweza kuelekezwa kwa mwandishi mwenyewe na si chombo hiki cha habari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news