Uchumi wa Tanzania unatarajia kuendelea kuimarika zaidi, MPC yabainisha

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sekta ya Fedha (MPC) imesema, ukuaji wa uchumi nchini unatarajiwa kuendelea kuimarika, kufuatia kuanza kupungua kwa athari zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 29, 2022 na Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (Monetary Policy Committee) ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof.Florens Luoga wakati akitoa taarifa kuhusu kikao cha kamati hiyo.

Kwa mujibu wa Prof.Luoga,MPC ilikutana Novemba 28, 2022 ambapo ilifanya tathmini ya utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi.

Kutokana na tathmini hiyo, na kwa kuzingatia athari za mtikisiko wa uchumi duniani kwenye mfumuko wa bei na shughuli za uchumi, Kamati iliridhia Benki Kuu iendelee na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi kwa mwezi Novemba na Desemba, 2022.

Aidha, utekelezaji huu wa sera ya fedha unalenga kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unaendelea kubakia ndani ya lengo na kuwezesha ukuaji wa uchumi nchini.

Pia, uamuzi huo unalenga kufikia malengo ya sera ya fedha ya robo ya mwaka inayoishia mwezi Desemba 2022.

Kamati pia ilijadili mwenendo wa uchumi wa Dunia na kubaini kuwa bado umeendelea kutoridhisha, hali ambayo imepelekea Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kushusha makadirio ya ukuaji wake kwa mwaka 2022 na mwaka 2023, ikilinganishwa na makadirio ya awali.

Kwa mujibu wa Prof.Luoga, mfumuko wa bei umeendelea kuwa juu ya malengo katika nchi nyingi kutokana na ongezeko la bei za bidhaa na mabadiliko ya hali ya hewa, na kupelekea benki kuu kuchukua hatua za kupunguza ukwasi ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Vilevile, kamati ilijadili na kuridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi nchini kwa kipindi cha hivi karibuni, licha ya kukabiliana na changamoto zilizotokana na mwenendo wa uchumi wa dunia.

Kamati ilibainisha kuwa, utekelezaji wa sera ya fedha uliendana na malengo yaliyowekwa na matokeo yake yalikuwa ya kuridhisha.

Aidha, kiwango cha ukwasi katika sekta ya benki kilikuwa cha kutosha na ulikuwa sawia na lengo la kudhibiti ongezeko la mfumuko wa bei. Aidha, malengo ya sera ya fedha kwa mwezi Septemba 2022 yaliweza kufikiwa.

"Mwenendo wa uchumi nchini ulikuwa wa kuridhisha, ambapo kwa Tanzania Bara uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022.

"Hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa makadirio ya ukuaji wa asilimia 4.7 kwa mwaka 2022. Kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 5, sawia na makadirio ya ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2022.
 
Ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuendelea kuimarika, kufuatia kuanza kupungua kwa athari zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani.

"Mfumuko wa bei umeendelea kuwa wa wastani, japokuwa umekuwa ukiongezeka kutokana na kupanda kwa bei za vyakula na nishati. Kwa upande wa Tanzania Bara, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 4.9 kwa mwezi Oktoba 2022 kutoka asilimia 3.8 mwezi Julai 2021, kiwango ambacho bado kilikuwa chini ya lengo la asilimia 5.4 kwa kwaka 2022/23,"amefafanua Prof.Luoga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Kwa upande wa Zanzibar amefafanua kuwa, mfumuko wa bei umefikia asilimia 7.3 kutoka asilimia 2.2, ikilinganishwa na lengo la asilimia 5. Mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia ndani ya malengo katika kipindi kilichosalia kwa mwaka 2022/23;

"Ujazi wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi umeendelea kuongezeka kwa kiwango cha kuridhisha. Ujazi wa fedha ulikua kwa asilimia 13.4 mwezi Oktoba 2022, sawia na lengo la ukuaji wa asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23.

"Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa kasi zaidi, kufikia asilimia 22 na asilimia 23.7 mwezi Septemba na Oktoba 2022, mtawalia, ikilinganishwa na lengo la asilimia 10.7 kwa mwaka 2022/23,"amefafanua Prof.Luoga.

Pia amesema, mapato ya Serikali katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 yalikuwa ndani ya malengo. Kwa upande wa Tanzania Bara, mapato yalifikia asilimia 96 ya lengo, wakati kwa Zanzibar yalikuwa asilimia 98.5 ya lengo.

Matumizi yalifanyika kuendana na malengo na kwa kuzingatia umuhimu wa kukabiliana na madhara yatokanayo na athari za mtikisiko wa uchumi wa dunia, pamoja na kugharamia ujenzi wa miundombinu.

Amesema, sekta ya nje imeendelea kuwa thabiti na tulivu, licha ya changamoto zinazotokana na athari za uchumi wa dunia. Akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa imara, kiasi cha kutosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.2.

Kiwango hicho kilikuwa juu ya lengo la nchi la kutosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi minne. Kiwango cha utoshelevu wa fedha za kigeni katika kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kinatarajiwa kuongezeka kutokana na kuendelea kupungua kwa bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hususan bei ya mafuta; na

"Pia wenendo wa sekta ya benki ulikuwa wa kuridhisha, ukiwa na ukwasi wa kutosha kuendana na mahitaji ya shughuli mbalimbali za kiuchumi, pamoja na mtaji kulingana na misingi ya sheria na kanuni na yenye kutengeneza
faida.

"Vilevile, sekta imekuwa na ongezeko la rasilimali na amana, sambamba na kuongezeka kwa ubora wa mikopo kwa ujumla. Katika kipindi kinachoishia mwezi Oktoba 2022, kiwango cha mikopo chechefu kilipungua na kufikia asimia 7.2 ya mikopo yote kutoka asilimia 8.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2021,"amefafanua Prof.Luoga.

Post a Comment

0 Comments