Waziri Dkt.Tax aipongeza UAE kwa kufungua Ubalozi Mdogo jijini Zanzibar

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.Stergomena Tax amepongeza uamuzi wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wa kufungua Konseli Kuu (Ubalozi Mdogo) visiwani Zanzibar na kutoa wito kwa wananchi kutumia uwepo wa Konseli hiyo kuboresha ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, utalii na masoko kwa bidhaa za Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Konseli Mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Visiwani Zanzibar, Mhe. Balozi Saleh Ahmed Alhemeiri. Hafla hiyo fupi imefanyika hivi karibuni katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar. Mhe. Dkt. Tax yupo mjini Zanzibar kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Mabalozi wa Tanzania unaoendelea mjini hapo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.

Mhe. Dkt. Tax ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akipokea Hati za Utambulisho za Konseli Mkuu wa UAE, Zanzibar Mhe. Balozi Saleh Ahmed Alhemeiri katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Zanzibar.

Amesema hatua hiyo ni muhimu sana katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na UAE kwani sasa fursa nyingi zilizopo Zanzibar ikiwemo utalii, uchumi wa buluu na biashara vitashamiri zaidi na kukua.
Mhe. Dkt. Tax akizungumza na Mhe. Alhemeiri mara baada ya kupokea hati za utambulisho. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Tax alipongeza uamuzi wa Serikali wa kufungua Konseli Kuu Zanzibar na kutoa wito kwa watanzania kutumia uwepo wa Ofisi hiyo kuimarisha ushirikiano
Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Alhemeiri mara baada ya kumaliza mazungumzo.

Ameongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi zimeendelea kuimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali pamoja na kutafuta fursa za biashara, utalii, uwekezaji na
masoko kwa bidhaa za Tanzania ili kuiwainua kiuchumi watanzania wote.

Ameongeza kwamba kufunguliwa kwa Konseli Kuu hiyo ni matokeo ya ziara mbalimbali za viongozi hao nchini humo ikiwemo ile ya Mhe. Rais Samia aliyoifanya nchini UAE mwezi Februari 2022 wakati wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dubai Expo 2020.
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Alhemeiri wakiwa kati picha ya pamoja.

Pia amesema wakati wa ziara hiyo, pamoja na mambo mengine,Mikataba na Hati za Makubaliano mbalimbali zilisainiwa kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

“Napongeza kwa dhati uamuzi wa Serikali ya UAE wa kufungua Konseli Kuu au Ubalozi mdogo hapa Zanzibar. Ni imani yangu kuwa, uwepo wa Konseli Kuu hii utasaidia kuharakisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano ambayo tayari yamekubalika kwa manufaa ya pande hizi mbili,"amesema Dkt. Tax. 

Akitaja maeneo ya kipaumbele ya ushirikiano kwa upande wa Zanzibar, Mhe. Waziri Tax amesema ni pamoja na Uchumi wa Buluu hususan katika uvuvi wa bahari kuu, utalii, biashara na uwekezaji kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Alhemeiri wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza (kulia) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mariam Mrisho (kushoto).

Pia Mhe. Dkt Tax amemhakikishia ushirikiano Balozi huyo na kwamba ana imani kuwa kupitia yeye masuala mengi yatakamilika.

”Tutashirikiana na wewe kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizi mbili hususan kwa upande wa Zanzibar yanatekelezwa na kama ulivyosema awali kwa kiasi fulani Zanzibar inafanana na Dubai, basi tujielekeze kuigeuza Zanzibar kuwa Dubai ya Afria,"amesema Dkt. Tax.

Kwa upande wake, Mhe. Alhemeiri amesema amefarijika kuwepo Zanzibar na kwamba yupo tayari kushirikiana na Serikali hiyo katika kukuza biashara, kilimo, elimu, na uchumi wa buluu kwani zipo fursa lukuki katika Kisiwa hiki zinazohitaji kuendelezwa.
Picha ya pamoja. 

“Nia yetu ni kushirikiana na Serikali kukiendeleza Kisiwa kizuri cha Zanzibar. Nimeona zipo fursa nyingi za kufanyia kazi. Nitajikita zaidi kwenye masuala ya utalii, biashara, elimu, uchumi wa buluu na usafirishaji kwa kuzishawishi mamlaka za UAE kuongeza safari za moja kwa moja za Mashirika ya Ndege ya UAE kuja Zanzibar ili kukuza utalii," amesema Mhe. Alhemeiri.

Mhe. Dkt. Tax yupo jijini Zanzibar kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mabalozi wa Tanzania unaofanyika Kisiwanii humo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022.

Post a Comment

0 Comments