Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ataka changamoto za urasimishaji makazi Kivule kutatuliwa

NA MUNIR SHEMWETA

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete ameagiza ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam kuitisha miamala ya wananchi wa Kata ya Kivule wasiopatiwa hati katika zoezi la urasimishaji makazi holela ili waweze kutatuliwa changamoto katika zoezi hilo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na wananchi wa Kata ya Kivule wakati wa zoezi la utoaji hati lilitokana na zoezi la urasimishaji makazi holela katika eneo hilo Desemba 23,2022.

Ridhiwani ametoa kauli hiyo Desemba 23, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa Kivule katika Manispaa ya Ilala alipokwenda kutoa hati ikiwa ni juhudi za Wizara ya Ardhi kuwapelekea wananchi hatimiliki za ardhi katika maeneo yao.
"Kwa kuwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao waliacha namba zao za simu basi Kamishna itisha miamala ya wale waliolipa na kuwaelekeza ni kitu gani cha kufanya ili waweze kupata hati,"amesema Ridhiwani.

Katika mkutano huo, wananchi wa Kata ya Kivule Manispaa ya Ilala walimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, pamoja na wao kulipa 160,000 lakini wameshindwa kupatiwa hati na kueleza kuwa kumekuwepo mawasiliano hafifu baina ya wananchi na kamati zinazosimamia zoezi hilo. 

Wananchi hao wa Kivule pia walishusha lawama kwa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kuwa kinachelewesha kukamilisha zoezi la urasimishaji katika mitaa ya Kivule.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukran Kyando amesema, Chuo cha Ardhi Morogoro kimefanya kazi kwa zaidi ya asilimia 80, lakini fedha zilizotolewa na wananchi katika zoezi hilo ni asilimia 11 pekee.

"Kata ya Kivuke ina mitaa minne na Chuo cha Ardhi Morogoro kimeingia mkataba wa kufanya kazi katika mitaa hiyo kwa ajili ya kumalizia kazi ya urasimishaji, lakini zipo changamoto mbili yaani upande wa kampuni na ule wa wananchi kutolipia viwanja zaidi ya 7000 ambavyo vimeidhinishwa,"amesema Kyando.
Naibu Waziri wa Ardhi, Mhe. Ridhiwani kupitia mkutano huo amekitaka Chuo cha Ardhi Morogoro kupeleka miamala yote iliyofanyia kazi kwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, taarifa zote zinazokusanywa kuhusiana na zoezi la urasimishaji mwenye mamlaka nazo ni kamishna na siyo kampuni.
"Kama kuna maeneo yamekwama basi makampuni yaongee na kamishna ili kujua namna ya kutatua kero ili kwenda mbele na naelekeza hadi kufikia Februari 1,2023 suala la wananchi wa Kivule kuhusiana na uasimishaji makazi tuwe tumemalizana nalo,"amesema Ridhiwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news