Waziri Dkt.Mabula atoa onyo wanaoomba vibali vya ujenzi, kampuni nne zanyimwa kazi Dar

NA MUNIR SHEMWETA

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ameonya wale wanaoomba vibali vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati majengo na badala yake wanafanya ujenzi bila kuzingatia mipango kabambe ya uendelezaji miji katika maeneo husika huku akiwataka kuacha mara moja tabia hiyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati wa zoezi la utoaji hati leo Desemba 19, 2022. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almas Nyangasa.

Waziri Dkt.Mabula ametoa onyo hilo leo Desemba 19, 2022 wilayani Kigamboni Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo waliorasimishiwa makazi yao akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Dar es Salaam.

Akitolea mfano wa Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Kigamboni, Dkt.Mabula amesema, baadhi ya wananchi wameomba vibali kwa ajili ya ukarabati wa majengo na badala yake usiku wanabomoa jengo zima na kujenga usiku na mchana nyumba za kawaida ama maduka jambo ambalo ni kinyume na utaratibu mzima wa mpango kabambe wa uendelezaji miji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula akimkamkabidhin hati mkazi wa Kigamboni wakati wa zoezi la utoaji hati leo Desemba 19, 2022 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almas Nyangasa.

Ametaja maeneo yenye mchezo huo katika Mkoa wa Mwanza kuwa ni pamoja na Nyamaga, Pamba na Mabatini ambapo alisisitiza waliopewa vibali na kwenda kinyume na utaratibu wa mipango ya uendelezaji miji kusimamisha ujenzi mara moja kwa sababau ni lazima wajenge kwa mujibu wa mpango kabambe wa halmashauri husika.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza wakurugenzi na makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa kuhakikisha wanapita na kukagua kama kuna vibali vipya vilivyotolewa na ujenzi kufanyika kinyume na mipango kabambe ya uendelezaji miji kusitishwa mara moja.

"Tunahitaji kutengeneza miji yetu hatuhitaji kurudi nyuma, gharama iliyotumika kwenye uandaaji master plan ni kubwa sana, sasa haiwezekani kujengwa nyumba mpya katika eneo lenye mastaer plan,"amesema Dkt.Mabula.
Sambamba na onyo hilo Dkt.Mabula pia ameagiza makampuni manne yaliyokuwa yakifanya kazi ya urasimishaji makazi nchini kutopewa kazi kwenye halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam na nje ya mkoa huo mpaka hapo Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji itakapojiridhisha na adhabu ilihotolewa kwa kampuni hizo kutokana na mapungufu mablimbali yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji miradi ya urasimishaji makazi holela na kuyataja makampuni hayo kuwa ni Hosea co. ltd, Makazi Consult Ltd, Visible Planners na Ereco Development Estate Ltd

‘’Tunataka tutoe fundisho maana kazi ya urasimishaji imekuwa na kelele sana na lawama hizo zomeelekezwa au kuishia wizara ya ardhi wakati maelekezo ya mhe Rais katika kutekeleza zoezi la urasimishaji ni kushirikisha makampuni binafsi kwa lengo la kuleta ufanisi,’’amesema Dkt.Mabula.

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka wananchi wanaovamia maeneo ya ardhi kuchukuliwa kama wamefanya kosa la jinai na siyo wavamizi wa kawaida. 

Dkt.Mabula amesema, kumekuwa na tabia inayoonesha kuwa wananchi wanaochukua ardhi za watu kama wavamizi wakati watu hao wanatenda kosa la jinai na kusisitiza kuwa watu hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kama wakosaji wengine wa jinai.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almas Nyangasa alimuambia Waziri wa Ardhi kuwa wilaya yake inaendelea kujipanga vizuri katika masuala ya ardhi na kufanikiwa kuhakikisha maeneo yanapangwa na kupimwa kwa maelekezo ya mipango miji ingawa inakabiliwa na changamoto za vitendo vya uvamizi vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio waadilifu na kubainisha kuwa tatizo hilo wanaendelea kupambana nalo.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukran Kyado alisema kuwa, ofisi yake imekuwa ikishirikiana vyema na halmashauri ya Manispaa ya kigamboni katika masuala ya ardhi na kubainisha kuwa kuanzia julai 2022 idara ya ardhi kwenye halmashauri hiyo imefanikiwa kuandaa jumla ya hati 4,722.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news