Mbwana Samatta:Nitacheza timu yoyote, ili mradi niwe nimerudi nyumbani

NA DIRAMAKINI

NAHODHA na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Ally Samatta ameweka wazi mpango wake wa kucheza Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, kabla ya kutangaza kustaafu hivi karibuni.

Samatta amesema katika maisha yake ya soka hakupata nafasi ya kucheza kwa muda mrefu nchini Tanzania, hivyo anatamani kutumia nafasi hiyo kulijua vizuri Soka la Bongo.

Akizungumza na Salama Jabir kwenye Kipindi cha 'Salama Na', Samatta amesema anataka kujenga mahusiano na ukaribu na watu wa nyumbani kwa kuwa muda mwingi amekua akicheza soka lake nje ya nchi.

“Mipango yangu ni kuja kumalizia mpira wangu hapa nyumbani, kama ambavyo watu wanajua kuwa sijacheza kwa muda mrefu soka la nyumbani.

“Nitarudi kucheza ili kujenga mahusiano na watu pamoja na kulijua vizuri soka la nyumbani, na hii ninataka kuwaambia watu wasifikirie kuwa nitarudi kwenye timu yangu ya zamani, hapana, ninaweza kucheza timu yoyote.

“Siyo lazima ziwe timu hizo kubwa, nitacheza timu yoyote, ili mradi niwe nimerudi nyumbani na kutimiza dhamira yangu ya kujua vizuri ladha ya soka letu la Tanzania,” amesema Samatta.

Kabla ya kutimkia TP Mazembe Samatta alikuwa akiitumikia Simba SC iliyomsajili akitokea African Lyon iliyokuwa inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa wakati huo.

Mbali na TP Mazembe aliyoichezea kwa mafanikio makubwa Barani Afrika, Samatta amecheza soka Barani Ulaya akiwa na Klabu za KRC Genk (2016–2020) akifunga mabao 43 katika michezo 101 aliyocheza.

Msimu wa 2020–2021 alisajiliwa Aston Villa ya England aliyoitumikia katika michezo 14 na baadae alitimkia Uturuki kujiunga na Fenerbahçe (2020–2021).

Mwaka 2021–2022 aliuzwa kwa mkopo Antwerp ya Ubelgiji akicheza michezo 27 akifunga mabao matano kabla ya kurejea KRC Genk mapema mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news