Waziri Kairuki awaonya wanaokiuka mwongozo wa kutoa adhabu shuleni

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imesema hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya walimu ambao wanakiuka mwongozo wa kutoa adhabu kwa wanafunzi shuleni kama ilivyoanishwa wazi kupitia Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002.

Pia walimu wametakiwa kutambua kuwa, wamekasimiwa mamlaka ya kuwa walinzi wa watoto wanapokuwa shuleni, hivyo wasiwe sehemu ya kuwafanya watoto kuwa watoro kupitia adhabu wanazozitoa na zinazokiuka taratibu, miongozo na kanuni mbalimbali.
"Hatusemi watoto wasichapwe, lakini wachapwe kwa kufuata taratibu na vigezo na kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa;

Hayo yamesemwa leo Januari 25, 2023 na Waziri wa OR-TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki katika kikao kazi cha uboreshaji wa usimamizi wa elimu msingi, na sekondari kwa maafisa elimu kata, wakuu wa shule za sekondari, walimu wakuu wa shule za msingi na viongozi wa elimu ngazi ya halmashauri mkoani Dar es Salaam.

Mheshimiwa Waziri Kairuki amewataka walimu kote nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zilizoanishwa kwenye waraka huo ambao umeeleza wazi ni nani mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko na viboko vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi.

"Suala zima la adhabu ya viboko mashuleni linaongozwa na Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 na umeeleza bayana kabisa.Kwa mujibu wa mwongozo huo umeelekeza adhabu hiyo ya viboko inaweza kutolewa pale ambapo umetokea utovu wa nidhamu uliokithiri au makosa ya jinai yaliyotendeka ndani au nje ya shule yenye muelekeo wa kuishushia heshima shule,"amesema.

Kuhusu Waraka

Mwongozo wa kutoa adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 (1) (v) cha Sheria ya Elimu sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002 ambao unampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni za masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa masuala ya sheria hiyo umefafanua kwa kina kuhusu adhabu.

Aidha, miongoni mwa kanuni zilizotungwa ni pamoja na The Education (Corporal Punishment) Regulation G.N. 294 ya mwaka 2002. Kanuni hizi zinatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani.

Kanuni ya 3 (1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.

Pia Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne kwa tukio lolote.

Sheria imempa mwalimu mkuu wa shule husika mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo.

Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakua na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

Kanuni ya (5) inataka kila adhabu ya kiboko inayotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na mkuu wa shule husika.

Mheshimiwa Waziri Kairuki amefafanua kuwa,kwa mujibu wa waraka huo adhabu inayotolewa lazima izingatie vigezo ikiwemo ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na haipaswi kuzidi viboko vinne kwa wakati mmoja.

"Adhabu ya kiboko inayotolewa lazima izingatie vigezo ikiwemo ukubwa wa kosa, umri, afya, jinsia na haitakiwi kuzidi viboko vinne kwa wakati mmoja na inapaswa kutolewa kwa makosa ya utovu wa nidhamu uliokithiri, ama kwa makosa yatakayotendeka ndani ama yatakayotendeka nje yatakayoishushia heshima shule.

"Na utoaji wa adhabu hiyo kwa mtoto inaelezwa wazi kuwa, mtoto wa kike anapaswa kuchapwa mkononi na mtoto wa kiume anapaswa kuchapwa kwenye makalio,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki amebainisha kuwa, adhabu hizo kwa mtoto wa kike baada ya kutolewa kibali na Mwalimu Mkuu wa shule inapaswa kutolea na mwalimu wa kike na kwa upande wa kiume inapaswa kutolewa na mwalimu wa kiume.

Labda pale tu ambapo shule husika haina mwalimu wa kike, basi Mkuu wa Shule atatoa maelekezo kwa mwalimu aliyemteua.

"Waraka huo umeeleza kuwa mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko ni mwalimu mkuu au mkuu wa shule husika au mwalimu mwingine atakayekuwa ameteuliwa tena kwa maandishi,"amesema.
Wakati huo huo,kwa kuwa waraka unamtambua Mwalimu Mkuu kama mtu mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko kwa mwanafunzi husika basi unamtaka pia atie saini yake katika kitabu hicho maalumu kila adhabu ya viboko inapotolewa.

Ukikataa adhabu

Waraka wa Elimu (Na.24) kuhusu adhabu ya viboko unasema mwanafunzi anapokataa adhabu ya viboko sharti asimamishwe shule ili kupisha hatua zingine za kinidhamu juu ya kosa lake.

Pia waraka huo unawaonya walimu kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya yeyote ambaye atakiuka utaratibu ulioidhinisha na waraka huu.

Kwamba kupitia Waraka wa Elimu (Na.24) kuhusu adhabu ya viboko ni marufuku kwa mwalimu yeyote kuonekana na fimbo mkononi kwa lengo la kumuadhibu mwanafunzi shuleni.

Post a Comment

0 Comments