Mwanasiasa Hassan Mussa Takrima afariki

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Hemed Suleiman Abdulla ameongoza viongozi wa chama na Serikali, wanafamilia, na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Kumuombea Mwanasiasa Mkongwe nchini, Mhe. Hassan Mussa Takrima iliyosaliwa Msikiti wa Fuoni meli tano Wilaya ya Magharibi B.
Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifika nyumbani kwa marehemu kutoa pole kufuatia msiba huo na kueleza kuwa marehemu alikuwa ni kiongozi mwenye hekima na busara kipindi chote cha uongozi wake akiwa mtumishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, Alhaj Hemed ameeleza kuwa Marehemu alikuwa ni muumini wa Umoja na Mshikamano na kuwataka wafiwa kuyaendeleza mema hayo pamoja na kuwa na subira kipindi chote cha Msiba na kuendelea kumuombea Dua marehemu huyo.

Akimuelezea Mheshimiwa Takrima aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar ndugu Vuai Ali Vuai amesema, marehemu katika Utumishi wake alikuwa ni Kiongozi wa mfano ambae alitumia Elimu na uzoefu wake katika kukiletea maendeleo Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa ujumla.

Marehemu katika uhai wake ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi.

Marehemu Hassan Mussa Takrima amefariki usiku wa kuamia leo nyumbani kwake Fuoni Meli Tano na kuzikwa Kijijini kwao Makunduchi Miwaleni.

Innaa Lillaahi wainnaa Ilaihi Raajiun.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news