Wizara yatoa maelekezo kwa wamiliki wa shule nchini

NA MWANDISHI WETU 

WIZARA ya Elimu imewakumbusha wamiliki wa shule kutoingiza shuleni vitabu vyenye maudhui ambayo hayaendani na mila na desturi na utamaduni wa nchi yetu.

Vitabu hivyo vimekuwa na hadithi ambazo maudhui yake yanahatarisha ukuaji na malezi ya mwanafunzi na pia kupotosha mila zetu katika makuuzi ya watoto na watanzania kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Michael amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini kuwa kuna baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikiingiza na kutumia vitabu ambavyo maudhui yake yanakinzana maadili ya kitanzania.

Amesema, ni vizuri wamiliki na waendeshaji wa shule wakafuata Waraka Na 4 wa mwaka 2014 uliotolewa na Wizara ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kuhakikisha kuwa vitabu vya ziada na kiada vinavyotumika katika shule vina maudhui yanayoendana na mila na desturi na utamaduni wa nchi yetu.

"Wamiliki na waendeshaji wa shule zote za Umma na binafsi zilizosajiliwa hakikisheni mnafuata naa kuzingatia waraka huo pamoja na miongozo inayosimamia elimu ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria na mpaka kufutiwa usajili shule," amesema Katibu Mkuu Michael.

Amesema Wizara itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia utoaji wa elimu na kuhakikisha njia za ufundishaji na ujifunzaji zinazingatia ubora na maslahi ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news