SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-3

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia.. Majina mbalimbali yalikuwa yametajwa kwa ajili ya mtoto huyo, majina hayo ni pamoja na Kashinje, Masalu, Kalekwa, Tombina na THE BOMBOM.

Endelea

Ndugu waliendelea kuvutana juu ya jina sahihi lililostahili kwa mtoto huyo. Katika kujadiliana majina mawili yalielekea kuzungumzwa sana, majina hayo yalikuwa ni Tombina na THE BOMBOM.
Hatimaye waliamua kupiga kura ili kuchagua jina moja baina ya hayo, baada ya kura kupigwa jina la THE BOMBOM lilipata kura nyingi.

Hatimaye mtoto huyo alipewa jina la THE BOMBOM,kila mmoja aliridhia jina hilo kupitia kura zilizoamua.

Kwa kuwa ilikuwa ni msibani, wazee wa ukoo huo walikuwa wamehudhuria karibu wote. Kabla ya kutandua matanga wazee kadhaa wa ukoo huo waliamua kumfanyia tambiko mtoto huyo yaani THE BOMBOM.

Walimchukua na kumpeleka katikati ya zizi la ng'ombe, wazee hao walikuwa wamevaa kaniki wakiwa wamefunga rubega. Kaniki walizokuwa wamevaa zilikuwa ni nyeusi tii mithili ya giza, hata kwa upande wa mtoto alikuwa amevalishwa nguo zenye rangi nyeusi pia.

Walipofika katikati ya zizi walikusanya kinyesi cha ng'ombe kibichi wakaanza kumpaka huku wakizungumza maneno fulani.

Kinyesi hicho kilichanganywa na dawa za aina tofauti tofauti, jambo hili lilifanyika muda wa saa sita mchana.

Ng'ombe wachache weusi tii walikuwa wameachwa zizini humo kwa ajili ya tambiko. Wazee waliendelea kumtambikia mtoto huyo pasi na shida, ukafika muda wa kumtemea mate kichwani mtoto huyo.

Kila mzee alimtemea mate yaliyomfanya mtoto huyo kulowana zaidi. Mambo yalikuwa yamepangiliwa vyema, kila tukio lilifanyika kwa utaratibu maalimu. Baada ya hapo ulifika muda wa kumchanja chale mtoto huyo, mzee aliyekuwa ameandaliwa kufanya kazi hiyo alianza.

Damu zilichuruzika mfano wa bomba la maji, wazee hawakujali hilo maana walichokuwa wakifanya kilikuwa na umuhimu kwa maisha ya mtoto.

Walipokamilisha tambiko hilo walimchukua mtoto huyo na kwenda naye porini. Kule porini kulifanyika matambiko ya kila aina, malengo ya matambiko hayo kwa mtoto ilikuwa ni kuondoa mikosi katika ukoo na familia kwa ujumla.

Mtoto huyo hakuwa na wazazi wote yaani alikuwa yatima, baba alikufa baada ya kumbaka mama wa mtoto huyo.

Mama naye alifariki muda mfupi baada ya kumzaa mtoto huyo, wazazi pekee walezi waliokuwa wamesalia alikuwa ni babu na bibi.

Hivyo basi, tambiko hilo lilifanyika kwa malengo ya kuondoa mikosi katika familia na ukoo kwa ujumla.

Madawa mbalimbali ya kumlinda mtoto na nguvu za kichawi au kiganga alichanjiwa. Katika ulimwengu wa kichawi au kiganga, mtoto anayebakia baada ya wazazi wake kufa kipindi cha kujifungua hutumika kama kizimba. Kwa namna moja au nyingine, wachawi wangemtafuta kwa ajili ya kumuua.

Maisha yaliendelea kama kawaida, mtoto huyo alilelewa na bibi yake. Afya ya mtoto huyo iliendelea kuimalika kila uchwapo, alifutuka mithili ya gogo la mpingo mbele ya mchonga vinyago.

Mashavu yalivimba mfano wa mimba ya kicheche, alikuwa ni mtoto mwenye siha njema. Katika makuzi ya mtoto huyo, kuna mambo ya kushangaza yalikuwa yakijitokeza mara kwa mara.

Mambo haya yaliwafanya wanafamilia kumpenda zaidi, akiwa na umri wa miezi mitatu alianza kutambaa jambo ambalo ni tofauti kabisa na makuzi ya watoto wengine.

Mtoto huyo alikuwa ni kipenzi cha watu katika familia nzima, pia wadudu walimpenda sana. Ilikuwa ni kawaida kumkuta anacheza na nyoka wa aina mbalimbali, nyuki na wadudu wengine kama manyugi walipenda kucheza na mtoto huyo.

Ajabu hakuna siku hata moja alidhurika, kila walipochoka kucheza na mtoto huyo waliondoka na kumuacha akiwa salama salimini.

Alipenda kucheza na wanyama wote kama vile: mbuzi, kondoo, mbwa, ng'ombe, punda na ngamia. Kuna muda wanyama wakali kama Simba na chui walionekana nyumbani hapo wakicheza na mtoto huyo.

Kadri alivyokuwa akikuwa ndivyo maajabu yalivyoongezeka kwa kijana huyo. Alikuwa ni mpole, mkarimu na asiyependa makuu, kuna muda aliweza kutatua ugomvi wa mbwa na mbwa waliokuwa wakipigana pale nyumbani.

Wahenga walisema jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza, hapa hawakukosea hata kidogo. Kwa upande mwingine mtoto huyu alikuwa na siri iliyofichika, ni watu wachache sana waliolifahamu hilo.

Mtoto huyo alianza uchawi siku ya kuzaliwa, bibi yake mlezi ndiye aliyemfundisha uchawi huo. Bibi huyo ndiye aliyekuwa mchawi Mkuu kanda ya Magu na vijiji vingine vya jirani.

Bibi huyo ndiye aliyegundua nguvu za ajabu mwilini mwa mtoto mara baada ya kuzaliwa, alibaini kuwa mtoto huyo alikuwa tofauti na watoto wengine.

Baada ya kumfuatilia kwa kina aligundua kuwa mtoto huyo alipaswa kusaidiwa kwa namna yeyote kufikia malengo fulani.

Bibi huyo alianza kutoka naye kila alipokwenda uchawini, kwa kuwa alikuwa ndiye kiongozi wa wachawi hakuna mchawi ambaye angeleta ubishi.

Baadhi ya wachawi waliwahi kuoteshwa kuwa katika familia ya kiongozi wao wa uchawi, atazaliwa mtoto wa ajabu ambaye angekuwa msaada kwa wachawi wote wa Afrika.

Hatimaye yalikuwa yamekamilika, licha ya udogo ule, lakini mtoto THE BOMBOM aliendelea kufanya mambo makubwa.

Kitendo cha kuzungumza na wanyama wa aina mbalimbali, wadudu na viumbe wengine ilikuwa ni ushahidi tosha wa utabiri wa ndoto za wachawi hao.

Ndugu msomaji unaweza kijifunza uchawi kwa njia tatu, njia ya kwanza ni kupitia watu wanaokuzunguka. Endapo wazazi wako au watu wako wana taaluma hiyo, unaweza kijifunza uchawi ungali bado ni kichanga.

Zipo aina fulani ya dawa ambazo zinaweza kuchanjwa mikononi, miguuni, utosini na kinywani. Baada ya hapo unaweza kupakwa dawa fulani ambazo zitabadili mizimu yako kuwa ya kichawi.

Mara nyingi wachawi wa namna hii ndiyo huwa magwiji, maana wao hukulia kwenye uchawi na wana asili ya uchawi.

Njia ya pili ni uchawi wa kununua, huu hujikita zaidi kwa mtu yeyote aliyevutiwa na uchawi. Mtu huyo hupewa masharti kadhaa kama vile kutoa kafara ya baba, mama, mtoto au mwenzi.

Endapo atatimiza na masharti mengine huanza kufundishwa uchawi huo. Njia ya tatu ni baadhi ya watu wana nguvu fulani miilini mwao, watu hawa ni ngumu kwa wao kujitambua. Wachawi huwabaini haraka kupitia kukutana nao, wanapombaini huwa wanatengeneza urafiki kisha wanaanza kumsogeza taratibu.

Wachawi walimpenda sana THE BOMBOM licha ya kuwa katika umri mdogo. Kila walipozunguka kwa waganga na waganguzi, waliambiwa kuwa mtoto aliyetabiriwa muda mrefu alikuwa ndiye huyo.

Katika historia za wachawi waliopita, mtoto huyo alitabiriwa namna atakavyotungwa mimba na vifo vya wazazi wake.

Walitabiri namna atakavyokuwa, mitihani atakayopitia na namna atakavyowaunganisha wachawi wote. Walitabiri pia kuwa mtoto huyo atafanya uchawi mchana na usiku, ataloga peupe na gizani. Watu watampenda, wachawi kwa wasio wachawi.

Hatimaye alipofikisha miaka mitano THE BOMBOM aliandikishwa kujiunga na darasa la kwanza katika shule ya msingi Ilungu iliyopo Magu Jineri.

Mwalimu wa darasa la kwanza Mwalimu Nyambocha, alitokea kumpenda sana kulingana na uwezo wake mtoto huyo.

Akiwa darasa la kwanza mtoto huyo alikuwa na uwezo wa hali ya juu. Japo hakusoma elimu ya awali lakini alijua kuhesabu, kuandika na kusoma vyema.

Kilichomshangaza zaidi Mwalimu Nyambocha, ni uwezo wa mtoto huyo kuzungumza lugha nne kwa ufasaha.

Alizungumza lugha mama Kisukuma ambayo ilikuwa ni lugha yao, mara nyingi kabila hili hujivunia lugha yao.

Si rahisi kuwakuta wasukuma wakizungumza lugha nyingine tofauti na kisukuma hata kama ni wasomi kiasi gani.

Pia aliweza kuandika na kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili alifahamu kwa kina sarufi ya lugha hii, aliifahamu semantiki, sintakisia, fonolojia na mofolojia ya maneno ya Kiswahili.

Licha ya umri ule pia, aliweza kuzungumza kwa lahaja nyingi kama kimtang'ata, kiyao, kipate, kilamu, kingazija na kiunguja.

Lugha zingine alizozimudu ni kiingereza na kiarabu, aliweza kuziandika na kuzizungumza kwa ufasaha.

Mwalimu Nyambocha alitokea kumpenda kijana huyo, walimu wa shule ya msingi Ilungu walibaki wakimshangaa mtoto huyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo bwana Magaka, aliamua kumueleza afisa elimu wa wilaya juu ya mtoto huyo.

Afisa elimu alipofika shuleni hapo hakuamini alichokiona, kila mtihani aliopewa mtoto huyo alipata alama zote.

Ikabidi mtoto huyo apandishwe darasa kupitia mfumo wa elimu Prem, na kupelekwa darasa la sita. Yalikuwa ni maajabu makubwa kwa mji wa Magu na nchi kwa ujumla, mtoto wa miaka minne kusoma darasa la sita ilishangaza.

Taarifa za mtoto huyo zilizagaa nchi nzima, wasomi mbalimbali walikuwa wakifika shuleni hapo kufanya mahojiano.

Mle darasani mtoto huyo aliendelea kufanya vizuri, ilikuwa ni kawaida kumkuta darasa la saba akiwafundisha wanafunzi wengine wakati wa mapumziko.

Kila mwanafunzi alimpenda, kuna muda wanafunzi wenzake hawakumielewa walipomkuta akicheza na wanyama wakali. Hakuna hata mmoja aliyekuwa akijia siri iliyokuwa nyuma ya mtoto huyo shuleni hapo.

Habari za mtoto huyo zilimfikia Padri Samson Mcjohn, huyu alikuwa ni padri wa Othodox. Yeye alikuwa anatokea jimbo kuu la Magu Parokia ya Masanza.

Padri huyu alikuwa ni Mrusi aliyekuja kueneza habari za Mungu ndani ya Taifa letu. Padri huyo alipofika shuleni hapo alifuata taratibu zote, kisha akaomba kuzungumza na mtoto huyo faragha.

Walimu walimruhusu kuzungumza naye sehemu ya wazi ili asije akamfanyia mambo ya ajabu. Watu weupe si wa kuamini hata kidogo, wengi wao ni walaghai na matapeli wakubwa.

Hilo ndilo lililowafanya walimu kuruhusu mazungumzo hayo yafanyike peupe, lengo la walimu ilikuwa ni kumlinda mtoto huyo.

Hawakuwa wakijua upande wa pili wa mtoto huyo, alikuwa ni mchawi mkubwa mwenye uwezo wa kufanya jambo lolote.

Hakuhitaji ulinzi wa kibinadamu, mwenyewe alijitosheleza kwa lolote lile. Kwa umri huo alikuwa na uwezo wa kujibadili katika umbo la mdudu, mnyama au kiumbe yeyote kadri alivyojisikia.

Kwa umri huo alikuwa na uwezo wa kukifanya kitu kikabadilika katika umbo alilolitaka, mtoto huyo alikuwa na nguvu za ajabu japo walimu na jamii hawakulijua hilo.

Ndugu msomaji, taratibu mambo yanaanza kuchanganya. Unadhani nini kitamtokea Padri Samson Mcjohn katika mazungumzo yao? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

WATOGWA?

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news