Rais Dkt.Mwinyi aendelea kuifungua Zanzibar kiuchumi, bandari jumushi ya Mangapwani mambo safi

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema eneo la Mangapwani kwa sasa litakuwa kituo kikuu cha biashara ya mafuta nchini.
Hayo yamesemwa Machi 4, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa Bohari ya Mafuta Mangapwani iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja,

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amezitaka wizara zinazohusika kuzielekeza kampuni zote za mafuta kuelekeza shughuli zote za mafuta kwenye eneo hilo. 

“Serikali imekusudia kampuni zote za mafuta kushushia mafuta yao hapa Mangapwani,"amesema Rais Dkt.Mwinyi.
Amesema, hatua za awali za ujenzi wa bandari hiyo ni kuanza kwa ujenzi wa barabara kubwa ya kilomita 60 ambayo alieleza itakuwa barabara ya kwanza kubwa na yenye ubora kwa Zanzibar na uwezo wa kuhudumia magari makubwa ya kubebea mizigo mizito kulingana na uhalisia wa bandari yenyewe. 

Dkt.Mwinyi amesema, bandari jumushi ya Mangapwani itahusisha bandari ya makontena itakayokuwa na gati ya urefu wa kilomita moja itakayohudumia sio Zanzibar pekee bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na makontena yatakayoshushwa bandarini hapo yaende hadi Dar es Salaam, Mombasa, Beira hadi Durban Afrika Kusini yakitokea Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe.Dkt.Amani Abeid Karume alipowasili katika viwanja vya Kampuni ya Mafuta ya United Petroleum (UP) Mangapwani kwa ajili ya uzinduzi wa Bohari ya Mafuta ya kampuni hiyo. (Picha na Ikulu). 

“Tunataka bandari hii isihudumie Zanzibar pekee, tunataka Dar es Salaam, Mombasa, Beira hadi Durban Afika Kusini waitumie bandari hii,"ameeleza Rais Dkt.Mwinyi.

Bandari nyingine inayotarajiwa kujengwa eneo hilo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameeleza ni bandari ya nafaka itakayohusisha ushushwaji wa bidhaa zote za vyakula ikiwemo mchele, maharage, mahindi, unga wa ngano na vyakula vingine ambavyo vitashushwa kwa muda mchache ili viwafikie wananchi kwa wakati, ujenzi mwingine ni wa bandari ya mafuta itakayohifadhi lita milioni 21. 
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza bandari nyingine itakayojengwa kwenye eneo hilo ni bandari ya uvuvi itakayokidhi Sera ya Uchumi wa Buluu nchini, amesema bado Serikali haijavuna vya kutosha rasilimali za bahari na ujenzi wa bandari ya kisasa ya uvuvi inalengo la kuleta meli kubwa zitakazovuna vizuri matunda ya baharini wakiwemo samaki wakubwa. 

Vilevile Dkt.Mwinyi alieleza Serikali inatarajia kuwa na mafuta ya kutosha na kuweka akiba ili Zanzibar iuze mafuta hadi nchi nyingine zisizokuwa na bahari na ujenzi wa bandari jumushi ya Mangapwani ni ufumbuzi wa changamoto zizilizopo kwenye bandari ya Malindi ambako meli hutumia siku 5, 7 hadi 10 kushusha mizigo hiyo, hali inayosababisha kupunguza uchumi wa nchi. 
Akizungumzia kwenye hafla hiyo Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara amesema wizara hiyo inagusa maisha ya watu ya kila siku na kueleza nia ya Serikali kuwaondoshea wananchi changamoto zote zinazotokana na masuala ya maji, umeme na mafuta.

Pia amesema katika jitihada za Serikali kupunguza kero hizo, inatarajia kuzindua tenki kubwa la maji safi na salama Chakechake Pemba, lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni moja ambalo litakuwa la kwanza kwa ukubwa kwa Zanzibar nzima. 
Naye Mkurugenzi wa masuala ya ushirika wa makampuni ya Bakhresa, Hussein Sufiani ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiasha pamoja na kuwafanikishia mradi wao huo wa Bohari ya Mafuta ya Mangapwani.

Ameihakikishia Serikali kwamba kampuni za Bakhresa zitaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa majukumu yao ya kila siku na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wao. 
Baadae Rais Dkt.Mwinyi alifanya ziara ya kushtukiza kwa kutembelea ujenzi wa mtaro Meli Kumi njia ya Bumbwini, ujenzi wa Soko la Chuini na Soko la Jumbi na Mwanakwerekwe kukagua ujenzi na maendeleo ya miradi hiyo ilivyofikia. Pia alitembelea eneo la waanika dagaa, Mangapwani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news