Waandamana kulaani ukatili wa kijinsia na matendo ya ushoga

NA DIRAMAKINI

BARAZA Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Katavi wamefanya maandamano ya amani lengo likiwa ni kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na matendo ya ushoga.

Maandamano hayo yaliyopita maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi, Machi 22, 2023 yalianzia katika Msikiti wa Nuru uliopo katika mji wa zamani na kumalizikia katika msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Katavi Omary Muna amesema, maandamano hayo ni kuunga mkono juhudi za viongozi wa Serikali pamoja na kumuunga mkono Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zuberi ambapo wanapinga vikali matendo hayo yasiyofaa katika jamii.

“Tunakasirishwa na jambo hili kwa sababu tunatambua hii ni laana ya Mwenyezi Mungu, na pindi jambo hili likiendelea kuenea litatuangamiza wote, tutapoteza vizazi vyetu na hatutopata watu ambao watamtambua Mwenyezi Mungu, wote tutakuwa tumemuiga shetani kitendo ambacho Mwenyezi Mungu amekiharamisha na anakikataa,”amesema.

Naye mgeni rasmi Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu amewataka waislamu na wasio waislamu mkoani humo kuungana na kukemea vitendo hivyo kwa kuwa watu wanaofanya matendo ya ukatili pamoja na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wanaishi nao majumbani na mtaani.

Pia amesema, hawataishia tu kwenye maandamano bali watajitahidi kupita maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi ikiwemo maeneo ya shule na vituo vya kulelea watoto ya yatima ili kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuwa matendo hayo hayakubaliki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news