Waziri Mkuu:Changamkieni fursa kujenga uchumi wa kidijitali

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanawake wote na Watanzania kwa ujumla waendelee kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali.

Ametoa wito huo leo Machi 10, 2023 wakati akizungumza na wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Tano wa Mwanamke Kiongozi kwa mwaka 2023 uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliambatana na mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi ambapo jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti. Washiriki 11 wa Programu hiyo walijidhamini wenyewe na wengine 54 wanatoka kwenye kampuni 29.
Akitoa msisitizo kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo, Waziri Mkuu amesema: "Wanawake wajitokeze kwa wingi kushiriki katika programu hii kwani imeendelea kuwa na matokeo chanya kwa washiriki na kuleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji wao wa kazi na kugusa maisha yao binafsi.

“Pia nitoe rai kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kiendelee kutoa mafunzo haya ya uongozi kwa wanawake pamoja na kuendelea kuwa vinara katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa maeneo ya kazi."

Waziri Mkuu amesema suala la mabadiliko ya kidigitali ni moja ya vipaumbele vya Taifa kwani maendeleo ya uchumi yanategemea sana utandawazi. "Lakini pia katika mabadiliko haya ni muhimu kutambua mchango wa wanawake katika uchumi wetu na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi wa kidijitali."
Amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa uchumi wa kidijitali, imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ambayo itaiwezesha nchi kutumia vema fursa za kiteknolojia zilizopo katika kuinua uchumi.

"Ili kutimiza azma hiyo, tayari Mkakati wa Taifa wa Brodibandi wa Mwaka 2021–2025 ambao utawezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo mwaka 2025 umeshaandaliwa. Serikali inaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali ili kuhakikisha nchi yetu haibaki nyuma katika ulimwengu wa kidijitali."

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Nchi (OWM-Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wataendelea kusimamia sheria za kazi na masuala ya ajira nchini na kuweka mazingira rafiki katika sehemu za kazi.

Akielezea kuhusu suala la kima cha chini cha mshahara kwenye sekta binafsi, Prof. Ndalichako alisema: “Utekelezaji wa Kima cha Chini ulianza tarehe 1 Januari, 2023. Niwasihi ATE iendelee kutoa elimu na kuwasimamia wale ambao bado hawajatekeleza kikamilifu kwani hiyo ni haki ya kila mfanyakazi.”

Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima alisema Serikali ya awamu ya sita imewainua wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa za kiteknolojia na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kupambana na ukatili wa kijinsia. Amesema Serikali imeratibu programu ya kuwezesha wanawake katika maendeleo na mwelekeo wa kidijitali ili wafahamu masuala ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dkt. Saada Salum Mkuya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA) aliiomba ATE iangalie uwezekano wa kupeleka hadi ngazi ya chini zaidi Programu ya Mwanamke Kiongozi ili iweze kuibua vipaji vingi zaidi. "ATE iangalie uwezekano wa kushuka hadi shule za sekondari na vyuo vikuu ili kuibua vipaji vya wanawake wengi zaidi, " alisema.
Naye Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Doran alisema kuwa tangu waanze programu hiyo kwa kushirikiana na ESAMI, wamekwishatoa mafunzo kwa wanawake 274 kutoka kampuni 79 wakiwemo Wabunge na wawakilishi 150.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news