Waziri Prof.Mbarawa atoa maagizo kwa viongozi Sekta ya Uchukuzi, idara na taasisi zake

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka viongozi wa Sekta ya Uchukuzi, idara na taasisi zake kubaini mapungufu ya watumishi na kuyafanyia kazi ikiwemo kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wasiotimiza wajibu wao.
Akizungumza leo Machi 20, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi, Profesa Mbarawa amesema viongozi wa idara na taasisi ni wajibu wao kugundua changamoto za watumishi wa sekta na kuwachulia hatua wale wasiotimiza wajibu wao. 
“Niwaombe viongozi wote wa Sekta ya Uchukuzi na taasisi zake, viongozi wabaini mapungufu yaliyopo kwa watumishi na kufanyia kazi. Aidha tusisite kuchukua hatua kwa watumishi wasiotimiza wajibu wao,”amesema.

Aidha, ametoa rai kwa taaisisi zote zilizopo chini ya Sekta ya Uchukuzi kuhakikisha zinawashirikisha watumishi wao katika kupitia mipango na bajeti za taasisi kabla ya kuziwasilisha kwa msajili wa hazina. 
Katika hatua nyingine, Prof.Mbarawa amezitaka taasisi kuwasilisha michango ya watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kupunguza usumbufu kwa wastaafu ili kuepuka adhabu za tozo inayotokana na ucheleweshaji wa kuwasilisha michango hiyo.

“Taasisi nyingi za umma hazitekelezi wajibu huo na kuichafua Serikali, hivyo kila taasisi ifanye uhakiki na uchambuzi wa madeni ya watumishi hususanI wastaafu na kuainisha mikakati ya kulipa madeni hayo,”amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi, Gabriel Migire amesema sekta yake imejipanga kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na serikali inakamilika kwa wakati.

“Nikuhakikishie tunakwenda kuwa wakali ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa na kukamilika kwa wakati hii itasaidia malengo ya serikali kufikiwa kama ilivyopangwa,”amesema.
Aidha, amesema Sekta ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 inatarajia kutekeleza miradi ya barabara, ujenzi wa Reli ya SGR, bandari, usafiri wa anga, ununuzi wa rada, pamoja na kuboresha vyuo vya mafunzo katika Sekta ya Uchukuzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news