Waziri Ummy:Kagera ipo salama, wananchi msiwe na hofu kuhusu Marburg

NA MWANDISHI WAF

WAZIRI wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kutembelea katika Kijiji cha Ntoma Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kwa lengo la kujionea hali inavyoendelea baada ya kutangazwa kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg mkoani humo.

Katika ziara hiyo, Waziri Ummy ameambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Zabron Yoti pamoja na Mwakilishi wa Shirika la UNICEF, Bi. Shalini Bahuguna.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa sasa hali ni salama na kuwataka wananchi wa kijiji hicho na watanzania kwa ujumla kuondoa hofu kwa kuwa Serikali inawajali wananchi wake.

“Niwatoe hofu Watanzania tuendelee kufanya kazi zetu, lakini tuzingatie maelekezo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kuepuka kushikana mikono hususani kipindi hiki, lakini pia tujitahidi kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni,”amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo unamalizika na hautatokea tena katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kanyangele Bw. Hamim Hassan ameishukuru Serikali kwa kufanya juhudi kubwa ambapo hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyeongezeka kwa kuthibitika kuwa na ugonjwa huo.

“Hatua za Serikali kupitia Wizara ya Afya zilizochukuliwa za kuwaweka sehemu maalumu waliokuwa karibu na wagonjwa imesaidia sana kutoendeleza maambukizi kwingine na hali ni shwari kwa sasa.” amesema Bw. Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news