SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-28

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...kiashiria kingine ni kuvunjwa kwa vyungu juu au pembeni mwa kaburi au kukatwa ama kung'olewa kwa miti ya kaburi upande wa kulia kama mlipanda. Ukiona mambo hayo mojawapo au yote tambua hakuna mtu.

Endelea.

Wazungu hao walikuwa wamelizunguka kaburi hilo huku wakicheza ngoma za kichawi za asili yao. Kulikuwa na makundi mengi ya wachawi ambao waliendelea na shughuli zao za kichawi makaburini hapo.

Jambo la kushangaza, wale wachawi hawakuwa na uwezo wa kuwaona wachawi hao wa kizungu. Ni kundi moja tu la mtoto THE BOMBOM ndiyo walikuwa na uwezo wa kutoonekana na mchawi yeyote huku wao wakiona kila kitu. 

Lile kaburi lililokuwa wamelizunguka wazungu hao lilikuwa limejengwa kwa matofari ya kuchoma kisha likanakishiwa kwa marumaru ya rangi nyeusi.

Kaburi hilo lilikuwa na mwinuko wa wastani toka chini hadi juu, kichwani kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa kwa herufi za kuchonga.

Maandishi hayo yalisomeka BISHOP MACHIMU K. MADAKOGAZA. Kwa haraka haraka mtoto THE BOMBOM na kundi lake waligundua lilikuwa ni kaburi la Askofu wa madhehebu ya kiroho. Kwa kuwa wazungu hawakuwa na uwezo wa kuwaona mahasimu wao, waliendelea na shughuli za kufukua kaburi.

Walimwaga ile dawa yao juu ya kaburi kisha kiongozi wao akanuia maneno fulani, baada ya sekunde kadhaa lile kaburi lilijigawa sehemu mbili kuanzia kichwani hadi miguuni.

Bada ya hapo kiongozi wao alichukua fimbo fulani akaipiga kaburini hapo upande wa pili penye mpasuko. Sanduku lililokuwa kaburini likatoka nje ya kaburi, mzungu huyo alikuwa na usinga wa mkia wa kicheche akaugusisha kwenye sanduku hilo likafunguka.

Ndani ya sanduku hilo kulikuwa na mwili wa binadamu aliyeonekana kusinyaa zaidi, ngozi yake iligandamana na mifupa ya mwili wake.

Kichwa chake kilibaki fuvu tu ambalo lilizungukwa na matundu sehemu ya macho, pua na masikio. Mikono yake ilikuwa imelala chini ya sanduku hilo huku ikiwa imebakia mifupa mitupu, ila sehemu ya mkono wa kushoto kulikuwa na hirizi kubwa nyeusi.

Miguu ya marehemu huyo ilikuwa imesinyaa mfano wa ndizi iliyooza, mguu wa kulia alikuwa na hirizi fulani nyeusi. Shingoni mwake alikuwa na kidani fulani kilichoonekana kung'ara zaidi, wale wazungu baada ya kukiona kidani hicho walishangilia kwa furaha kuu.

Tayari mtoto THE BOMBOM na kundi lake waligundua sababu za wazungu hao kwenda makaburini huko. Lengo lao lilikuwa ni kidani hicho, yamkini kidani hicho kilikuwa na maana kubwa kwa wazungu hao.

Kabla hawajamvua marehemu kidani hicho, mtoto THE BOMBOM aliwahi haraka kumvua marehemu na kukitia mikononi mwake.

Kwa kuwa wachawi hao walikuwa hawana uwezo wa kuwaona kundi la mtoto huyo, akili yao ikawatuma kuwa ilikuwa ni nguvu ya madawa baina yao na kidani hicho.

Ghafla kile kidani kikapotea kabisa machoni mwao, wakabaki wakishangaa maana waliamini kuwa uchawi wao una nguvu kuliko ule wa Kiafrika.

Walimwaga dawa ya kuongeza uoni ili wawe na uwanda mpana wa kuona lililojificha maeneo hayo, lakini hawakufanikiwa kuona chochote.

Kuna muda walihisi labda kulikuwa na wachawi waliokuwa wakiwawangia, wakamwaga aina nyingine ya madawa ili kuondoa hali hiyo lakini mambo yakabaki vilevile.

Ghafla wazungu hao walifanikiwa kumuona mchawi mmoja wa kundi la mtoto THE BOMBOM, huu ulikuwa ni mpango wa makusudi uliofanywa na mtoto huyo.

Wakati hawajachukua maamuzi yeyote yale, yule mchawi alipotea kiaina aina kwenye upeo wa macho yao. Wakaanza kuhaha kumwaga aina mbalimbali za madawa, lakini haikuwasaidia.

Mara wakafanikiwa kuona mkono uliokuwa umeshika kidani, mkono huo ulikuzwa na kuonekana kama wa mtu mzima wakati ulikuwa ni wa mtoto huyo.

Wachawi hao wa kizungu wakabaki wakishangaa, tayari ukweli juu ya kidani hicho walikuwa wameshaelewa. Walikuwa wamezidiwa ujanja na mchawi mwingine ambaye hawakuwa wakimfahamu, ghafla ule mkono wenye kidani ulipotea.

Kabla hawajachukua maamuzi yoyote, walishangaa kuona jiwe kubwa linatua kichwani mwa kiongozi wao. Lilikuwa ni jiwe kubwa lililompeleka chini kiongozi huyo wa wachawi wa kizungu, pale chini akawa anarukaruka mithili ya mbuzi aliyechinjwa.

Taharuki ikawavaa wachawi hao, wakati huo kundi la mtoto nabii lilikuwa likifurahishwa na taharuki hiyo. Jiwe alilopigwa mzungu huyo liliondoa meno yake ya mbele, huku pua yake ikiwa imesokomezwa kwa ndani.
Walimchukua kiongozi wao kisha wakaondoka, lilikuwa ni pigo kubwa kwa upande wao maana aliyefanyiwa unyama huo alikuwa ni kiongozi wao.

Katika harakati ya kuondoka eneo hilo walimsahau yule mateka waliyekuwa naye toka awali. Walijisahau pia hata kurudisha lile sanduku la yule marehemu kaburini.

Kundi la mtoto huyo, walilirudisha sanduku hilo kaburini kama ulivyokuwa awali, kisha wakamchukua yule mateka aliyeachwa na wale wachawi wa kizungu.

Mpaka hapo ilikuwa ni saa nane na dakika sita za usiku, bado kulikuwa na muda wa kutosha kuendelea na shughuli zao.

Pembeni kidogo mwa sehemu walipokuwa wamesimama, kulikuwa na jamaa wawili waliokuwa wakiendelea na shughuli zao. Watu hao hawakuwa wachawi wala waganga, walikuwa bize na shughuli iliyokuwa imewapeleka

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji si wote ambao huenda makaburini wakati wa usiku ni wachawi. Yapo makundi mbalimbali ambayo huenda makaburini wakati wa usiku kufanya shughuli zao.

Waganga ni kundi la kwanza ambao huenda eneo hilo kwa shughuli maalumu, shughuli hizo ni pamoja na kuchukua vizimba kwa ajili ya mchanganyo wa dawa zao, kutibu watu pamoja na shughuli mbalimbali.

Kundi la pili ni wachawi wenyewe, hakuna mchawi ambaye hajawahi kufika makaburini. Eneo hili ndiyo sehemu mojawapo ya kufanyia kazi zao, baadhi ya vizimba hupatikana makaburini.

Wapo baadhi ya watu ili umloge ni lazima uende kwenye kaburi la babu au bibi yake mzaa baba, kule kuna dawa ambayo humwagwa kwa ajili ya kuweka mambo sawa dhidi ya mhusika.

Pia wachawi huenda makaburini kucheza ngoma zao, baadhi ya uchawi wao huwalazimisha kucheza ngoma juu ya kaburi la mtu.

Lakini pia wachawi huenda makaburini kwa ajili kufukua maiti kwa malengo tofauti tofauti. Kundi la tatu ambao huenda makaburini ni wagonjwa ambao huambatana na waganga, wao huwa na muda maalumu siyo kila muda huenda kule kwa ajili ya matibabu. Na kundi la mwisho ni wafanyabiashara wa viungo vya binadamu.

Kwa kuwa wale wazungu walikuwa wameshaondoka maeneo hayo, kundi la mtoto huyo liliwasogelea wale jamaa wawili waliokuwa wakiendelea na shughuli zao.

Kulingana na nguvu za madawa waliyokuwa nayo hakuna mtu engeliweza kuwaona kundi la mtoto huyo. Wale jamaa walikuwa wamefukua maiti mbili ambazo moja ilikuwa na siku mbili toka izikwe na nyingine ilikuwa imezikwa siku hiyo.

Kila mmoja alikuwa bize na shughuli yake huku wakiwa kimya, kwa haraka haraka mtoto THE BOMBOM alibaini kuwa jamaa walikuwa wauzaji wa viungo vya binadamu.

Mmoja alikuwa akishughulikia kukata nyeti za maiti wa kiume, japo zilikuwa zimevimba yeye hakujali aliendelea na kazi yake.

Jamaa huyo alifanikiwa kutoa zakali na korodani na kuziweka kwenye kijimfuko chake. Baada ya hapo alizitoa pamba zilizowekwa mdomoni kwa maiti huyo kisha akajaribu kuutanua mdomo ukashindikana.

Akatoa kifaa fulani mfano wa nyundo kwenye mkoba wake wa vifaa, akamtwisha nyundo moja ya nguvu maiti huyo taya zikapishana.

Akachukua kamba fulani ya nailoni akaufunga ulimi wa maiti huyo kisha akasimama mgogoni mwa maiti na kuanza kuuvuta ulimi huo. Hakuwa na huruma hata kidogo juu ya kazi aliyokuwa akiifanya maeneo hayo.

Ulimi ule ulianza kuvutika huku ukitoka nje ya mdomo wa maiti huyo, alipotosheka na urefu wa ulimi huo alichukua panga lenye ncha kali akaukata mara moja.

Ulimi ulipokatika aliuchukua na kuuhifadhi kwenye kijimkoba chake, wakati watu hao wakiendelea na shughuli zao mtoto THE BOMBOM na kundi lake walikuwa wakishuhudia hatua kwa hatua.

Baada ya kuutoa ulimi alichukua kisu na kukata ziwa la maiti huyo la upande wa kulia kisha akaliweka kwenye mfuko wake.

Akatoa pia koromeo, makalio, vidole na masikio. Namna alivyokuwa akivitoa viungo hivyo hakuwa anasumbuka hata kidogo, ilionesha haikuwa mara yake ya kwanza katika shughuli hiyo.

Yule mwenzake alikuwa anashughulika na maiti wa kike, maiti huyo alikuwa kazikwa siku hiyo. Inavyosemekana alifariki wakati yupo kwenye hekaheka ya kujifungua, wakati umauti unamfika alikuwa bado hajatoka mtoto nje.

Kwa kuwa alijifungulia zahanati hawakuweza kumpasua ili kumtoa mtoto huyo, kwa hiyo mwanamke huyo alizikwa akiwa na mtoto wake tumboni.

Hili ni dili kubwa kwa wachawi pamoja na wauzaji wa viungo vya binadamu. Ndiyo maana yule jamaa alipomfukua maiti huyo jambo la kwanza ilikuwa ni kumpasua mama huyo na kutoa kichanga.

Kichanga cha namna hiyo hutumika zaidi kama kizimba kwenye mazindiko ya aina mbalimbali. Hutumiwa kuwanyamazisha watu wanaokusakama, kwa jambo lolote ulilowafanyia.

Mara nyingi ni katika siasa na maofisini, pia upande wa kesi na kashfa mbalimbali. Lakini pia katika masuala ya kichawi hutumika kukamua mafuta ambayo huwa na kazi mbalimbali za kichawi.

Maziwa ya mama huyo yalikatwa na kuweka kwenye mfuko, ni kizimba kizuri kwenye mvuto wa biashara. Sehemu za siri za mama huyo zilikatwa na kuondolewa eneo lake la asili, hivi ni vizimba kwenye shughuli za kiganga na kichawi. Jamaa walikuwa bize kweli kweli, walikuwa na roho ngumu.

Mtoto THE BOMBOM na kundi lake waliachana na jamaa hao wakaamua kuendelea na safari yao. Walirudi na barabara kuu iendayo makaburini, kabla hawajafika kwa Mzee Mashikolo waliingia kushoto na kuachana na barabara ya mawe inayoshuka hadi kwa Mzinza.

Walipita Parokiani maana Kanisa la Roman Catholic na Majengo ya Parokia yapo sehemu mbili tofauti. Baada ya kuvuka parokia kwa mbele yake upande wa kulia walilivuka kanisa la Waadventist Wasabato kisha wakashuka kijimlima hadi mtaa wa Kilimo.

Waliachana na barabara iendayo Muhandu na Kakebe wakaifuata ile iendayo Shule ya Msingi Igoma. Walipofika shuleni hapo waligundua kulikuwa na sherehe kubwa ya wachawi. eneo la uwanja wa shule lilifurika idadi kubwa ya wachawi.

Madarasa ya shule hiyo yalitumika kupikia chakula na kuhifadhia maji, kulikuwa na pombe nyingi za kienyeji pamoja na nyama.

Eneo lote lilikuwa jeupe utadhani mchana kweupe, viganja vya watoto vilikuwa vimezingira eneo lote na kutoa mwanga wa kutosha.

Hata kama ungeliangusha punje ya ulezi au ya mbegu ya mchicha ungeliiona kwa urahisi. Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji kwa kiasi kikubwa mwili wa binadamu una umeme wa asili.

Sehemu za mwili za binadamu zenye umeme mwingi ni viganja na nyayo zake. Hata hivyo ukubwa wa umeme hutofautiana kutoka rika moja kwenda jingine, kwa upande wa watoto wachanga ndiyo huwa na umeme mkubwa kuliko binadamu yeyote.

Watoto hao huchukuliwa kichawi kisha viganja vyao hukatwa na kuchanganywa na madawa mengine ili kutoa mwanga huo.

Kiuhalisia mwanga huo ni mkali zaidi ya kurunzi la basi, huweza kumulika eneo kubwa kuliko balbu tunazozitumia majumbani.

Taa hizi mara nyingi hata watu wa kawaida wamewahi kuziona, lakini ni ngumu sana kung'amua mpaka uelezwe. Taa hizi ndizo hutumiwa na wachawi katika shughuli zao, kuna muda unaweza kuona taa za gari kwa mbali sana nyakati za usiku. Ile siyo gari bali ni wachawi wanaendelea na shughuli zao, hizo siyo taa za gari bali ni umeme wa kichawi.

Ukiona taa nyingi zinawaka nyakati za usiku sehemu ambapo kwa asili hakuna majumba eneo hilo juwa ni umeme wa kichawi.

Ukiuona umeme huo uko eneo mbali sana na eneo ulilopo wewe, basi tambua umeme huo uko mazingira ya karibu sana na ulipo.

Ikitokea ukaona umeme huo upo karibu na mazingira uliyomo basi tambua umeme huo uko kilomita nyingi sana toka uliposimama. Hii ni kanuni za kichawi katika umeme huo, viganja hivyo hutoa mwanga mkubwa sana.

Mara nyingi shughuli au sherehe za kichawi hufanyika mazingira ya namna hii, wachawi walikuwa bize na ngoma zao. Wapo waliokuwa wamelewa chakari na pombe ya kienyeji, nyama zilikuwa nyingi kuliko maelezo.

Ndugu msomaji unapaswa kujua imani ya kichawi ina nguvu kubwa kuliko imani za makanisa yenu au misikiti. Maeneo ya makanisa au misikiti ndiyo hutumiwa kwa kiasi kikubwa na wachawi hao katika shughuli zao.

Baadhi ya misukule huhifadhiwa mashuleni, misikitini na makanisani, hutegemeana na uwezo wa wachawi wenyewe. Dawa mbaya za kichawi hazihifadhiwi ndani maana ni hatari, kwa hiyo zipo zinazohifadhiwa kando kando ya mto, porini, makanisani na misikitini au mapangoni.

Mtoto THE BOMBOM na kundi lao walitaka kuona nguvu za wachawi hao, walimtuma mchawi mwenzao kwenda kuchukua chungu cha nyama walichokuwa wanakula viongozi wao.

Yule mchawi aliwasogelea wachawi hao kisha akachukua chungu hicho, wale wachawi hawakugundua hata kidogo maana waliendelea kuchota mchanga na kula wakijua ni nyama ndani ya chungu.

Kwa mbali kidogo walifanikiwa kumuona mganga mmoja aliyekuwa amezamia kwenye sherehe hiyo ya wachawi. Wale wachawi walioandaa sherehe hiyo hawakuwa na uwezo wa kumuona, japo yeye alikuwa akiwachezesha sherehe apendavyo.

Mganga huyo alikuwa amekwama kwa mtoto THE BOMBOM na kundi lake, wao waliweza kumuona lakini yeye hakuweza.

Waliamua kumchezea kama alivyokuwa akiwafanyia wenzie, wakati anatembea walimuwekea gogo kwa mbele yake akaliparamia na kudondoka chini.

Kundi la mtoto huyo wakawa wanamcheka mganga huyo aliyekuwa akijifanya mjanja, wakati anasimama akakutana na kofi shavuni kwake akadondoka chini.

Akachomoka mbio kuelekea nyumbani kwake, lengo lake ilikuwa kujinisuru na dhahama iliyokuwa mbele yake. Alipofika kwa mbele kidogo alipigwa mtama akajibwaga chini mithili ya furushi la magimbi.

Ndugu msomaji mtoto THE BOMBOM yupo kwenye sherehe ya kichawi ambayo haimhusu, lakini wamekutana na mganga aliyekuwa amezamia sherehe hiyo.

Unadhani nini kitampata? Je, wale wazungu wamefurahishwa na kitendo kilichowapata pale makaburini? Je, watanyamaza au watalipa kisasi? Tafadhali endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

MADELA MINZA?

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news