Waziri Mkuu atoa agizo kwa watendaji wa halmashauri

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezielekeza halmashauri zote nchini zihakikishe maeneo yote yanayotwaliwa kutoka kwa wananchi yanalipiwa fidia kwa wakati ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza siku za usoni.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma leo Juni 28, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na ya jiji la Dodoma ya kutolipwa fidia baada ya maeneo yao kutwaliwa na halmashauri ya jiji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Juni 28, 2023 wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo umeahirishwa hadi Agosti 29 mwaka huu.

Amesema, mahitaji ya uendelezaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kuanzisha makazi yameendelea kuongezeka. “Ongezeko hilo ni muhimu likazingatiwa katika upangaji wa miji yetu hapa nchini.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza halmashauri zote kupima maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo viwanja kwa ajili ya makazi badala ya kuacha wananchi kujenga kiholela.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaelekeza Maafisa Masuuli waimarishe usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024.

Pia, Waziri Mkuu amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali zifanye vikao kwa njia ya mtandao bila kuathiri tija ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za umma na gharama zisizo za lazima za uendeshaji wa vikao vya Serikali.

“Watendaji wa Serikali, imarisheni ukusanyaji wa mapato na kufanya matumizi kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2023/2024 sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Serikali wazingatie kanuni, sheria na taratibu katika manunuzi na matumizi ya fedha za umma ili kufikia shabaha na malengo ya uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news