BoT kuja na mfumo mpya wa utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia riba za benki kuu

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeueleza umma kuwa, katika jitihada za kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa Sera ya Fedha, inatarajia kubadilisha mfumo wa sasa wa utekelezaji wa sera ya fedha.

Mfumo ambao unatumia ujazi wa fedha, na kuanza kutumia mfumo mpya unaotumia riba ya Benki Kuu (Central Bank Policy Rate) katika kusimamia malengo mapana ya kiuchumi ya kudumisha utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi kuanzia mwezi Januari 2024.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa leo Juni 28, 2023 na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba ambapo imefafanua kuwa, mfumo huu ulianza kutumika duniani mwaka 1990 ambapo hadi sasa unatumiwa na Benki Kuu za nchi 45.

"Utekelezaji wa Mfumo wa Riba ya Benki Kuu umeonesha matokeo mazuri katika usimamizi wa sera ya fedha na kuimarisha misingi ya utekelezaji wake katika mazingira ya uwazi katika nchi zinazotumia mfumo huu.

"Maelezo na ufafanuzi zaidi kuhusu mfumo huu mpya wa sera ya fedha yameambatishwa na taarifa hii kama Kiambatisho Na. I.

"Aidha, maelezo ya ziada yanapatikana pia katika Tamko la Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania ya 2023/24 na Tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania: www.bot.go.tz/Publications/Filter/48?lang=sw
 
Kwa muktadha huu, ili kuhakikisha kuwa mabadiliko haya yanafanyika kwa ufanisi, Benki Kuu ya Tanzania imeandaa Mwongozo wa utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia riba ya Benki Kuu ambao umeambatishwa na taarifa hii kama Kiambatisho Na. II.

"Madhumuni ya Mwongozo huu ni kutoa taarifa muhimu kwa wadau ili kuongeza uelewa kuhusu sera ya fedha, hatua na taratibu zinazohusika katika mfumo mpya wa sera ya fedha kwa kutumia riba.

"Mwongozo huu utasaidia kutoa ufafanuzi kuhusu uandaaji na utekelezaji wa sera ya fedha ili kuwezesha wadau kupangilia shughuli zao na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera ya fedha.

"Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya mfumo mpya wa sera ya fedha na hivyo kuwezesha kufikia malengo ya sera ya fedha ya kudumisha utulivu wa bei na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi,"imefafanua sehemu ya taarifa iliyotolewa na Gavana Tutuba leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news