Rais Dkt.Samia abadilisha jina la CFR kuwa Dr. Salim Ahmed Salim Centre for Foreign Relations

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amekibadilisha jina Chuo cha Diplomasia nchini na kukipa jina la Waziri Mkuu Mstaafu Dkt.Salim Ahmed Salim.

“Na kwa sababu mcheza kwao hutunzwa, na tumesema alikuwa mwanadiplomasia mahiri, tumekubaliana kukipa Chuo kile cha Diplomasia jina na sasa rasmi kitakuwa kinaitwa Dr. Salim Ahmed Salim Centre for Foreign Relations.”

Aidha, Rais Dkt.Samia amesema lengo la kukipa jina hilo ni kuonesha mchango uliotolewa na mwanadiplomasia Dkt. Salim ambae alifanya kazi kwa muda mrefu katika nyanja ya kidiplomasia ya kimataifa kwa nidhamu bila kukata tamaa.

Rais Dkt.Samia amesema hayo leo Septemba 30,2023 kwenye hafla ya uzinduzi wa tovuti ya nyaraka za Dkt.Salim Ahmed Salim, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

Mheshimiwa Rais Samia amemuelezea Dkt. Salim kama kiongozi aliyethamini elimu katika jamii na aliyesaidia watu wengi kufikia maendeleo na ndoto zao kwa kutoa ushauri na mafundisho mbalimbali.

Rais Samia ameeleza kuwa katika uongozi wake, Dkt. Salim alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa masuala ya uzalendo, muungano na umoja ambao yalichangia katika kudumisha amani na umoja wa taifa.

Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wa umma kuiga mfano wa Dkt. Salim kwa kutunza kumbukumbu za maisha yao kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadae ili zisaidie kukuza na kuimarisha uelewa wa juhudi za kila kiongozi, historia ya nchi na Bara la Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news