Tunahitaji wawekezaji wengi Sekta ya Uchumi wa Buluu-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar bado ina mahitaji makubwa ya uwekezaji kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu kupitia Utalii, Uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya samaki, Bandari, Mafuta na gesi pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 4, 2023 Ikulu jijini Zanzibar alipozungumza na mabalozi wateule waliofika kujitambulisha, kupokea nasaha pamoja na kuaga kuelekea vituo vyao vya kazi kwenda kuiwakilisha Tanzania Kimataifa.

Rais Dkt. Mwinyi aliwasihi mabalozi hao kuzichangamkia fursa za uwekezaji huko kwenye vituo vyao vya kazi na kuzileta nchini ili kuiimarisha Utalii wa Zanzibar ambao nitegemeo kwa uchumi wa nchi unaochangia asilimia 30 ya pato la taifa.

Aliwataka mabalozi hao kuangalia zaidi soko jipya la utalii mbali na kutangaza utalii wa fukwe na Urithi lakini pia kuangalia fursa mpya za utalii wa mikutano, michezo na uwekezaji ili kuitangaza zaidi Zanzibar na kuiingiza watalii wengi wa maeneo mengine ya dunia ikiwemo China ambayo ina watalii wachache Afrika.

Kuhusu sekta ya Uvuvi na ufugaji wa samaki, Rais Dkt.Mwinyi aliwataka mabalozi hao kuitangaza zaidi fursa hiyo pamoja na kutafuta wawekezaji na masoko ya kilimo cha Mwani ambapo Zanzibar inaongoza kwa kuzalisha mwani Afrika.

Pia aliwataka mabalozi hao kuangalia fursa ya masoko ya bidhaa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ikiwemo mazao ya viungo.

Rais Dkt. Mwinyi pia aliwaelekeza mabalozi hao kuzichangamkia fursa za fedha, mitaji na mikopo pamoja na kuimarisha ushirikiano mwema kwa nyanja zote zikiwemo elimu ili kubadilishana uzoefu baina ya Tanzania na mataifa wanayokwenda kuiwakisha huko duniani.

Sambamba na hayo pia Rais Dkt.Mwinyi aliizungumzia fursa ya Bandari jumuishi kwa Zanzibar kwa sasa inahitaji Bandari kubwa ili kukidhi mahitaji ya uchumi wake kama kituo muhimu cha usafirishaji, usambasaji wa bidhaa na kutoa huduma na kufanyia biasha ikiwemo kupokelea mizigo, kusafirishia mazao, na mahitaji mbalimbali ikiwemo mafuta, nafaka, na kukuza uchumi wake.

Akizungumzia suala la mafuta na gesi pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini, Rais Dk. Mwinyi alieleza Zanzibar inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta hiyo ili kuimarisha sekta ya biashara na uchumi wake kupitia bandari za Zanzibar, Pemba, Tanga, Dar es Salaam, Mtwata, mengine wakiwemo Msumbiji, visiwa vya komoro na kwengineko.

“Zanzibar inahitaji vyombo vya usafiri wa majini kwa safari za Pemba, Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na kwengineko kama Msumbiji, Komoro na sehemu nyengine za visiwa nilizonungukwa na bahari kwa maeneo karibu, Uchumi wa Buluu umejikita kwenye maeneo mengi ya uchumi unahitaji wawekezaji,”alisisitiza Rais Dkt.Mwinyi.

Hata, hivyo Rais Dk. Mwinyi aliwataka Mabalozi hao kuendelea kuimarisha ushirikiano mzuri na kuimarisha ujirani mwema uliopo kwa watakaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi jirani sambamba na kuwaahidi ushirikiano mzuri mabalozi hao baina yao na Serikali ya SMZ ili kutekeleza vyema majukumu ya kazi zao.

Kwa upande wao mabalozi hao walimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuzifanyia kazi nasaha na maelekezo aliyowapa wakati wote wa utumishi wao na kumuahidi kuchangamkia vyema fursa zilizomo kwenye maeneo yao ya kazi kwa lengo la kuendelea kuiimarisha Diplomasia ya Uchumi na kuiendeleza kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Buluu.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenziwe, Balozi Khamis Mussa Omar anaekwenda kuiwakisha Tanzania jijini Beijing, China alimuahidi Rais Dkt. Mwinyi mbali na kuzichangamkia fursa za uchumi na uwekezaji kwenye vituo vyao vya kazi alimuhakikisha Rais Dk. Mwinyi watakwenda kuboresha zaidi uhusiani na ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na mataifa hayo pia kuimarisha ujirani mwema wa Mabalozi wa vituo vilivyopo kwenye nchi jirani kwa kuhakikisha wanasimamia usalama wa nchi na kukuza uchumi na biashara baina yao.

Mabalozi wengine ni Balozi Hassan Mwamweta anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani na mataifa ya Bulgaria, Czech, Hungary, Old Swiss, Poland, Slovakia na Switzerland.

Wengine ni Balozi, Habibu Awesu Muhamed anaekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Qatar, Balozi Mohamed Juma Saudi Arabia, Imani Njikai Algeria, Balozi Meja Jenerali Ramson Mwaisaka atakaeiwakilisha Tanzania nchini Misri, Balozi Gelasuis Byakanwa ataiwakilisha Tanzania nchini Burundi na Balozi Dk. Benard Kibesse ataiwakilisha Tanzania jijini Nairobi, Kenya

Mabalozi hao nane waliapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan Agosti 16 mwaka huu baada ya kuwateua kushika nafasi hizo Mwezi Mei mwaka huu.

Wakati huo huo Rais Dkt.Mwinyi alizungumza na Mkuu wa Jeshi kutoka nchini India, Jenerali Manoj Pande na ujumbe wake wa watu watano waliofika Ikulu jijini Zanzibar kumtembelea.

Katika mazungumzo yao Rais Dkt.Mwinyi aliueleza ujumbe huo uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na India na kushirikiana kwenye masuala mbalimabli ikiwemo ulinzi na usalama, masuala ya uchumi na huduma za jamii ikiwemo elimu, maji na teknolojia.

Alisema, Ubalozi Mdogo wa India uliopo Zanzibar umekua na ushirikiano mzuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kushirikiana kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayoletwa Zanzibar na nchi hiyo.

Naye Jenerali Manoj alisema, mbali na ushirikiano uliopo baina ya India na Tanzania pia aliisifu Zanzibar kwa kuwa nchi ya kwanza duniani kuweka Taasisi ya Teknolojia ya IIT ya India na kutoa huduma kwa Watanzania na wasio watanzania watakaofika Zanzibar kupokea huduma za chuo hicho.

Pia Mkuu huyo alisifu Zanzibar kwa ukarimu wa watu wake na kueleza kuvutiwa kwake na utamaduni wa Wazanzibari.

Uhusiano wa diplomasia uliopo baina ya Tanzania na India ni wa historia ambapo India ilifungua Ubalozi wake, Dar es Salaam mwezi, Novemba mwaka 1962 na mwaka 1974 India ilifungua ubalozi mdogo Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news