DCEA yafichua dawa za kulevya zinavyosababisha vilio katika jamii

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewataka Watanzania kujiepusha na matumizi ya aina zote za dawa za kulevya kwa kuwa zina madhara katika nyanja zote za kijamii ikiwemo kiafya.
Pia, imewataka wale ambao wanajihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja, kwa kuwa mkono wa Serikali ni mrefu na unafika popote na kwa wakati.

Wito huo umetolewa Novemba 13, 2023 na Kamishna Msaidizi wa Kinga na Huduma za Jamii-DCEA, Moza Makumbuli wakati akiwasilisha mada ya aina za dawa za kulevya, sababu za matumizi na madhara yake katika jamii.

Kamishna Makumbuli alikuwa anawasilisha mada hiyo katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyoratibiwa na mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.

Amesema, bangi ni dawa haramu inayoongozwa kwa kupatikana na kutumiwa zaidi nchini ikifuatiwa na heroin, mirungi na cocaine na hivi karibuni methamphetamine.

Kamishna huyo amesema, bangi ni miongoni mwa vileta njozi ambayo humfanya mtumiaji kuhisi, kuona na wakati mwingine kusikia vitu visivyokuwepo au tofauti na uhalisia.

Pia, amefafanua kuwa, dawa za kulevya ni kemikali ambazo ziingiapo mwilini huathiri ubongo wa mtumiaji na kumsababishia kuwa na matendo, hisia, fikra na muonekano tofauti na matarajio ya jamii.

Amesema, kemikali hizo hutokana na mimea na madini ambayo ni mali ghafi muhimu kwa mahitaji mengine ya mwanadamu.

“Dawa za kulevya huwa zinaenda kuvuruga mfumo mzima wa fahamu na kubadilisha namna ambavyo ubongo unafanya kazi, kwa hiyo mtu anakuwa na fikra, hisia na tabia tofauti.

“Suala la bangi ni mtihani, inaonekana wengi wanatumia, hata ukiangalia habari mfano ile ya biskuti za bangi mtandaoni comments za watu ni kama vile wanaona bangi inachelewa kuhalalishwa, bangi haifai tujiepushe kutumia,"amefafanua.

Kamishna Makumbuli amebainisha kuwa, katika jamii, kukiwa na matumizi makubwa ya dawa za kulevya matukio ya uhalifu huwa yanaongezeka.

Pia, kukosekana kwa haki kutokana na rushwa kutamalaki miongoni mwa jamii, kwani wauzaji huwa wanatumia rushwa kunyamazisha baadhi ya watu ili kuendelea kutekeleza uhalifu wao.

“Vile vile, dawa za kulevya ni chanzo cha biashara haramu ya binadamu ambapo wafanyabiashara wengi huwa wanatumia watu kama mali kauli, kwa kuweka watu rehani.Pia, watumiaji wa dawa za kulevya huwa hawaajiriki na ni vigumu kuajiriwa.

“Kama ni mwanafunzi shule inaisha. Ukiwapa nafasi hao watu, unakuta uchumi unahodhiwa na watu wachache, kwa hiyo mtu mmoja anakuwa anapata fedha za maana huku wengine wakiendelea kuteseka, wauza dawa za kulevya huwa wanahodhi fedha na mali nyingi na wana uwezo wa kununua mali zozote,"amesisitiza Kamishna huyo.

Ameitaka jamii kutambua kuwa, vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya wananchi na mamlaka za Serikali hususani DCEA ili kuhakikisha kuwa, jamii na Taifa linaendelea kuwa salama.

Kamishna huyo ameitaka jamii kutambua kuwa, pale ambapo dawa za kulevya zinatamalaki katika jamii, Taifa huwa linatumia fedha nyingi ambazo zinapaswa kwenda katika miradi mingine ya maendeleo kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu kwa waraibu na kuendesha taasisi.

"Hivyo, kwa umoja wetu tuendelee kushirikiana kwa kuhakikisha tunawafichua wale ambao wanajihusisha na biashara za dawa za kulevya katika jamii zetu, ukiwa na taarifa unaweza kutumia namba 119 kupiga bure na taarifa zako zitapokelewa kwa usiri mkubwa, dhamira ikiwa ni kuiokoa jamii dhidi ya dawa za kulevya."

Vile vile, Kamishna huyo amesema, pale ambapo biashara ya dawa za kulevya inashamiri katika jamii,mazao na biashara halali huwa haziwavutii tena watu badala yake wanajikita katika biashara ya dawa za kulevya, hivyo kunakuwa na umaskini mkubwa katika jamii.

Kwa upande wa kimazingira, amesema wale ambao wanajihusisha na kilimo mfano cha bangi huwa wanakata miti, kuharibu vyanzo vya maji kwa ajili ya kufanikisha kilimo hicho haramu kwa manufaa yao.

Pia, amesema wanaojidunga sindano ambao mara nyingi huwa na VVU na homa ya manjano huwa wanazitupa ovyo, jambo ambalo ni hatari kwa afya na mazingira.

"Na wakati mwingine, hao wafanyabiashara wa dawa za kulevya huwa na nguvu za kisiasa ambapo hufanya maamuzi ni kiongozi wanataka akae madarakani na wanawea kumuondoa."

Hata hivyo, Kamishna Makumbuli amewataka vijana kujikita zaidi katika stadi za maisha kwa kujiepusha na makundi mbalimbali, kujiepusha na tamaa ya vitu na kujihusisha na dini.

Dkt.Mfisi

Naye Kamishina wa Kinga na Tiba wa mamlaka hiyo, Dkt.Peter Mfisi amesema, Watanzania mbalimbali wamekuwa wakikamatwa katika mataifa mbalimbali kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya ingawa hawana takwimu rasmi za walionyongwa.

Dkt.Mfisi katika semina hiyo alikuwa akiwasilisha mada ya afya ya akili na dawa za kulevya ikiwemo tiba kwa waraibu sambamba na ijue Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

"Mamlaka tunachoweza kueleza hatuna takwimu za idadi ya watanzania ambao wamenyongwa kwa sababu ya kukamatwa na dawa za kulevya nje ya Tanzania.Tunazo takwimu zinazonesha watanzania 1200 wamekamatwa kwa dawa za kulevya nje ya Tanzania."

Akijibu swali la wapi watuhumiwa wa dawa za kulevya wanakamatwa kati ya Tanzania na nchi nyingine amesema, kwa Tanzania watu wengi wanakamatwa kwa dawa mbalimbali za kulevya huku akitoa mfano kwamba watu 800 wamekamatwa nchini katika siku za karibuni.

Kamishna Dkt.Mfisi akijibu swali la kwa nini Serikali isiruhusu kilimo cha bangi ili kuuza nje ya nchi kuwezesha Taifa kupata kipato amesema,kuhalalisha kilimo hicho haramu sio jambo rahisi.

Amesema, nchi ambazo zimeruhusu kilimo cha bangi wameweka utaratibu ukiwemo wa bangi kulimwa katika green house ili kukidhi ubora unaohitajika katika soko lao.

"Bangi yetu inalimwa katika maeneo ambayo hayako katika utaratibu, hivyo hata kuuza katika sokoni haiwezekani lakini nchi ambazo zinaruhusu kilimo hicho wameweka vigezo vinavyotakiwa.

"Vile vile,nchi ambazo zimeruhusu kilimo cha bangi au kutumia bangi wameweka na umri ili kuepusha watoto kuvuta.Mtoto mdogo ubongo wake unaendelea kukua, hivyo akivuta bangi kunamsababisha athari, ndio maana mtoto hawezi kuruhusiwa kutumia,"amesema Dkt.Mfisi.

Pia, amesema si bangi zote zinatumika kutengeneza dawa, bali zipo bangi ambazo zimekidhi viwango vinavyotakiwa.

"Hata hivyo takwimu zimebainisha nchi zilizohusu kilimo cha bangi zimebainika kuongezeka kwa matukio ya uhalifu pamoja na afya ya akili,"amesema Dkt.Mfisi.

Akizungumzia kuhusu kuteketekeza dawa za kulevya kama heroin, bangi, mirungi na cocaine, Dkt.Mfisi amesema, uteketezaji wa dawa hizo uko kwa mujibu wa sheria ambayo inaeleza jinsi ya kuziteketeza.

Kamishna huyo amefafanua kwamba, baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Kenya na Somalia zimekuwa zikitimika kama mapito ya kupitisha dawa za kulevya kuelekea Ulaya na mataifa mengine.

Wakati huo huo,Kamishna Dkt.Mfisi amesema, mamlaka hiyo inajivunia weledi mkubwa walionao watumishi wa wake jambo ambalo linawezesha kutekeleza majukumu yao kwa usiri na mafanikio yoyote bila kushawishiwa na mtu yeyote.

“Watendaji wa mamlaka yetu wanawezeshwa vizuri kutimiza majukumu yao, ndiyo maana wapo makini na hawashiriki vitendo vya rushwa,"amebainisha Kamishna Dkt.Mfisi licha ya kukiri kuwa, wauzaji wa dawa za kulevya wana mbinu nyingi ikiwemo kutaka kutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kufanikisha uhalifu wao.

Amesema, DCEA ni mamlaka inayojumuisha watumishi kutoka vitengo mbalimbali muhimu vya Serikali, hivyo kila mmoja anatimiza wajibu na jukumu lake kwa weledi na ufanisi ili kulinda kibarua chake.

Kamishna Machibya

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ukaguzi na Sayansi Jinai, Siliwa Machibya amesema, bila kemikali bashirifu hakuna dawa za kulevya.

Machibya alikuwa akiwasilisha mada ya kemikali bashirifu na udhibiti wake katika semina hiyo ambapo amesema, kemikali ambazo zinachepushwa na watu ambao si waaminifu zimekuwa zikitengeneza heroin, cocaine,bangi za kutengeneza, mirungi na nyinginezo.

"Hizi ni kemikali zenye matumizi ya kawaida katika kutengeneza bidhaa mbalimbali viwandani, lakini kemikali hizo zikichepushwa huweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya.

"Hivyo kwa pamoja ndugu zetu wanahabari na wahariri tujikite sana kuelimisha jamii kuhusu kemikali hizi ili kuepusha uzalishaji wa dawa za kulevya.Kemikali bashirifu siyo nzuri, lazima zidhibitiwe,"amesema Kamishna huyo.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia DCEA, Florence Khambi amesema kuwa, lengo la semina hiyo ambayo ni mara ya pili kukutana na wahariri ni kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu dawa za kulevya.

“Katika kuhakikisha umma wa Tanzania unapata elimu kuhusu dawa za kulevya, katika kufanikisha hili mamlaka imeona ni muhimu kuvishirikisha vyombo vya habari hapa nchini.

“Kwani tunaamini kuwa ninyi ni wadau muhimu katika kuunganisha daraja la jamii katika kupata elimu kuhusu dawa za kulevya.

“Hivyo, ni vyema mkapata uelewa huu kuhusu dawa za kulevya ili kuweza kutoa elimu sahihi kwa jamii na taarifa itafika kwa umma kama ilivyokusudiwa,”amefafanua Bi.Khambi.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news