REA yaendelea kubisha hodi maeneo ya Delta na visiwani

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesema kuwa,inatekeleza mradi wa kupeleka umeme katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa nchini.

Hayo yamesemwa Novemba 23, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati mbadala na Jadidifu wa REA, Mhandisi Advera Mwijage katika kikao kazi kati ya wakala huo na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mhandisi Mwijage amesema, mradi huo unajumuisha ujenzi wa mifumo midogo ya kusambaza umeme katika maeneo yenye vyanzo vya nishati jadidifu kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji.

Pia, amesema mikataba miwili ya mradi wa Ikondo-Matembwe Hydro Power ulisainiwa mwezi Februari mwaka huu na mkataba wa mradi wa Mwenga Hydro Power ulisainiwa mwezi Machi mwaka huu.

Amesema kuwa miradi hiyo itaunganisha jumla ya wateja wa awali 2,168 katika vijiji 42 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.06.

"Tunayo maeneo ambayo hayafikiki ikiwemo visiwa, lakini tunayo maeneo tunayoita Delta ni maeneo yenye majimaji hasa ukienda Ukanda wa Pwani, yako mengi sana, kuna vijiji vingi sana mpaka unapita kwenye Delta halafu ndiyo unafika kwenye hivyo vijiji.

"Lakini, pia tunayo maeneo ambayo kulingana na mkakati wa REA na mpango wa REA ni maeneo ambayo hatuwezi kufikia kwa miaka mitatu, minne, mitano ijayo sasa hatuwezi kukaa chini na kuacha wale wananchi wanakosa nishati kwa sababu ya mpangilio wa Serikali uliopo.

"Kwa hiyo lazima tutafute mbinu mbadala za kuhakikisha wale wananchi pia wanapata huduma ya umeme, ndiyo maana tukaja na miradi ya kusambaza umeme kwa kutumia nishati ya jua, hii miradi ilifanyika kuanzia mwaka 2012 mpaka leo bado inaendelea.

"Lakini, lengo kubwa tuliloanza nalo ni kupeleka kwenye shule za sekondari ambazo zipo kwenye hayo maeneo ambayo hayatafikiwa kwa wakati, lakini pia huduma za afya, vituo vya polisi pamoja na nyumba za walimu,"amesema Mhandisi Mwijage.

Vile vile anafafanua kuwa, miaka 10 iliyopita kila mwalimu aliyekuwa anapangiwa kwenda vijijini alikuwa baada ya miezi miwili au mitatu anahamia mjini kutokana na changamoto ya nishati ya umeme.

"Kwa hiyo, ilikuwa ni changamoto kubwa sana, lakini kama Serikali ikasema lazima twende na mkakati wa kuhakikisha nyumba hizi pia za walimu wanapata nishati ya umeme.

"Kwa hiyo ni miradi ambayo tumetekeleza na zaidi tuliangalia zile wilaya ambazo ziko chini sana ambapo tulikuja na wilaya kama tisa, ambazo zilibahatika kupata miundombinu ya umeme wa jua.

"Lakini, kwa sasa hivi kwa sababu mtandao mkubwa wa umeme umekwenda maeneo mengi ya nchi yetu, tumejikita sana kwenye maeneo ambayo ni ya visiwa, maeneo ambayo hatuna mpango wa kupeleka cable kwa maana ya kusambaza umeme wa gridi.

"Maeneo hayo ambayo tunayapatia nishati kwa kutumia tunasema gridi ndogondogo ambazo zinajengwa kwa nishati ya jua au kwa nishati ya ya upepo, na wananchi walioko maeneo yale wanapata huduma ya umeme."ameongeza Mhandisi Mwijage.

Amefafanua kuwa, kwa sasa katika visiwa 196 vilivyopo hapa nchini (Tanzania Bara) mpaka sasa kuna visiwa ambavyo havikaliki.

"Kuna visiwa ambavyo havikaliki, vinakalika kwa msimu wa kuvua ndiyo unakuta watu, lakini ule msimu ukishapita ni kwamba havina watu, kwa hiyo visiwa wa namna ile hauwezi kupeleka nishati ya umeme huko, ni visiwa 53 kati ya 196.

"Kwa hiyo visiwa vinavyobaki ambavyo ni takribani 143 visiwa 71 havina kabisa umeme, lakini visiwa 72 vimeguswa na huduma ya umeme kupitia aina mbalimbali ya ufadhili, kwa hiyo kwa sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika visiwa.

"Na, mpango wa sasa ni kuhakikisha hivyo visiwa vyote nilivyotaja 71 na vyenyewe vinafikiwa na huduma ya umeme,hapo kwenye hivyo visiwa, kuna visiwa ambavyo vina watu wengi, kwa mfano ukienda katika Kisiwa cha Koma unaweza kukuta zaidi ya kaya 5,000 kisiwa kimoja.

Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao kazi hicho kati ya REA, wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa uratibu wa ofisi hiyo ambapo amesema, vikao hivyo vina umuhimu mkubwa kwani vinaupa umma fursa ya kutambua taasisi na mashirika yao yalipotoka, yalipo, yanapoelekea na mafanikio yake kwa ustawi bora wa Taifa.

"Lakini, vipo visiwa watu wanakaa, lakini haizidi kaya 200 hadi 300, sasa sisi kama REA hatumiliki miradi, sisi siyo kama TANESCO, REA haimiliki miradi ila inawezesha ile miradi kufanyika.

"Aidha, kwa kutoa fedha, lakini pia kwa kutoa utaalamu elekezi kwa maana hiyo hii miradi ninayoisema ya Gridi Ndogo yote inamilikiwa na makampuni binafsi, kwa hiyo kazi kubwa ya Serikali ni kuyawezesha haya makampuni aina mbalimbali ya fedha tunazokuwa nazo ndani ya taasisi.

"Kuhakikiha ile huduma ambayo sisi kama Serikali hatuwezi kuipeleka leo, basi wenye tunawapa tuseme kama vitendea kazi, kuwawezesha kiuchumi ili waweze kufanya hiyo kazi.

"Kwa hiyo hiyo tumeifanya, na tunaendelea nayo, lengo letu kubwa ni kwamba tukifika 2025 vijiji vyote viwe vimepata umeme, sasa hatuongelei vya huku tu, lakini kuna wenzetu wavuvi ambao nao wanachangia uchumi mkubwa kwa ajili ya shughuli zao za uvuvi.

"Kwa hiyo lazima tuwawezeshe wawe na majokofu wahifahidi mazo yao ya bahari au yanayotoka kwenye maziwa tofauti tofauti ili waweze kufanya shughuli zao kwa urahisi na pia kutengeneza ajira katika maeneo yao."

Wakati huo huo, Mhandisi Mwijage amesema, Serikali kupitia REA imewapata waendelezaji watatu ambao ni Jumeme, Volt Africa na Green Leaf Technology wa miradi ya kusambaza umeme kwa kutumia nguvu ya jua, itakayotekelezwa katika visiwa 28 vilivyopo katika mikoa ya Kagera (8), Mwanza (13).

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya wahariri ambapo licha ya kuwapongeza REA kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuhakikisha nishati ya umeme inafika vijijini, pia amewashauri kuhakikisha hawapotei kwenye vyombo vya habari, angalau kila mwezi wawe na watu ambao watakwenda kushuhudia mafanikio yanayoendelea huko mikoani kwa ajili ya kuhabarisha umma.

Mikoa mingine ambayo miradi hiyo itatekelezwa ni Mara (3) na Lindi (4) na hivyo kuunganisha wateja 9,515 kwa gharama ya shilingi bilioni 11.18.

“Wakala unakamilisha taratibu za kusaini mkataba na Kampuni ya Jumeme wakati Kampuni za Volti Africa na Green Leaf Technology zikikamilisha taratibu za kimazingira kabla ya kuendelea na hatua ya kusaini mikataba."

Pia, amesema megwati 18 za umeme wa nishati jadidifu zimeunganishwa katika Gridi ya Taifa ikiwa i sawa na asilimia tano ya mchango katika gridi hiyo.

Katika hatua nyingine,REA imeanza kutekeleza mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000 yenye thamani ya shilingi bilioni 3 na mpaka sasa mitungi 42,000 imeshasambazwa.

Amesema, kwa mwaka wa fedha 2023/24 shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kusamabaza mitungi ya gesi ya kupikia na kwa sasa wakala umeshatangaza kwa ajili ya wasambazaji wa mitungi kuomba.

Mhandisi huyo akizungumzia, Mradi wa Kusambaza Gesi Asilia (CNG) amesema unajumuisha mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani (Pembezoni mwa Mkuza wa Bomba Kuu la Kusafirisha Gesi Asilia).

"Utekelezaji wa mradi huu utahusisha REA na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ukihusisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia (CNG),"

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni taasisi ya Serikali inayojitegemea ambayo ipo chini ya Wizara ya Nishati ikiwa na jumuku kubwa la kuhamasisha, kuratibu na kuwezesha uanzishwaji na uendelezaji wa miradi ya nishati vijiji

REA ilianzishwa kwa Sheria ya Nishati Vijijini Na.8 ya mwaka 2005 na kuanza kazi rasmi mwezi Oktoba 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa iliyokuwa Sera ya Nishati ya mwaka 2003.Aidha, Sheria ya Nishati Vijijini pamoja na kuanzisha wakala, pia imeanzisha Bodi ya Mfuko wa Nishati Vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news