Kenneth Simbaya awapa somo wanahabari nchini

NA FRESHA KINASA.

MKURUGENZI wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya amewataka Wanachama wa Klabu za Waandishi wa Habari wa mikoa yote nchini kuwa sehemu sahihi ya kuchangia maendeleo chanya ya klabu zao ikiwa ni pamoja na kuandika habari zinazoleta matokeo chanya kwa jamii.

Amesema, klabu ili zipige hatua wanachama wake Wanajukumu la kuandika habari ambazo zinathamani kwa jamii na ziwanufaishe Wananchi kwani taaluma yao ni muhimu sana kuwasemea wasio na sauti, badala ya kufanya kazi hiyo kwa mazoea.

Ameyasema hayo Novemba 23, 2023 wakati akifungua semina ya mafunzo ya kundi la pili kwa Waandishi wa Habari 28 wa Habari za 'Usawa wa Kijinsia' ambao ni wanachama wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini yanayofanyika Ukumbi wa Flomi Hotel mjini Morogoro yakiwa yameandaliwa na UTPC kwa udhamini wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania.

Katika mafunzo hayo, kila klabu imetuma mwandishi mmoja anayeandika habari za Kijinsia, huku mafunzo hayo yakiwa ni moja kati ya utekelezaji wa Mpango mkakati wa UTPC 2023-2025 uliobeba kauli mbiu ya 'Moving from good to Great'.

"Tunaweza kuongeza thamani ya kukuza taasisi kwa kufanya kazi ya Uandishi wa Habari unaoleta matokeo chanya kwa jamii. Klabu zetu tunapaswa kuziona zikipiga hatua kubwa na hatua haziji tu kirahisi, bali wanachama wake kutoa mchango chanya kwenye Klabu zao kwa kufanya uandishi ambao unamanufaa,"amesema Kenneth na kuongeza kuwa.

"UTPC haiwezi kukua bila Klabu zetu kukua na kuwa na matokeo makubwa. Klabu za Waandishi wa Habari zikituangusha UTPC imekufa, nimatumaini ya UTPC kuona Klabu zikipiga hatua kwa Wanachama kufanya kazi zenye matokeo kwa weledi unaotakiwa na kuachana na mazoea ya huko nyuma,"amesema Simbaya.

Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuitumia vyema fursa waliyoipata kwani ni wengi wameshindwa kupata na pia wawe sehemu muhimu ya kuandika habari za Usawa wa Kijinsia kwa ufanisi unaotakiwa na kuwa mabalozi wazuri wa kufanya jukumu hilo kikamilifu.

"Tushirikianeni kuisaidia UTPC kuleta matokeo, na hayo matokeo yataleta rasilimali kwa pamoja tutapiga hatua kwenda mbele, hapa katikati UTPC tuliona mambo hayakuwa sawa lakini kwa awamu hii tuonesheni mfano kwa matokeo ya kazi zenye ubora ambao zitaangalia maslahi mapana ya Jamii yetu." Amesema Kenneth.

Kwa upande wake Hilda Kileo Ofisa wa Progamu kutoka UTPC amesema kuwa, mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari namna ya kuandika habari zitakazowezesha kufanikisha malengo ya Maendeleo endelevu kwa Watanzania wote wanawake na wasichana kama ilivyoanishwa katika lengo la 5 la SDG's pamoja na kuhakikisha kuwa mipango ya Maendeleo ya Tanzania na SDG's zote 17 zinatekelezwa kwa kuzingatia Usawa wa Kijinsia.

Fresha Kinasa ni Mwandishi wa Habari na Mwanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari kutoka Mkoa wa Mara ameishukuru UTPC kwa kuandaa mafunzo hayo, amesema yatamsaidia kumpa uelewa mpana juu ya uandishi wa habari za Usawa wa Kijinsia kwa ubora utakaoleta matokeo chanya na mabadiliko.

Naye Severine Blasio mwanachama kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro ambaye anashiriki mafunzo hayo amesema kwamba " kupitia mafunzo haya nitaongeza uelewa juu ya masuala ya Jinsia na kuongeza uwezo wa uandishi wa habari za Kijinsia."amesema Blasio.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news