MPC:Akiba ya fedha za kigeni inatosha kuagiza bidhaa,huduma nje ya nchi kwa miezi minne

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imesema,akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha ikiwa ni takribani dola bilioni 5 kwa mwezi Novemba 2023, kiasi kinachotosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi kinachozidi miezi minne.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba leo Desemba 19,2023.

Amesema, hayo yalibainika baada ya kamati hiyo kufanya kikao chake cha 229 tarehe 18 Desemba 2023, kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi.

Vile vile anafafanua kuwa,thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani iliipungua kwa asilimia 7.8 kwa mwaka, hali inayoakisi upungufu wa fedha za kigeni nchini.

"Hata hivyo, akiba ya fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuwa ya kutosha,"amefafanua Mwenyekiti huyo.

Aidha, amesema Sekta ya fedha iliendelea kuwa thabiti. Sekta ya benki ilibaki imara ikiwa na mitaji ya kutosha na ubora wa rasilimali za benki ukiongezeka, kiwango cha mikopo chechefu kilipungua kufikia asilimia 5.3 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.2 mwezi Oktoba 2022.

"Kamati ya Sera ya fedha iliridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kukabiliana na uhaba wa fedha za kigeni nchini.

"Vilevile, utekelezaji wa sera zenye lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, unatarajiwa kuimarisha urari wa bidhaa, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, kuongeza akiba ya fedha za kigeni na hivyo kupelekea utulivu wa thamani ya Shilingi."

Kamati pia ilipongeza jitihada zilizochukuliwa na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya programu mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwa ni pamoja na yale yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF ya Extended Credit Facility (ECF).

Wakati huo huo, Kamati ilibaini na kupongeza hatua zillizofikiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kuhamia kwenye mfumo mpya wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha utakaoanza Januari 2024.

"Utekelezaji huu utalenga riba za muda mfupi katika soko la fedha badala ya fedha taslimu
(reserve money) katika kukabiliana na mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi."

Mfumo huu unatambulika kama Mfumo wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha unaotumia riba.

Kwa kuzingatia matarajio ya utulivu katika mfumuko wa bei na kuendelea kuimarika kwa
mazingira ya biashara nchini, Kamati iliridhia kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha
inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi mwezi Desemba 2023.

Aidha,maamuzi haya yalizingatia mwenendo usioridhisha katika uchumi wa dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news