Waziri Mkuu atoa maagizo uvunaji wa maji

DAR ES SALAAM-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji iongeze kasi katika uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua pamoja na kujengeni mabwawa ya kukinga maji ili yatumike wakati wa kiangazi, kwenye ukame na kuzuia mafuriko.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza viongozi wa Bodi za Maji wa Mabonde waongeze jitihada katika uhifadhi wa vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kutangaza maeneo hayo kwenye gazeti la Serikali kama maeneo tengefu ili kuyalinda kisheria.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Jumapili, Februari 11, 2024 baada ya kufungua Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Taifa la Sekta Mtambuka kuhusu Usimamizi na Uendeshaji wa Rasilimali za Maji katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Bodi za Maji za Mabonde zitekeleze agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti Rafiki wa Maji katika Vyanzo vya Maji nchini iliyofanyika Tarehe 16 Novemba 2022 kwa kupanda angalau miti rafiki wa maji milioni 2.5 kwa mwaka."

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini zijenge na kusafisha miundombinu ya kusafirisha ama kuondoa maji ya mvua katika maeneo yao ili kuzuia mafuriko. “Wizara ya Madini idhibiti uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji kuhimiza wachimbaji kuzingatia utunzaji wa mazingira.”

Kwa upande wa Wakala wa Misitu Tanzania, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wake wadhibiti upandaji wa miti mingi ya kibiashara katika vyanzo vya maji kwa kuwa miti ikikatwa eneo litabaki kuwa jangwa, piasuala hilo litekelezwe sambamba na kusitisha kutoa vibali vya kuvuna misitu kwenye vyanzo vya maji.

Awali, Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika ujednzi wa miradi wa maji, ambapo amesema ulindaji wa rasilimali za maji utaendelea kupewa kipaumbele nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde ambaye ameongea kwa niaba ya mawaziri wa kisekta amesema wataendelea kushirikiana kuhakikisha kwa pamoja wanazilinda rasilimali za maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news